Msajili ailima TLP barua
Muktasari:
- Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeutaka uongozi wa TLP kujieleza Kwa nini umeshindwa kufanya uchaguzi kuziba nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, marehemu Augustine Mrema na kusababisha malalamiko.
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imeutaka uongozi wa chama cha labour Party (TLP) kujibu malalamiko yaliowasilishwa na wagombea wa nafasi ya uenyekiti ya kutofanyika uchaguzi wa kuziba nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, marehemu Augustine Mrema.
Machi 6 mwaka huu waliokuwa wagombea wa nafasi ya uenyekiti waliwasilisha malalamiko katika ofisi ya msajili kuhusu kuvunjwa kwa mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi huo.
Barua iliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa juzi Machi 9 imesema Msajili ampokea barua kutoka kwa wagombea wa nafasi hiyo, wakilalamika kwamba mkutano mkuu wa chama uliokuwa umepangwa kufanyika Machi 6, ulihairishwa bila kufuata taratibu, uliopo katika katiba na kanuni za chama.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 5B cha sheria ya vyama vya siasa sura ya 258, uongozi wa TLP mnapaswa kuwasilisha maelezo kwa msajili wa vyama vya siasa kujibu malalamiko yaliyowasilishwa na wagombaea hao, ili msajili ajue ukweli wa suala hilo,” imeeleza barua hiyo
Aidha maelezo hayo yanapaswa kuwasilishwa ofisi ya Msajili kabla ya Machi 15 saa 9:30 Alasiri.
Kwa mujibu wa barua hiyo, wagombea hao wamemwomba Msajili aiamuri TLP kuitisha mkutano mkuu maalumu haraka iwezekanavyo ili demokrasia ndani ya chama itekelezwe.
“Kuna wajumbe zaidi ya 150 wapo Dar es Salaam, tangu Machi 5, hadi leo wakisubiri kufanyika kwa mkutanao huo,” imeeleza barua hiyo.
Miongoni mwa wagombea hao ni Kinanzaro Mwanga, Abuu Changawa, Stanley Ndamugomba, Aivan Maganza.