Lema aeleza sababu za kuiacha familia yake Canada

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema ametaja sababu ya kurudi Tanzania bila familia yake kuwa amekuja kuandaa mazingira.


Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema ametaja sababu ya kurudi Tanzania bila familia yake kuwa amekuja kuandaa mazingira.

Lema ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Machi 2, 2023 kupitia mahojiano maalum aliyofanya na Mwananchi Digital, amesema amekubaliana na familia yake kurudi kwa awamu.

Amesema kukimbia na watoto na mke ni jambo gumu lakini yeye akisikia anatafutwa inakua ni rahisi na kwamba kama familia wamekubaliana kurudi kwa awamu.

"Tumekubaliana turudi kwa awamu na mimi ndo nitangulie kuja kuweka mazingira mazuri, kuna vitu vingi vya kufanya na tulivyofika Canada mke wangu alianza shule na watoto pia, yule mkubwa anatarajia kuanza chuo kati ya mwezi wa saba au wa nane” amesema Lema

Lema amerejea nchini jana akitokea Canada alikokimbilia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, alipokelewa na wafuasi na wanachadema katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).