Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kazini haonekani, yuko wapi huyu?

Hakuna asiyejua kwamba kitendo cha kumzushia kifo mtu yeyote ni kosa la kisheria. Mtu hasa akiwa kiongozi anapozushiwa jambo la namna hiyo, athari zake huwa kubwa kwa familia yake, viongozi wenzake na Taifa zima kwa jumla.

Kunaweza kukatokea taharuki na kutupiana maneno ya kutokuaminiana baina ya Serikali na wananchi. Hivyo kitendo hicho si cha kuungwa mkono na wazushaji hawana budi kutafutwa na kufikishwa kwenye vyombo vinavyohusika.

Watanzania wanaishi kidugu. Wanapomchagua mwenzao wanayemwamini kwenye nafasi ya uongozi, ni lazima wote watakuwa macho na usalama wa mtu huyo. Wanajua kwamba mti wenye matunda haukosi kurushiwa mawe, hivyo ni lazima kumkinga kiongozi wao dhidi ya mahasidi wachache waliojificha miongoni mwao. Mahasidi hawa wanaweza kuwa raia au viongozi wa ndani na hata nje ya Tanzania.

Bado Watanzania wangali wanashusha pumzi wakimshukuru Mungu baada ya pumzi zao kupanda pasi na yeyote kuzishusha. Kwa zaidi ya mwezi mmoja walikuwa wakiulizana alipo mpendwa wao, kiongozi namba mbili kwenye nchi, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango. Hakuwepo kutekeleza majukumu yake ofisini, hakuonekana kwenye ziara mikoani, hakuhudhuria misa kanisani, hakuwa amepumzika nyumbani wala hakukuwa na taarifa ya kulazwa hospitalini. Lakini baada ya siku 40 akajitokeza hadharani akiwa mzima wa afya.

Nakumbuka siku ile Mama ulimwambia Dk Mpango kwamba akiwa mtu wa watu ni lazima watu hao watahangaika kwa kutokuonekana kwake. Ni kweli ukiwa kipenzi cha watu uwe tayari kujibu maswali yao hata kama huyapendi. Mmoja atakuuliza ulikuwa wapi, mwingine mbona sijakuona kwenye sherehe yetu, au mbona sijakuona kanisani.

Hata kama watu hao wanaokupenda watakuwa wamekuwekea ulinzi wa kuaminika, wanahabari watakaoripoti mienendo yako na waangalizi wa afya yako, lakini hawataondoa umakini kwako kwa kuwa wao ndio waliosababisha vyote hivyo. Wanaamini kuwa baya lolote litakalokusibu, wao ndio watakuwa wahusika namba moja. Kwa hiyo wanajiweka kwenye nafasi ya mbele kukabiliana na majanga yako.

Ni kawaida ya mtu aliyekwisha kuumwa na nyoka kushtuka pale atakapoguswa na ujani. Historia inaonesha kutokea kwa hali kama hizo katika nyakati tofauti.

Walishawahi “kupotelewa” na wapendwa wao, wakahangaika kwa sababu ya kutokupata taarifa za moja kwa moja, wakahoji bila kurudishiwa majibu ya kuridhisha, na kwa bahati mbaya wakaja kupokea taarifa zisizopendeza huko mwishoni.

Ni kweli si lazima kuelezwa kila jambo kuhusu viongozi wao. Inawezekana kiongozi alikutana na vumbi wakati akiwa kazini kukagua miradi ya ujenzi, akabanwa na mafua makali yaliyomzuia kuingia ofisini kwa siku kadhaa.

Hali kama hii ni ya kawaida kwa binadamu, na inayotegemewa kurekebika baada ya muda mfupi. Si lazima watu waache shughuli zao na kuhofu juu ya afya ya kiongozi.

Serikali inao uwezo wa kuwatoa wasiwasi wananchi watakaoanzisha maswali. Hata ikisema ukweli kwamba anaumwa haitaleta taharuki. Lakini itakapoona kuwa kuna dalili za kuibuka kwa taharuki, Serikali hiyo inaweza kutumia mtindo wa “sema neno moja na roho yangu itapona”. Hata ikibidi kutumika kwa protokali za kisiasa, watu wataridhika kuliko kukausha kama vile hakuna kinachoendelea.

Hili si jambo geni. Kwenye familia zetu kunapotokea jambo kubwa la kushtusha, watoto hawaambiwi mapema.

Kama baba kasimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa kadhia yake, watoto wanaweza kuambiwa baba yupo likizo ya muda mfupi na wakaridhia. Jambo kubwa la kuzingatiwa ni kutobadilika kwa maisha ya kila siku pale nyumbani. Lakini kama baba huyo amekamatwa, huwezi kuwaambia watoto kuwa yupo likizo wakati hawamwoni nyumbani.

Kwa mawazo yangu, Serikali ndiyo huwa ina majibu sahihi. Kwa kawaida viongozi wakuu ni taasisi zenye idara zote muhimu kama afya, habari, ulinzi na kadhalika. Familia ya kiongozi inalazimika kuingia kwenye taasisi hiyo ikiwa ni sehemu muhimu ya kiongozi huyo. Kwa vyovyote kiongozi hataweza kufanya kazi kwa ustadi iwapo mmoja wa familia yake atakuwa kwenye matatizo.

Kiprotokali familia ya kiongozi haina nguvu ya kutoa majibu ya moja kwa moja kwa wananchi, labda itokee familia hiyo imekosa imani kwa Serikali yao. Lakini katika utaratibu wa kawaida; kiongozi, walinzi wake, madaktari na wanahabari wote kwa pamoja ni sehemu ya taasisi inayowajibika Serikalini.

Hivyo linapotokea la kutokea, taarifa zitawasilishwa Serikalini na kurudishwa kwenye familia. Serikali itashirikiana na familia kutoa majibu kwa wananchi.

Mwaka 1964, Mwalimu Nyerere alinusurika kwenye mapinduzi yaliyopangwa kummaliza. Hakukuwa na taarifa rasmi kwa umma za mahala alipojificha. Taifa liliingia kwenye hekaheka na hofu juu ya kiongozi wao.

Lakini askari waaminifu wakalizima jaribio hilo na taarifa ilitolewa kuwa Mwalimu alikuwa salama. Kumbe alifichwa nyumbani kwa raia mmoja wa kawaida.

Taarifa ya Mwalimu kuwa salama ingechelewa kutoka, wananchi wasingelikaa kimya na kuamini kwamba si lazima kujua kila kitu.

Kusingelikuwa na utulivu. Hii ndiyo maana ya kutoa taarifa kwa wakati, taarifa huwakusanya wananchi pamoja kuendelea na dira ya kiongozi wao hata kama haonekani machoni mwao.