Kurejea Lissu, Lema matunda ya maridhiano ya kisiasa

Muktasari:

Vikao vya maridhiano ya kisiasa pamoja na kuonyesha dalili ya mwelekeo mpya wa siasa nchini, pia vimejenga imani kwa wanasiasa, kurejea kwa viongozi wa upinzani waliokuwa uhamishoni ni kielelezo kimojawapo, Mwananchi Digital inachambua.


Dar es Salaam. Vikao vya maridhiano ya kisiasa pamoja na kuonyesha dalili ya mwelekeo mpya wa siasa nchini, pia vimejenga imani kwa wanasiasa, kurejea kwa viongozi wa upinzani waliokuwa uhamishoni ni kielelezo kimojawapo, Mwananchi Digital inachambua.

Katika kipindi cha miaka sita, wanasiasa watatu wa upinzani walikimbia nchi kwenda uhamishoni, kwa kile walichokieleza kuwa kumekuwa na matishio kadhaa ya usalama wao kwa sababu za kisiasa.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema na Mbunge wa zamani wa Rorya mkoani Mara, Ezekia Wenje ni miongoni mwa wanasiasa hao.

Tofauti na ilivyokuwa wakati huo, hatimaye sasa wanasiasa hao wanatarajia kurejea nchini na Lissu amethibitisha kulitekeleza hilo Januari 25, 2023.

Akizungumza wakati wa mkutano wake kwa njia ya mtandao akiwa nchini Ubelgiji leo Januari 13, Lissu amesema kurejea kwake na wenzake kutokana na wito wa Kamati kuu ya Chadema ili waje kushiriki moja kwa moja harakati za mapambano ya kidemokrasia.

“Kamati Kuu iliazimia, pamoja na mambo mengine, kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya kisiasa mimi na wenzangu ambao tumekuwa uhamishoni tangu mwisho wa Uchafuzi Mkuu wa 2020 turudi nyumbani, ili kushiriki moja kwa moja katika harakati za mapambano ya kidemokrasia tukiwa nchini,” amesema Lissu.

Hatua ya kurejea kwa wanasiasa hao ni matokeo ya juhudi kadhaa za maridhiano ya kisiasa zilizoanza Machi 4, 2022 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe Ikulu, Dar es Salaam.

Kukutana na kuzungumza kwao, kulifungua milango ya majadiliano kuelekea maridhiano ya kisiasa yaliyohusisha timu ya watu watano kutoka Chadema, kadhalika idadi kama hiyo kutoka CCM.

Mazungumzo baina ya pande hizo mbili yamelenga pamoja na mambo mengine kuanza mchakato wa Katiba Mpya, kufanya mabadiliko katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuruhusu mikutano ya siasa.

Matunda ya majadiliano hayo ni kuruhusiwa kwa mchakato wa Katiba Mpya na mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, mambo ambayo ndiyo haswa yanayowarejesha wanasiasa hao.