Mbowe asikitishwa na wanaobeza maridhiano CCM, Chadema

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwasalimia wakazi wa mkoa wa Mwanza wakati wa maandamano yake kuelekea katika uwanja wa Furahisha kuzindua mkutano wa hadhara wa chama hicho kanda ya Victoria. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewashangaa waliombeza wakati akifanya maridhiano na Rais Samia Suluhu Hassan, akisema ni machungu makubwa aliyoyapata tangu aanze kutumikia chama hicho kwa miaka 30.

Mwanza. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameeleza kusikitishwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho kumfikiria kuwa anasaliti Watanzania kwa kufanya maridhiano ya kisiasa na CCM.

 Akizungumza na wananchi leo Jumamosi Januari 21, 2023 wakati wa ufunguzi wa mikutano ya hadhara ya chama hicho, Mbowe amemshukuru Rais Samia kwa kukubali maridhiano na hoja za Chadema.

“Yawezekana baadhi yetu msinielewe, namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan nimekaa naye kwenye vikao vingi vya kutafuta maridhiano.

“Yawezekana miongoni mwenu akanyanyuka yeyote kunikebehi, hatanipindisha msimamo wangu kwa sababu nachokisimamia kwa niaba ya nafsi yangu binafsi na kwa niaba ya Taifa hili, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.

“Madam President alisimama kuiunga mkono hoja ya Chadema alafu nakutana na wanachama wa Chadema wanamuona alikosea, this is madness (huu ni uendawazimu),” amesema.

Amesema hatowafurahisha watu wanaotaka amtukane Rais Samia akisema kwa neno la kiingereza “I will never do that!”

Chadema yakiwasha Mwanza, Mbowe achukizwa 'kulamba asali'

Amesema wakati wanachama wakiona ugumu upande wa CCM kulikuwa na ugumu kuliko upande wa Chadema kwa sababu walijua maridhiano yoyote ya kisiasa wanakwenda kuiua na kuidumaza CCM.

“Nyinyi badala ya kunipongeza Mbowe mnakuja na mawazo ya kiharamia, Mbowe karamba asali hataki Katiba mpya hataki tume huru,” amesema.

Amesema walipoanza mazungumzo ya maridhiano moja ya misingi waliyokubaliana kuwa msingi wa mazungumzo hayo ni usiri, hivyo hata vuongozi wa Chadema walimuona akiingia na kutoka Ikulu bila kutambua kinachoendelea.

Pamoja na kumpongeza Rais, Mbowe amesema hataacha kuikosoa Serikali yake na maridhiano yao hayamaanishi vyama hivyo vitaungana bali Chadema itaendelea kuwa chama kikuu cha upinzani nchini na baadaye kuwa chama tawala.