Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makalla azusha tafrani, wadau wamkalia kooni

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla.

Muktasari:

  • Juzi, Makalla akizungumza na wanachama wa CCM mkoani Simiyu, alitoa shutuma dhidi ya viongozi wa Chadema, kuwa wamepanga kutumia fedha wanazochangisha kupitia kampeni yake ya Tone Tone, kununua virusi vya Ebola na Mpox kisha kuvisambaza nchini

Dar es Salaam. Kauli yenye tuhuma iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla imezusha sintofahamu huku wadau wakiwamo viongozi wa kisiasa wakimtaka ajitokeze kutoa ushahidi au aombe radhi.

Juzi, Makalla akizungumza na wanachama wa CCM mkoani Simiyu, alitoa shutuma dhidi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa wamepanga kutumia fedha wanazochangisha kupitia kampeni yake ya Tone Tone, kununua virusi vya Ebola na Mpox kisha kuvisambaza nchini.

"Hawa watu hasa viongozi waandamizi ambao familia zao hazipo Tanzania wanataka kutumia michango ya Tone Tone eti kufika wakati, wakanunue virusi vya Ebola na Mpox ili visambae Tanzania na uchaguzi usifanyike," amedai Makalla.

Makalla ambaye amewahi kuwa naibu waziri wa wizara mbalimbali na mkuu wa mkoa, amesema, "hili ni jambo la hatari, Chadema na wenyewe wapo watakaokufa kwa jambo hili, lakini wenzetu wengine hawana familia hapa Tanzania tushindane kwa hoja."

Kutokana na kauli hizo, Mwananchi imemtafuta Makalla jana Jumapili Machi 23, 2025 lakini jitihada hazikuzaa matunda.

Hata hivyo, wadau mbalimbali wamehoji kauli hizo huku wakimtaka kuthibitisha au kuomba radhi kwa kuzusha taharuki.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo za Makalla, amesema hawezi kumjibu kwa kuwa kufanya hivyo ni kumpa heshima asiyostahili.

"Kaka huo ujinga wa Amos Makalla nitaujibuje mimi, kumjibu ni kumpa heshima asiyostahili," amesema Lissu.

Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sabatho Nyamsenda amesema kauli hiyo ni hatari kwa siasa za Tanzania inayojiandaa kufanya uchaguzi wake baadaye mwaka huu.

"Hizo ni tuhuma nzito kutolewa na kama hilo ni kweli, viongozi wa Chadema wangepaswa kukamatwa na chama kufutiwa usajili, lakini hata Makalla mwenyewe anaonekana haiamini kauli yake," amesema Dk Nyamsenda.

Kwa uzito wa tuhuma hizo, Dk Nyamsenda amesema Makalla anapaswa atafutwe kuthibitisha kauli yake na kama hana uthibitisho anastahili hatua sio tu ndani ya chama chake, bali hata za kisheria.

Pia, ameichukulia kauli ya Makalla kama mbinu za CCM kuwakatisha tamaa Watanzania wanaoiunga mkono Chadema.

Kiongozi mstaafu wa ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kauli ya Makalla haina afya kwenye siasa za Tanzania na anapaswa kuomba radhi kwa umma.

Zitto amesema kauli hiyo ni hatari hasa wakati huu nchi ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu.

“Hii kauli ni ya hatari sana, sio kauli ya kiuenezi bali ni ya kinazi na anapaswa kuomba radhi haraka,” amesema Zitto.


Makalla alitaka kuchekesha umma-Cheyo

Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo amesema kama kweli Makalla ametamka kauli hiyo basi alitaka kuchekesha umma. ”Huyo alitaka tu kuchekesha,” amesema Cheyo bila kuongeza jambo lingine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Makini, Coaster Kibonde amesema kauli ya namna hiyo haikupaswa kutolewa na kiongozi mkubwa wa CCM bila kuwa na ushahidi.

“Kampeni ya Chadema inalenga chama kupata fedha ili kuendesha shughuli za kisiasa, sasa kama Makalla anajua kinachoendelea angeleta ushahidi mbele ya wananchi au wahusika wakamatwe,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa DP, Philipo Fumbo amesema kauli ya Makalla ni kauli sawa na zilizokosa mwelekeo.

“Anataka kuogopesha watu dhidi ya chama husika hakuna jambo lingine, kama ni kweli wangeshawakamata hizi propaganda zisizo na maana. Kauli kama hizi hazipaswi kutolewa na kiongozi, ambaye aliwahi kuhudumu Serikali na mkubwa anashangaza umma,” amesema.


Kubeba virusi ni kosa la ugaidi

Mtaalamu wa afya ya umma, Dk Ali Mzige amesema virusi vya magonjwa ambukizi vinaweza kubebwa sehemu moja kwenda kuhifadhiwa ili kama ugonjwa ule ukatokea, vile virusi vinaweza kwenda kutumika kutengeneza chanjo ya ugonjwa huo.

Ametolea mfano wa ugonjwa wa ndui, uliokuwa ukiitwa ‘small pox’, alisema kuna maabara mbili pekee duniani zimeruhusiwa kuhifadhi virusi vya 'small pox,' moja ipo Russia na nyingine ipo Marekani, hivyo kama ndui itatokea virusi vipo vinaweza kutengeneza chanjo ya ndui.

Amesema kuna uwezekano wa virusi kubebwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini kote duniani inatambulika ni kosa la ugaidi ‘Bioterrorism’ (Ugaidi wa kibayolojia ni ugaidi unaohusisha kutolewa kwa makusudi au usambazaji wa mawakala wa kibaiolojia. Wakala hawa ni pamoja na bakteria, virusi, wadudu, kuvu au sumu zao.

“Kama utabeba virusi kutoka nchi moja kwenda nyingine, utashtakiwa kwa kifungu bioterrorism kwamba hilo ni kosa la jinai kwa kuhamisha virusi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Ndiyo maana Shirika la Afya Duniani kuna kitu kinaitwa International Health Regulation, kwamba kitu ambacho kinapatikana kwenye nchi na hiyo nchi ina masharti gani ya kuzuia, ndiyo maana magonjwa yote lazima yaripotiwe WHO kwa ajili ya kumbukumbu na ufuatiliaji,” amesema Dk Mzige.

Amesema mtu anaweza kutumia hao wadudu kuua watu wengine, ambao ni usaliti wa hali ya juu unaoitwa 'bioterrorism' na mhusika akijulikana, hushtakiwa na adhabu ya kifungo.

“Ndiyo maana mtu akiwa na virusi lazima atibiwe mpaka apone, baada ya siku 42 kama hakuna kisa kingine, tunasema hakuna tena virusi yaani vimedhibitiwa. Tanzania ni moja ya nchi wanachama wa WHO na hata kama kuna vita na machafuko lazima watu waingie wachanje sababu usipofanya hivyo watakufa,” amesema.

Dk Mzige amesema kosa hilo linashtakiwa Mahakama za kimataifa au nchi husika.

Kwa mara ya mwisho, Ugonjwa wa Ebola umeripotiwa nchini Uganda baada ya Wizara ya Afya ya nchi hiyo, kuthibitisha mlipuko wa ugonjwa wa virusi hivyo ‘Sudan Ebola Virus Disease’ (SVD) jijini Kampala baada ya sampuli kuthibitishwa na maabara tatu za kitaifa.


Ebola Afrika Mashariki

Ugonjwa wa Ebola umeendelea kuwa tishio Afrika Mashariki, huku Uganda ikishuhudia milipuko kadhaa katika miaka ya nyuma.

Aina ya 'Sudan Ebola Virus' inatofautiana na aina ya Zaire, ikiwa na kiwango cha juu cha vifo na kwa sasa haina chanjo iliyoidhinishwa.

Mlipuko wa karibuni nchini Uganda ulitokea mwaka wa 2022 na kusababisha hatua kubwa za afya ya umma kuchukuliwa.