Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbowe amlipua Silinde kwa usaliti

Wafuasi wa Chadema wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Tunduma jana. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

  • Ajibu akisema hoja zinazoibuliwa ni za kuwapa moyo wananchi

Tunduma/Dar. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemtaka Mbunge wa Tunduma (CCM), David Silinde kwenda kanisani kuomba radhi kutokana na dhambi ya usaliti aliyoifanya ndani ya chama hicho.

Silinde ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), aliwahi kuwa mbunge wa Momba mkoani Songwe kwa tiketi ya Chadema, kabla ya kufukuzwa na kwenda CCM, Julai 2020.

Akihutubia mkutano wa hadhara jana uliofanyika Tunduma, Mbowe alisema Tunduma ni moja ya maeneo yaliyoteswa kipindi cha miaka mitano na robo iliyopita kama ambavyo yeye alivyopitia gerezani.

“Natambua wako wana Tunduma 70 wamepita magerezani, lakini sisi angalau tuko hai, maana kuna wengine waliopotea ikiwemo wasaidizi wetu.

“Wako waliouawa na wengine walipigwa risasi, namwambia mdogo wangu Silinde ulikubalije kwenda kuwa kiongozi wa damu ya wana Chadema,” alihoji Mbowe.

Hata hivyo, Mbowe kabla ya kuwapandisha jukwaani wanachama waliowahi kwende gerezani kipindi hicho na kuwapa pole, alinukuu maandiko kwenye Biblia;

“Ndugu zangu wa Tunduma naomba mnisikilize huyu kijana Silinde nilimpokea Chadema mtoto mdogo yuko chuo kikuu, tukamfundisha siasa mwaka 2008, tukamleta Tunduma na kumnunulia nguo na viatu,” alisema.

Alisema kipindi hicho hakuwa na nguo hata za kumwezesha kupiga picha na viongozi huku akimfananisha Yuda Iskarioti aliyemsaliti Yesu.

“Huyu Silinde alisaliti ndugu zake waliomleta waliomlea, akasaliti wana Tunduma na wana Chadema, akasaliti na mageuzi akijua CCM ni Mungu akisahau chama hiki kimeanza na Mungu na kinamaliza na Mungu,” alisema.

Alimkanya Silinde akidai usaliti alioufanyia Chadema hautamuacha salama na kwamba wao ni Wakristo, hivyo wanamuomba akafanye toba kwa kufanya ibada na kuwaomba msamaha wana Tunduma.

Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Mwananchi lilimtafuta Silinde kuhusu tuhuma hizo na akasema wakati anajiunga na chama hicho ilikuwa hiyari yake na hata alipoamua kuondoka ilikuwa ni hiyari yake baada ya kuondolewa.

Alisema hoja alizotuhumiwa ni za kisiasa za kuwapa moyo wananchi huku akiwataka kujenga hoja na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mikutano ya hadhara nchini.

Awali katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mchugaji Peter Msigwa alisema Tanzania inapoteza Sh35 bilioni kwa mwezi kwenye mipaka yake yote kwa sababu ya miumdombinu mibovu.

Alisema takwimu zinaonyesha mpaka wa Tunduma kwa siku unapitisha magari ya mafuta 120, kama miundombinu ingeboreshwa yangepita magari 240.

“Takwimu zinaonyesha malori yanapita 80 kwa siku na kama miundombinu ingeboreshwa malori yatapita 280, kama mizigo hii ingepita ingeongeza kipato,”alisema Msigwa.

Alisema Serikali inapata Sh264 bilioni kwa mwaka pamoja na ubovu huo, Tunduma malori yamejaa yanazuia mzunguko wa fedha, walioko madarakani wameshindwa kufikiri na kutengeneza miundombinu ambayo itasababisha malori yaende haraka.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Catherine Ruge aliitaka Serikali kuona namna ya kurudisha upya mezani muswada wa Bima ya Afya kwa wote na kuboresha changamoto zilizopo, ili kukidhi matakwa ya wananchi.

Stephano Simbeye (Tunduma), Fortune Francis na Tuzo Mapunda (Dar)