Mbowe awapa mbinu za ushindi Chadema

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesema kuwa endapo uchaguzi ujao utakuwa huru na haki basi chama hicho kitapata ushindi wa kishindo

Serengeti. Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesema kuwa endapo uchaguzi ujao utakuwa huru na haki basi chama hicho kitapata ushindi wa kishindo mapema.

Ameyasema hayo leo Machi 15, 2023 mjini Mugumu wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara.

"Nasema hivi tukienda kwa haki kabisa yaani hawa CCM tunawapiga mapema sana kabla ya misa ya kwanza kuisha," amesema.

Amesema kuwa chama chake ndicho chama pkee cha uponzani kilichobakia na chenye nia ya kweli ya kupambania haki ya wananchi na kuwaondoa katika lindi la umasikini.

Mbowe amesema kuwa ili chama hicho kiweze kupata ushindi huo lazima mambo kadhaa yafanyike ikiwepo mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi pamoja na tume huru ya uchaguzi.

Ameongeza kuwa pamoja na mambo yote watanzania wanatakiwa kukiunga mkono chama hicho katika harakati zake za kudai ukombozi wa nchi bila kujali itikadi zao za vyama.

"Huu sio muda wa kulalamika fanyeni maamuzi kama walivyofanya wenzetu wa Kenya, walijitambua wakajua matatizo yao yanasababishwa na nini wakaamua kuyakataa nadhani mnawafuatilia," amesema.