Lema azungumzia kauli ya Waziri Mkuu kuhusu utekaji
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Godbless Lema akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Dodoma. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Kauli za viongozi kuhusu masuala ya utekaji zimepingwa na makada wa Chadema kwa madai kuwa ni kivuli cha kujificha katika mpango unaolengwa mbeleni.
Dodoma. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mlezi wa chama hicho Kanda ya Kati, Godbless Lema amejibu kauli ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuhusu utekaji.
Lema alisema hayo kwenye mkutano wa hadharani jijini Dodoma jana Jumapili Mei 24, 2026 ambapo alieleza kuwa kauli ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ni kivuli cha kujificha katika mpango unaolengwa mbeleni.
Jana, akiwa mkoani Iringa, Waziri Mkuu alisema kuna matukio ya ajabu yanayotengenezwa kwa ajili ya kuichafua Serikali ikiwemo alichosema ni michezo, kama vile mtu kutekwa lakini akaonekana akiwa na pingu.
Lema alidai alifahamiana na Dk Mwigulu tangu alipokuwa waziri kivuli wa mambo ya ndani. Alidai Dk Mwigulu akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani yalitokea mauaji ikiwemo yale ya Kibiti na upoteaji wa Ben Saanane na wengine.
“Namfahamu Mwigulu (Dk Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu) ambaye mambo mengi yalitokea akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwemo waliopata madhila kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga ambako alikuwa mratibu wa kampeni za CCM,” alidai Lema.
Mbunge huyo wa zamani wa Arusha, alidai si haki Waziri Mkuu kutoa kauli za namna ile wakati kipindi Lissu alipigwa risasi, hakuwahi kusema nani aliondoa kamera za nyumbani alipokuwa akiishi.
Mahinyila apiga kijembe
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyika alisema wanaotaka kurudi ndani ya chama hicho wanakaribishwa isipokuwa hawatakiwi kufika na kwenda moja kwa moja.
Mahinyila alisema ni vema wanaorudi wabaki sebuleni kwanza kabla ya kuingia vyumbani.
Kauli ya Mahinyila imekuja siku moja baada ya aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini na mwenyekiti wa zamani wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa kutangaza kurudi Chadema baada ya kutoka CCM.
“Sisi vijana hatuzuii wenzetu wanaporudi, tunasema karibuni sana nyumbani, lakini mkifika tulieni sebuleni kwanza ili mpate kujua tuna nini kwenye chama,” alisema Mahinyila.
Mahinyila ambaye ni mwenyeji wa Dodoma, aliwataka vijana kutorudi nyumba katika kupigania haki na ardhi ya Dodoma.
Alisema awali kulikuwa na migogoro ya ardhi katika Jiji la Dodoma ilivyokuwa inazalishwa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) lakini akaeleza kuwa kwa sasa migogoro ya ardhi chini ya jiji ndiyo imekuwa mikubwa na mingi kuliko awali.
Sugu ashangiliwa
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi (Sugu) aliamsha shangwe katika mkutano wa wananchi na viongozi wa chama hicho jijini Dodoma.
Katika mkutano huo, Sugu alianza kwa kusema kilio chake ni kutaka haki na uhuru wa kufanya biashara ili kuzalisha ajira, siyo kutafuta ubunge.
Mshereheshaji alimuita Sugu na mara kelele za shangwe zikaibuka na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekaa mbali na jukwaa wote waanza kukimbia jukwaani huku wakipiga kelele kwa wimbo “Sugu, Sugu, Sugu”.
Hali hiyo imeendelea hivyo kwa dakika zaidi ya moja hadi Sugu mwenyewe alipowaomba watulie ili wasikilize hotuba za viongozi wa kitaifa.
Sugu alisema kilio cha viongozi wa Chadema siyo kutaka ubunge bali kuwe na haki ya kufanya uchaguzi na amani ili wafanye biashara.
Hata hivyo, Sugu alitumia muda mfupi kuliko wengine walioitwa jukwaani akiishambulia Tume ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025 kwamba taarifa yake kuhusu matukio na idadi ya vifo siyo sahihi.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob (Bon Yai) alisema watenda haki wanaishia jela lakini mafisadi wanadunda mtaani, akidai kuwa Lissu anasota gerezani kwa kutafuta haki wakati waliolisababishia hasara Taifa wanadunda mtaani.