Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KONA YA FYATU MFYATUZI: Bomoa mijengo yote ya Kalia Koo

Wapendwa mafyatu na mashabiki wangu, jongea ugani tudurusu na kujadili hii ishu kwa utuo na uzuri. Keibuni sana waghoshi na waghoshingwa woshe. Du, nimesahau hadi nikamwaga ung’eng’e utadhani wote ni wabritish!

Chapu chapu. Kwanza, natuma salamu za rambirambi kwa wahanga wa janga la kikaya la Kalia Koo. Pili, namshukuru mheshimiwa rahis kwa namna alivyolishughulikia balaa hili japo wapo machizi wanaomlaumu kuwa aliacha msiba na kwenda ughaibuni, wasijue yeye anaweza kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja bila kujali alipo, iwe ndani au ughaibuni.

Baada ya chimbuachimbua na kutofuata sheria kufanyika ili kuongeza ukubwa majumba ambayo yamesajiliwa kwa shughuli nyingine kujiingiza kwenye biashara isiyolipiwa kodi ya kuhifadhi bidhaa kuwafyatua mafyatu wasio na hatia, sirkal imesema kuwa inaweza kuangusha mijengo yote iliyojengwa kiholela ili kuepusha maafa.

Nina dazeni ya maswali. Kwanza, je, hii ni kweli na inawezekana? Pili, na kama inawezekana inawezekana vipi? Tatu, mbona wahusika hawatuambii miujiza watakayotenda kuondosha jinai hii? Nne, je, wahusika walikuwa wapi na kwa nini sasa? Tano, je, yapo mengine kama haya kiasi gani ambayo yanajulikana ila yanangoja kupewa maelezo na ahadi baada ya kufyatuliwa mafyatu maskini tena wasio na hatia?

Sita, je, nani alisababisha jinai hii kama siyo uholela wa muda mrefu? Saba, je, nani atawafidia wenye mijengo hii ambayo imefyatuliwa kimazabe? Nane, je, hili ndilo jibu na suluhu au siasa ili vumbi litue na mafyatu wasahau mambo yaendelee kama kawa?

Tisa, je, ipo mijengo mingapi ya mchongo kama hiyo inayongoja kudondoka, kudondokea na kuwafyatua mafyatu maskini wa kutengenezwa a.k.a kusikinishwa? Kumi, je, nani anapaswa kulaumu au kulaumiwa usawa huu? Kumi na moja, je, wahusika–kama kweli wapo, wote tunajua wapo – walikuwa wapi? Kumi na mbili, je, hii ndiyo suluhu la tatizo husika?

Nimesikia wengi wakimwaga michozi kwa kufyatuliwa wahanga wa kuporomoka kwa mjengo huko Kalia Koo. Wapo waliomwaga sifa kwa uokozi ulioonekana wazi kusuasua tokana na ukosefu wa zana. Wengine, walijitoa kimasomaso na kupiga siasa kwenye msiba ilimradi kila fyatu na lake.

Naongeza maswali. Mosi, je, ni michozi ya kweli au ya mamba? Pili, je, nini kifanyike badala ya kulialia na kutoa ahadi hewa na kufanya mambo kisiasa badala ya kuyafanya kisayansi? Tatu, je tatizo ni Kalia Koo tu au kaya nzima au Kalia Koo ni kielelezo cha uoza chungu nzima ambao tunaujua au kutoujua lakini tumeshindwa kuukabili?

Nne, je, tumefanya utafiti gani kujua ukubwa wa tatizo ili kulitafutia suluhu kisayansi na si kisiasa?

Tano, je, barabara na reli zetu ziko katika hali gani kuhusiana na uholela na hata uhujumu huu? Sita, je, ilikuwaje mafyatu wakajichukulia sheria mikononi na kuchimbuachimbua jengo kuongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa?

Saba, je, ni wangapi wameishafanya hivyo ili kujipatia kipato zaidi wasijue ni mtego wa panya unasao waliomo na wasiokuwemo? Nane, je, ni kuwananga au vibaya nao kuwalaumu kwa tamaa na ujinga wao? Tisa, kwa nini tusirejee utaratibu wa zamani ambapo ujenzi wa maghorofa ulikuwa ukisimamiwa barabara kuepuka majanga badala ya kujivunia majanga yanayongoja kutokea kwa kisingizio kuwa uchumi na utajiri vimekua kayani wakati ni majanga na mawenge yanayongojea kutokea.

Kumi, je, tumejifunza nini tokana na janga hili? Kumi na moja, je waliosababisha balaa hili wameishakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria? Kumi na mbili, je, wako wangapi hawajakamatwa hata kama wanajulikana?

Kwa walioona namna vyombo vyetu vya uokozi vilivyo apechealolo kwa upande wa zana za kuokolea, watakubaliana nami kuwa tuna matatizo mengi tu tena makubwa ya kujitakia. Unashangaa. Inakuwaje tunaweza kununua mashangingi na mashumbwengu kwa ajili ya wanene na kushindwa kununua zana za uokozi?

Nani ameona namna Kalia Koo ilivyojengwa hovyo kwa mbanano kiasi cha kukosa hata njia za kupumulia na kupitisha vikosi na zana za uokozi? Nisionekane mchochezi, naomba tujiulize pamoja. Je, zana za uokozi zinagharimu kiasi gani? Je, kati ya zana za uokozi zinazoweza kuwasaidia walio wengi na magari ya fahari ya walaji wachache ni nini kiwe kipaumbele chetu?

Leo tunaongelea kuporomoka kwa majengo. Nani anaona hatari ya moto inayongoja kutokea?

Nani anaona hatari ya kuziba mitaro ya kupitisha machafu inayongoja kutokea kiasi cha kufurisha mitaa yetu kama siyo nayo kuchangia kuporomoka kwa majengo mabovu yaliyojengwa holela na kwa viwango vya chini kutokana na tamaa, ubinafsi, ujinga, na rushwa na mifumo mibovu mbali na utamaduni wa hovyo wa kutopambana na waroho wachache wanaohatarisha usalama wa wengi?

Kwa vile nina majonzi ya kupoteza mafyatu wasio na hatia, leo sitachonga sana. Badala yake nahanikiza kuwa haki itendeke kwa wahanga. Wahusika au mifumo mibovu na ya kirushwa, ukiachia mbali tamaa na ujinga, waliosababisha janga hili wamekamatwa? Kama hawajakamatwa, ni kwa nini? Kama wamekamatwa, tutarajie nini kama kaya? Naona mhariri ananikodolea mimacho kuwa nimechonga sana. Si tuonane wiki ijayo.