Msajili abariki Mbatia kung’olewa

James Mbatia

Muktasari:

  • Ikiwa imepita miezi mitano tangu kuibuka kwa mvutano wa makada ndani ya Chama cha NCCR Mageuzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imebariki kung’olewa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.

Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi mitano tangu kuibuka kwa mvutano wa makada ndani ya Chama cha NCCR Mageuzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imebariki kung’olewa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.

Mei 21, Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi iliitisha mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Jeshi la Wokovu Kurasini na miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni pamoja na kumsimamisha James Mbatia kujihusisha na shughuli za chama.

Hata hivyo, Septemba 24, mkutano mkuu maalum wa NCCR Mageuzi uliofanyika jijini Dodoma ulimvua uanachama James Mbatia na kumfuta uongozi aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Angelina Rutairwa.

Mwananchi limeiona barua iliyotoka ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa nchini na kusainiwa na Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza ikihalalalisha mabadiliko ya viongozi hao wakuu wa chama hicho kikongwe cha upinzani nchini.

Katika barua hiyo iliyoandikwa Oktoba 24, msajili ameeleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 23, 26, 28 na 31(2) ya Kanuni na Usajili na Ufuatiliaji wa Vyama vya Siasa, vikao hivyo vya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama yalifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na katiba ya NCCR Mageuzi.

“Msajili wa Vyama vya Siasa ameridhika kuwa kikao cha halmashauri kuu ya chama chenu cha Septemba 23, kikao cha halmashauri kuu cha Septemba 24 na mkutano mkuu wa Septemba 24 uliofanya mabadiliko ya uongozi na katiba ya chama chenu yalifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa,” inasomeka sehemu ya barua hiyo iliyotolewa na msajili.

Akizungumza na wanahabari hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa NCCR (Bara) Joseph Selasini alisema sasa umefika wakati mtu yeyote atakayeongea na kujitambulisha kama kiongozi wa chama kinyume na utaratibu, sheria itafuata mkondo wake.

“Imefika wakati sasa msajili afuate sheria, kuna mkakati uliopo kuhakikisha vurugu ndani ya chama hiki haziishi, tunamwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) kuyafanyia kazi malalamiko yetu,” alisema Selasini.

Kuanzia Novemba 7, alisema chama hicho kitaanza ziara ya kwenda mikoani na kumtaka IGP pamoja na wasaidi wake kushughulikia taarifa zilizopo mezani kwake kwa kuwa maisha yao yapo rehani lich ay akutekeleza wajibu wao wa kikatiba kufanya shughuli halali.

“Baada ya kukamilisha vikao vyetu jijini Dodoma ukiwamo mkutano mkuu, sheria inasema kabla ya mkutano unatakiwa kupeleka taarifa kwa msajili siku 28 kabla ya kufanyika mkutano na tulifanya hivyo,”

“Lakini, siku 14 baada ya mutano unatakiwa kupeleka taarifa ya kilichojiri ambapo sisi tulipeleka taarifa ya mkutano na mabadiliko ya uongozi Septemba 28,” alisema Selasini.

Gazeti hili lilimtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliyesema hayupo ofisini, hata hivyo Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza alikiri kuwa barau hiyo imetoka ofisini kwao.

Alipotafutwa Mbatia alisema jambo lolote linapokuwa mahakamani hawezi kulizungumzia kwani hata Bunge lenyewe haliwezi kuzugumzia jambo hilo.

Alisema kwa kitendo kilichofanywa na ofisi ya msajili, ni kuingilia mahakama na akataka wananchi kujifunza ukweli kwamba tawala wa sheria haupo wala kuzingatiwa nchini.

“Mimi niseme tu haya niliyategemea, kama msajili amefanya hivyo, anatangaza kila mtu ajichukulie sheria mkononi, sitaki kuwa sehemu ya kujadili mambo yaliyoko mahakamani,” alisema Mbatia.

Kwa mujibu wa kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho, miongoni mwa tuhuma zilizokuwa zinamkabili Mbatia ni pamoja na kuuza mali za chama kinyume na utaratibu yakiwamo mashamba na nyumba zilizopo maeneo tofauti nchini pamoja na kuchochea migogoro ndani ya chama hicho jambo ambalo h alikubaliki kwa mujibu wa katiba yao hata sheria za nchi.