Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lowassa wa CCM ndo yuleyule wa Chadema

Mama huku kwetu uswahilini kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukisumbuliwa na ugonjwa wa macho, almaarufu “red eyes”. Ugonjwa huu humfanya mtu ashindwe kabisa kufanya shughuli zake, kwani macho yanauma zaidi ya yaliyodondoshewa tindikali. Anapokutana na mwanga anahisi kichwa kutaka kubutuka, na anapoinama anahisi macho yakitaka kudondoka. Hakuna anayeombea janga hili limfike.

Pale alipoonekana mtu mwenye macho mekundu kama moto, kila mmoja alihangaika kivyake. Wapo waliotumia njia za kitaalamu kama kutokugusana naye, au ikitokea bahati mbaya basi kunawa mikono na uso kwa sabuni na maji tiririka. Wengine walitahadhari hata kupita karibu yake.

Lakini wengine walienda mbali zaidi kwa kukwepa hata kumtazama, ati kwa kuhofia maambukizi ya mawasiliano ya macho!

Hivi leo uswahilini tunahangaika zaidi maana kila mtu ana macho mekundu. Sasa ndio nagundua kuwa kwa zaidi ya wiki watu wamekuwa wakiomboleza kikwelikweli. Wengine walijikaza kisabuni mchana, lakini usiku wakalia vitandani mwao. Nilipofuatilia ndipo nilipoelewa uzito wa msiba uliolikumba Taifa baada ya kuondokewa na mtetezi, bingwa wa demokrasia ya kweli na maridhiano, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa.

Jambo hili linanipa fundisho kuwa walimwengu ni ndumilakuwili; wanaweza wakakupenda lakini wakakukanyagia, lakini wanaweza kukuchukia huku wakikukenulia tabasamu la mamba.

Leo hadi wana CCM na Chadema waliokuwa wakimnanga kwa majina mabaya wanalia mioyoni mwao, pengine na kumwomba Mungu msamaha kwa kuihukumu damu isiyo na hatia.

Binadamu tunao utamaduni wa kutokumsifia mtu anapofanya mazuri hata kwa mamia, kwa sababu tunaamini hivyo ndivyo anavyopaswa kufanya.

Lakini mtu huyo akikosea mara moja tu atashambuliwa kutoka kila upande. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa huko mitaani watu huwadunda wake zao kila kukicha, lakini hiyo si habari.

Ingetokea yeye akamchapa Mama Maria kofi moja tu, BBC na CNN wangekuja kupiga kambi nyumbani kwake.

Nimegundua pia wanasiasa wanaweza kukunjiana kisiasa tu.
Mioyoni mwao wanaelewa lipi lililo sahihi hata kama wanalikataa. Mwisho wa siku hawatakubali kama walikosea, ila itawaumiza sana. Wakati mwingine wanatamani zile karama za mwenzao zingelikuwa zao.

Hebu fikiria wangapi wametamani kusindikizwa na nyomi kama lile siku yao ya mwisho itakapofika.

Asilimia kubwa ya wanasiasa hawana utashi wa kusimama kwenye mstari mmoja. Hii inatokana na wananchi kugawanyika kwenye pande tofauti. Kwa kuwa watu ndio mtaji, wanasiasa nao hujiweka kwenye nafasi ya wavu wa samaki ili kuwanasa wote.

Lakini mzee wetu kwa kuwa alikuwa na mzuka wa Olaigwanani, alinyoosha mstari bila kujali mtaji wa kisiasa.

Mimi nina mawili yanayonifikirisha zaidi. Kwanza ni jinsi alivyojiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu bila kuisimika habari hiyo kuwa mtaji wake kisiasa.

Kila siku tunasikia huko duniani mbunge kakorofishana na Rais wake, kaanzisha chama kipya. Hapo siri zote anazijua yeye, na atazunguka nchi nzima kutafuta huruma ya wananchi na kujiongezea wafuasi. Huyo ni mbunge tu, vipi kama angelikuwa Waziri Mkuu!

La pili ni pale aliposimama kugombea urais kwa tiketi ya Chadema. Aliwavuta wapigakura wengi, wakiwemo viongozi wa CCM.

Wakati CCM wakitangazwa kuwa washindi, mahafidhina wa Chadema waligoma kwa madai kuwa walijumlisha kura za majimbo na kuuona ushindi wao.

Wakataka kuingia mtaani, lakini Lowassa aliwatuliza kwa maneno kuwa asingeweza kutawala akikanyaga damu za wahanga wa vurugu.

Pamoja na hayo, aliweka historia ya kuingiza wabunge na madiwani wengi kutoka upinzani kuliko kipindi chochote cha uchaguzi wa vyama vingi. Wakati huo ndipo tukaanza kuona wabunge wakishindana kwa hoja badala ya kupiga makofi kushangilia hoja yoyote iliyoletwa hapo.

Unyofu huu ni funzo kubwa kwa wanasiasa. Uongozi ni wito unaoambatana na vitu vingi sana, vikiwemo uzalendo, uwajibikaji wa dhati, utafutaji na utoaji wa haki, misimamo thabiti na kadhalika.

Viongozi wetu watambue kuwa baba anapaswa kuona aibu familia inapotetereka, hivyo nao hawana budi kuwajibika kwa dhati kwa ajili ya Taifa. Wananchi wanapolalamikia uzembe wa viongozi wao ni sawa na mtoto anapomlalamikia baba mzembe.

Inashangaza kumwona kiongozi wa Tanzania ya leo akiichukulia nchi yake kuwa shamba la bibi.

Anaiba fedha za walipakodi na kuzificha nje, wenye nchi tunaendelea kubaki makapuku.

Hivi sasa hawana hata haya, wala usishangae ukimsikia kiongozi mkubwa akitamba hadharani kuwa na mijengo Dubai na Marekani.

Hii inaleta picha mbaya sana kimataifa, kwani wanatuona sote hatuna akili.
Ni wakati wa viongozi kuwa wawazi. Wanyooshe misimamo yao kama alivyofanya mwenzao hadi tukamkubali katika kila upande aliosimama.

Watu walimtambua kwa utu wake na sio mdomo mtupu. Alipoona hakubaliani na mkubwa wake alimwambia, sio kama wafanyavyo sasa kuitikia na kupigia makofi hata mambo yenye ukakasi.

Wengine wanakitamani kiti chako hata kabla muhula haujaisha. Hivyo wanachekelea maovu ili wakukanyagie na kusema “Mi nilijua tu”. Hivi ndivyo wanasiasa uchwara wanavyotengeneza mitaji yao ya siasa.

Hakika si kila akwambiaye “Mama umeupiga mwingi” yupo pamoja nawe.
Ukimwona anaitikia kila kitu muulize alichoelewa, kama anazingua na wewe mzingue kabla jua halijachwa!