Mbowe achaguliwa bosi Vyama vya Demokrasia Afrika

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amechaguliwa kuwa mwenyekiti mwenza wa umoja wa vyama vya kidemokrasia katika bara la Afrika.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amechaguliwa kuw Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Vyama vya Demokrasia Afrika (DUA), katika mkutano mkutano mkuu wa umoja huo uliofanyika jana Novemba 9.


Taarifa iliyotolewa na Chadema jana Novemba 9, 2022 imeeleza kuwa Mbowe alichaguliwa katika mkutano mkuu wa vyama vya kidemokrasia uliofanyika Jijini Abidjan Ivory Coast ulioanza Novemba 6 mwaka huu.


Taarifa hiyo imesema katika mkutano huo, Louisa Atta - Agyemang wa chama tawala cha Ghana, NPP naye amechaguliwa kuwa mwenyekiti mwenza atakayesaidiana na Mbowe ili kuleta mageuzi ya kimfumo na utendaji ndani ya DUA, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya vyama ya mrengo wa kati Afrika.


"Mkutano mkuu wa DUA umeamua kuwa na wenyeviti wenza wawili ili kurahisisha utendaji na ufuatiliaji wa mkakati wa kueneza itikadi ya mrengo wa kati barani Afrika," imeeeleza taarifa.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wenyeviti wenza wataongoza bodi ya watu nane itakayojumuisha makamu wenyeviti kutoka kanda tano za Afrika ambazo ni kaskazini, (Morocco), magharibi (Togo na Nigeria), kati (Equatorial Guinea), mashariki (Kenya) na kusini (Malawi).


Kikao cha kwanza cha bodi ya DUA kilichongozwa na Mbowe kimeamua kuhamisha makao makuu ya sekretarieti ya umoja huo kutoka Ghana kwenda Afrika ya Kusini.


Kwa hatua hiyo Mbowe atakuwa mmoja wa makamu wenyeviti wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU), kutoka Afrika.