Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mjadala wa Majaliwa usiwe kichaka kuficha udhaifu Ajali ya precision

Muktasari:

Novemba 6, 2022, ndege ya kampuni ya Precision Air, PW 494, ilianguka Ziwa Victoria. Watu 19 walipoteza maisha, 24 waliokolewa. Shukurani kwa kijana Majaliwa Jackson na wavuvi wengine waliosaidia uokoaji.

Novemba 6, 2022, ndege ya kampuni ya Precision Air, PW 494, ilianguka Ziwa Victoria. Watu 19 walipoteza maisha, 24 waliokolewa. Shukurani kwa kijana Majaliwa Jackson na wavuvi wengine waliosaidia uokoaji.

Tangu kutokea kwa ajali hiyo Majaliwa amekuwa mada pendwa, hasa kwenye mitandao ya kijamii. Hata bungeni alifika. Mitaani watu wanapiga naye picha. Nasikia warembo kwa wingi wanaomba namba yake ya simu.

Acha watu wapige naye picha. Kazi aliyoifanya si ndogo. Si vibaya kumjadili, anastahili kujadiliwa. Tena isiwe yeye peke yake, bali na wavuvi wote ambao walipiga kasia Ziwa Victoria kuifuata ndege ilipo na kufanikiwa kuokoa watu 24.

Majaliwa ni shujaa, hili halipingiki. Kuvaa moyo wa ujasiri kuingia majini. Kupambana kuupiga mlango wa ndege kwa kasia baada ya kugundua waliopo ndani walikuwa wakijaribu kuufungua bila mafanikio. Mpaka kufanikiwa kuufungua. Ni ushujaa.

Chambilecho aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, kila mtu huhitaji bingwa wa kumvusha mahali. Watu 24 waliookolewa kwenye ndege ya Precision, Majaliwa ni bingwa wao. Bila kuwaweka kando wavuvi wengine.

Mambo yamekuwa mengi, siasa na harakati. Sio mbaya, ila makosa ni kwamba inakuwa rahisi kusahau kuwa jina la Majaliwa limeibuka kwa sababu kuna watu hawakutimiza wajibu wao.

Kusahau huko ndiko kunafanya ifike mahali ionekane kuna mvutano kati ya watu wanaounga mkono Majaliwa kupewa sifa, huku wengine wakiponda, wakiona kijana huyo ametengenezwa.

Mathalan, aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, alisema kuwa alipokuwa Mwanza, alizungumza na watu wawili walionusurika kwenye ajali ya Precision. Na wote walisema aliyefungua mlango ni mhudumu wa kike wa ndege.

Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alimjibu Sugu Tweeter kwa kuandika: “Majaliwa ni mkakati wa TISS kuondoa fikra katika uzembe wa uokoaji. Chukua kasia vunja mlango wa ndege ikiwa airport wacha kwenye maji, nakupa Sh10 milioni. Tafuta wakili Mangi nikupe hela ukiweza.”

Alichokisema Sugu ni maelezo kuwa walionusurika wanaamini aliyewafungulia mlango ni mhudumu wa ndege. Lema akaja kushusha tuhuma kwamba Majaliwa ametengenezwa kuficha kasoro za uokoaji.

Kwa akili ya kawaida tu, ushujaa wa Majaliwa ni matokeo ya kufeli kwa vyombo vya uokoaji. Sasa iweje Majaliwa aibuliwe na asifiwe, ili kufunika uzembe wa idara ya uokoaji? Wakati sifa za Majaliwa ni kipimo cha udhaifu wa mifumo ya uokoji.

Mtu mwenye fikra nzuri atauliza, kama lengo la Serikali ni kufukia uzembe wa idara ya uokoaji, mbona ingekuwa rahisi kumtambulisha Majaliwa kama kijana wa idara ya uokoji? Kisha wangempongeza na kutangaza kumpandisha cheo.

Majaliwa anasifiwa kwa sababu ni raia wa kawaida. Motisha ya fedha ambazo alipewa pamoja na fursa ya kujiunga na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ni kielelezo cha shukurani za Serikali. Vivyo hivyo, kukiri kuwa wahusika hawakufanya kazi yao.

Tujadili mlango

Maelezo ambayo Majaliwa aliyatoa siku ya kwanza ni kuwa alipoifikia ndege alikuta watu ndani ya ndege wakijaribu kufungua mlango bila mafanikio. Alichokifanya ni kujiongeza kwa kuupiga na kasia. Ukafunguka.

Mtu mwenye kuwaza vizuri atajua kuwa ndani mlango ulikuwa umeshaondolewa komeo zake, tatizo ukawa hauachii. Si kitu cha ajabu. Milango ya ndege haikutengenezwa kufungukia kwenye maji.

Milango ya ndege matumizi yake ni pale inapokuwa imeshatua tu. Kuna milango hufanya kazi kwa njia ya umeme, mingine kwa komeo za ndani na nje. Kuna ndege nimewahi kupanda, baada ya kutua, mlango ukafunguliwa kwa nje ndio abiria tukatoka.

Pamoja na kwamba milango ya ndege huundwa kwa kuzingatia usalama angani, kuna nyakati hufunguka yenyewe. Mwaka 2020, ndege ya Shirika la Pakistan International Airlines ATR 42, mlango wake ulifunguka wenyewe wakati ndege ikitua. Bahati nzuri hakukuwa na madhara. Ilifanikiwa kutua salama.

Machi 2021, ndege ya DHL Boeing 757, mlango wake wa mizigo ulifunguka ikiwa angani. Bahati njema pia ilitua salama. Hakukuwa na wafanyakazi waliojeruhiwa. Hivyo, kama mlango wa ndege unaweza kufunguka wenyewe angani, utashangaa kweli kufunguka baada ya Majaliwa kuugonga kasia, tena ukiwa umeondolewa komeo?

Mwaka 2019, ndege nyingine ya Pakistan International Airlines namba PK-702, Boeing 777, iliyokuwa ikisafiri kutoka Manchester, Uingereza kwenda Islamabad, Pakistan, ikiwa imeshafika kwenye eneo la kurukia (runway), abiria wa kike, alifungua mlango wa kutokea akidhani ni wa bafuni. Ilibidi abiria watolewe haraka kwa njia ya dharua (evacuation chute).

Ni mfano mwingine kuwa milango ya ndege inaweza kufunguka kwa urahisi. Hivyo, mjadala haupaswi kuwa Majaliwa aliongopa. Inaweza kurudisha nyuma wengine wenye moyo wa kujitolea. Maana mwishoni jitihada zao hutafsiriwa ni uongo. Pili, ni kujivunjia heshima.

Mathalan, Majaliwa, familia yake na wavuvi wengine, wanapoona kiongozi ambaye pengine awali walimheshimu, akisema kijana huyo alitengenezwa kimkakati, wakati sio kweli, je, wataendelea kumheshimu vilevile?

Ni ushauri kwa viongozi, kujiepusha na kutuhumu bila ushahidi. Hupunguza sifa na heshima. Huwajengea kutoaminika. Muhimu zaidi, viongozi wajiepushe kuchangia mada mitandaoni mithili ya wajenga ushawishi mitandaoni (social media influencers).

Kama kiongozi anaona influencers wa mitandaoni wanafaidi, aache uongozi. Kuna maneno akizungumza influencer hatashangaza. Maneno hayo hayo yakitamkwa na kiongozi, umma unabaki vinywa wazi.

Usahihi wa mjadala

Kwa mkazo, Majaliwa ajadiliwe. Hata hivyo, mijadala yenye afya kuhusu Majaliwa ilenge kutoa hamasa kwa vijana wengine zaidi kuwa na moyo wa kusaidia wengine.

Tupo kwenye ulimwengu ambao watu wanaweza kushuhudia ajali mbele ya macho yao, hatua tatu za mguu na wasitoe msaada. Wengine huondoka eneo la tukio. Wapo ambao huona kusaidia ni hatari kwao. Wasisahaulike wale wa kugeuza ajali fursa. Wezi!

Majaliwa aliingia ziwani. Akawa wa kwanza kuifikia ndege. Akasaidia kufungua mlango uliokuwa umegoma. Akasaidiana na wavuvu kuokoa watu 24. Akapata ajali ya kupigwa na mpira kichwani alipokuwa akiifunga ndege, ili waivute nchi kavu, waendelee kufanya uokoaji. Akazimia. Akazinduka hospitali.

Majaliwa anatakiwa ajadiliwe kwa namna ya kujenga hamasa kwa vijana wengine. Wakiona msaada unahitajika, watoke kwa moyo mmoja wasaidie wenye ujitaji. Hutokea kujitoa kwako kusaidia huambatana na neema. Kama Majaliwa!

Hata hivyo, mjadala wa Majaliwa kwa namna yake unapaswa kuwa sehemu “B”. Maana anajadiliwa kwa sababu ajali ilitokea. Vilevile waokoaji hawakufika eneo la tukio kwa wakati.

Sehemu “A” ya mjadala inatakiwa iwe kwa nini ajali ilitokea na mazingira yake, kisha ilikuwaje watu wa uokoaji na vifaa vyao hawakuonekana kipindi ambacho walihitajika mno?

Serikali inatenga bajeti kwa ajili ya uokoaji. Watu wanalipwa mishahara kwa ajili ya kazi hiyo. Siku ya uokoaji hawaonekani. Kwa nini? Ndege imeanguka kwenye maji jirani kabisa na uwanja. Watu wa uokoaji Uwanja wa Ndege Bukoba walikuwa wapi?

Viongozi wanapaswa kujielekeza kwenye masuala ya msingi. Sio kujadili vitu vyepesi mithili ya influencers wa mitandaoni. Taifa lazima liambiwe nini kilitokea kwa uzembe mkubwa kama ule wa watu 19 kufa ilhali ndege ilianguka majini jirani na uwanja?

Ingekuwa ndege ilianguka porini pengine lawama zingepungua. Au majini lakini mbali na uwanja wa ndege. Kungekuwa na kujitetea. Tatizo ilizama majini jirani na Uwanja wa Ndege Bukoba. Na inafahamika kila kiwanja kuna watu wa uokoaji. Taifa linahitaji maelezo.

Jinsi uongozi wa Uwanja wa Ndege Bukoba na Jeshi la Uokoaji wanavyokaa kimya, inashangaza mno. Hapa ndipo palipo na upande mmoja wa sehemu A ya mjadala. Mkazo uwe hapo.

Upande wa pili wa sehemu A ni kiini cha ajali. Mkurugenzi wa Utabiri, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Hamza Kabelwa alisema kuwa walitoa tahadhari siku moja kabla kuhusu hali ya hewa ya Kagera kuwa ingekuwa na mvua, mawingu na ukungu.

Katibu Mkuu-Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Gabriel Migire, alisema kuwa hali ya hewa ilikuwa mbaya, ukungu ulikuwa mkubwa, hivyo rubani aliweza kuona mbele kwa kilomita mbili wakati kwa uhalisia hupaswa aone si chini ya kilomita 10.

Chukua maelezo ya Kabelwa, ni kwamba TMA walishatabiri. Ufafanuzi wa Migire unaonyesha kuwa kilichotabiriwa na TMA ndicho kilitokea. Kwa maana hiyo, kama Precision Air wangezingatia ushauri wa kitaalamu, wasingepeleka ndege Bukoba, asubuhi ya Novemba 6, 2022.

Hili linaigusa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Mamla ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). TCAA kupitia taarifa ya TMA, wangezuia ndege kuingia na kutoka anga ya Kagera mpaka pale hali ingetulia. TAA wangekataza utuaji na upaaji wa ndege Uwanja wa Ndege Bukoba.

Inahusu pia uongozi wa Uwanja wa Ndege Bukoba. Kwa nini mamlaka zote hizo zilikaa kimya na kusababisha ndege iingie majini? Watu 19 wakapoteza maisha? Mjadala na shikizo viwe eneo hili. Majaliwa ni matokeo. Ni sehemu B.

Uwanja wa Ndege Bukoba ni mdogo. Barabara ya kutua na kurukia ndege ni fupi. Haina taa. Ilishaamuliwa ujengwe uwanja mwingine mkubwa na salama eneo la Omukanjunguti. Rais John Magufuli alikataa. Kwa nini alikataa? Mbona Uwanja wa Chato ulijengwa haraka? Tujadili hapa. Ndipo kwenye mantiki. Majaliwa tumsifu, ila asitumalizie akili.