Mapokezi ya Mbowe Musoma

Muktasari:

Msafara wa viongozi wa Chadema ukiongozwa na mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho,  Freeman Mbowe umelazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 8 kuja mjini Musoma kwenye eneo la uzinduzi wa mkutano wa hadhara.

Musoma. Msafara wa viongozi wa Chadema ukiongozwa na mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho,  Freeman Mbowe umelazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 8 kuja mjini Musoma kwenye eneo la uzinduzi wa mkutano wa hadhara.

Msafara huo umeanzia katika eneo la Bweri nje kidogo ya mji wa Musoma na unatarajiwa kufikia tamati kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo ambapo ndipo kunatarajiwa kufanyika uzinduzi wa mikutano ya hadhara kwa kanda ya Serengeti.

Akizungumza katika msafara huo leo Jumapili Januari 22, 2023 Mwenyekiti wa baraza la wazee mkoa wa Mara, Charles Kayere amesema wanachama wa chama hicho wamelazimika kuanza matembezi hayo kuanzia Bweri.

Wakati msafara huo ukisubiriwa kufika uwanjani jeshi la polisi limeimarisha ulinzi ambapo mbali na askari kuonekana maeneo tofauti ya uwanja lakini pia barabara ya Nyerere kwa upande wa mjini imefungwa kwa ajili ya usalama.

Barabara hiyo imefungwa hivyo kulazimu magari yanayotoka au kuingia mjini kupita barabara ya Mukendo ambapo kwa sasa waenda kwa miguu, pikipiki na baiskeli pekee ndizo zinazoruhusiwa kutumia barabara hiyo kwa upande wa mjini.