Mahakama yabariki Gachagua kufutwa kazi, kulipwa Sh1 bilioni
Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Katika uamuzi wa awali, mahakama imesema hakukuwa na ushahidi ulioonyesha kuwa kulikuwa na upendeleo, maamuzi yaliyopangwa mapema au mgongano wa kimasilahi katika mchakato wa kumtimua madarakani aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.
Nairobi. Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua na timu yake ya washauri wa kisiasa, wanatafakari hatua za kuchukua baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kuhalalisha mchakato wa kuondolewa kwake madarakani huku ikiamuru Seneti kumlipa fidia ya Ksh50 milioni (sawa Sh1 bilioni) kwa kukiuka haki yake ya kusikilizwa kwa usawa, wakati wa mchakato huo.
Katika uamuzi uliotolewa jana Jumatatu, Juni 7, 2026 na jopo la majaji watatu katika Mahakama za Milimani jijini Nairobi, mahakama ilibaini Seneti ilikiuka haki za Gachagua kwa kukataa kuahirisha vikao vya kesi yake ya kuondolewa madarakani, licha ya kuwasilisha taarifa kuwa alikuwa mgonjwa na hakuweza kushiriki kikamilifu katika mashauri hayo.
Hata hivyo, mahakama ilisema ukiukwaji huo haukuwa mkubwa kiasi cha kubatilisha uamuzi wa Bunge la Taifa na Seneti wa kumwondoa madarakani.
Uamuzi huo unaweka hitimisho muhimu katika moja ya mapambano makubwa ya kisiasa na kisheria kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya tangu kuanza kwa Serikali ya Rais William Ruto, huku ukimuachia Gachagua fursa ya kukata rufaa katika Mahakama za Juu.
Licha ya kupewa fidia, Gachagua alipata pigo baada ya mahakama kutupilia mbali hoja zake nyingi zilizolenga kuonyesha kuwa mchakato wa kuondolewa kwake ulikuwa na dosari za kikatiba.
Majaji walisisitiza Bunge la Taifa na Seneti zilitekeleza majukumu yao ya kikatiba ipasavyo katika kushughulikia hoja ya kumuondoa madarakani. Pia walikataa madai kuwa wabunge na maseneta walikuwa na upendeleo au walikuwa tayari wamefikia uamuzi kabla ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa dhidi yake.
Hukumu hiyo pia imeibua maswali kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Gachagua, hususan kuhusu nafasi yake katika siasa za upinzani na uwezekano wa kugombea nafasi za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Gachagua na chama chake cha Democracy for the Citizens Party (DCP) walikuwa na matumaini ya kupata ushindi ambao ungefuta kuondolewa kwake madarakani, na wakati huohuo kuimarisha nafasi yake kama mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani nchini humo.
Badala yake, kushindwa kwake mahakamani kunamlazimu kubadili mkakati na kuutumia uamuzi huo kama mtaji wa kisiasa kwa kuendelea kusisitiza madai yake ya muda mrefu kwamba amekuwa akilengwa kwa misingi ya kisiasa.
Mkakati huo unaweza kumsaidia kuimarisha uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wake, hasa katika maeneo ambayo amejijengea taswira ya mwanasiasa anayeadhibiwa kwa sababu ya kusema wazi anachoamini.
Kwa kuwasilisha kuondolewa kwake madarakani na changamoto zake za kisheria kama mateso ya kisiasa badala ya hatua za uwajibikaji, Gachagua anaweza kuongeza huruma ya wananchi na kujiweka kama mmoja wa vinara wa upinzani kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.
Hukumu hiyo imefungua njia kwa Profesa Kithure Kindiki kuendelea kuhudumu kama Naibu Rais wa Kenya.
Kesi hiyo ilijikita katika masuala saba makuu, ikiwamo iwapo maombi yaliyowasilishwa yalikuwa na msingi wa kisheria wa kusikilizwa mahakamani, kama kulikuwa na upendeleo katika mchakato wa kumwondoa, na iwapo wananchi walipata fursa ya kushiriki kikamilifu katika mchakato huo.
Masuala mengine yaliyopitiwa yalihusu uhalali wa baadhi ya kanuni za Bunge zilizopingwa, athari za kutokuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliyokamilika, pamoja na kama taratibu za kikatiba za kuondolewa madarakani na urithi wa madaraka zilifuatwa ipasavyo.
Mahakama pia ilichunguza iwapo Gachagua alipewa haki ya kusikilizwa kabla ya uamuzi wa mwisho kufikiwa.
Katika hoja hizo zote, walalamikaji walifanikiwa katika masuala mawili pekee; mamlaka ya mahakama kusikiliza shauri hilo na ukiukwaji wa haki ya kupata utawala wa haki unaozingatia taratibu za kisheria.
Majaji walisisitiza mchakato wa kumwondoa Naibu Rais madarakani hauko nje ya uchunguzi wa mahakama kwa sababu tu unahusisha masuala ya kisiasa.
Wakikataa hoja za Bunge la Taifa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mahakama ilisema Bunge hutekeleza mamlaka ya wananchi yaliyokabidhiwa kwake na Katiba, hivyo linaendelea kuwa chini ya usimamizi wa kikatiba.
“Hakuna chombo cha dola, ikiwamo Bunge, kilicho na kinga dhidi ya uchunguzi wa kikatiba,” walisema majaji.
Kuhusu madai kwamba wabunge na maseneta walikuwa tayari wameamua hatima ya Gachagua kabla ya kusikiliza mashauri yake, mahakama ilisema hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai hayo.
Kwa mujibu wa majaji, kuwa na msimamo wa kisiasa pekee hakutoshi kuthibitisha upendeleo usio wa kikatiba.
Mahakama pia ilisema Spika wa Bunge la Taifa na wa Seneti walikuwa na jukumu la kuratibu na kuendesha vikao pekee na hawakuwa waamuzi wa mwisho kwa kuwa hawakupiga kura kuhusu hoja ya kumwondoa Gachagua madarakani.
Katika suala la ushiriki wa umma, mahakama ilikataa madai kuwa wananchi walinyimwa fursa ya kushiriki katika mchakato huo.
Upande wa Gachagua ulidai wananchi walipewa chini ya saa 48 kupitia tuhuma zilizowasilishwa na kwamba takribani watu 200,000 pekee walishiriki kutoa maoni.
Hata hivyo, majaji walibaini kuwa Bunge la Taifa lilitoa taarifa kwa wakati kupitia vyombo vya habari na kuweka njia mbalimbali zilizowezesha wananchi kuwasilisha maoni yao.
“Katiba inahitaji ushiriki wa umma wenye maana, si ukamilifu,” walieleza majaji.
Vilevile, mahakama ilikataa hoja kwamba ushiriki wa umma ulikuwa wa lazima katika uteuzi na uidhinishaji wa Profesa Kindiki kuwa Naibu Rais.
Majaji walisema kuwa uidhinishaji wa mteule wa nafasi ya Naibu Rais hauhitaji ushiriki wa umma kwa kuwa Bunge hutekeleza mamlaka ya wananchi kwa niaba yao kama ilivyoelekezwa na Katiba.
Aidha, mahakama hiyo imesema hoja aliyowasilisha na Gachagua kwamba uteuzi wa Profesa Kindiki kuwa Naibu Rais haukukiuka Katiba ya Kenya.
Gachagua aliiambia mahakama kwamba Kindiki alikuwa anahudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Kitaifa na hakuwa amejiuzulu kazini alipoteuliwa na Rais William Ruto kuchukuwa nafasi ya Gachagua ambaye alikuwa ameondolewa madarakani na uamuzi wa Bunge la Seneti.
Uamuzi huo pia umesema kuwa ushirikishi wa umma uliofanywa na Bunge la Kitaifa ulizingatia katiba.
"Bunge la Seneti halikukiuka vifungu vya 10 wala 118 vya Katiba kwa kutofanya ushiriki wa umma ulio huru," mahakama imesema.
Mahakama ilibaini kuwa Bunge lilitoa ilani na kuhusisha ushirikishi kupitia vyanzo mbalimbali