Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nchimbi: Haki ndiyo msingi wa amani

Muktasari:

  • Asema hakuna mgongano kati ya kutetea haki na kulinda amani, akieleza kuwa misingi hiyo miwili inategemeana katika kujenga taifa lenye utulivu na maendeleo.



Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, amesema Tanzania haiwezi kuwa na amani ya kudumu bila haki, akisisitiza kuwa viongozi na wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kusimamia haki bila hofu ili kuimarisha umoja na mshikamano wa taifa.

Akizungumza leo, Julai 24, 2026, katika Mkutano Mkuu wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Dk Nchimbi amesema alifurahishwa na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan alipowaapisha majaji mwezi Mei mwaka huu aliposema, "Haki ni msingi wa amani," akieleza kuwa kauli hiyo inapaswa kuwa mwongozo kwa viongozi wote.

"Rais alisema haki ni msingi wa amani. Nilimshukuru kwa kulisema hadharani kwa sababu viongozi wote tulio chini yake tunapaswa kuhubiri jambo hilo. Ukianza kuogopa kutamka kwamba haki ni msingi wa amani, unaanza pia kuona haya kutekeleza haki," amesema Dk Nchimbi.

Amesema hakuna mgongano kati ya kutetea haki na kulinda amani, akieleza kuwa misingi hiyo miwili inategemeana katika kujenga taifa lenye utulivu na maendeleo.

"Haiwezekani mtetezi wa amani akawa adui wa haki, wala mtetezi wa haki akawa adui wa amani. Hilo halifikiriki. Tunapaswa kujiepusha na mtazamo huo," amesema.

Makamu wa Rais amesema anatamani kuona Tanzania ambayo kila mwananchi anajivunia utaifa wake, anahisi yuko salama na ana nafasi sawa ya kushiriki katika maendeleo ya nchi.

Dk Nchimbi amesema tofauti za kisiasa, dini na makabila hazipaswi kuwa chanzo cha migawanyiko, bali Watanzania wanapaswa kuunganishwa na utambulisho wao kama taifa moja.

"Ninatamani tuwe na Tanzania ambayo kila Mtanzania anajisikia fahari ya Utanzania wake, kila mmoja anajisikia yuko salama ndani ya nchi yake na ana hamu ya kuchangia maendeleo ya taifa. Natamani nchi ambayo tunatofautiana kwa itikadi, vyama vya siasa, dini na makabila, lakini tunakumbatiana kwa Utanzania wetu. Hiyo ndiyo Tanzania ninayoitamani," amesema.

Amesema jamii inapaswa kufikia hatua ambayo watu wenye mitazamo tofauti wanaweza kukutana, kujadiliana na kushirikiana bila kuwekewa tafsiri za uadui au uhasama.

"Ninatamani nikikutana na mwanaharakati yeyote nitambulike na nimtambue kwa uwezo wake wa kufikiri na kushawishi. Watu wasione nikikaa na mtu mwenye mawazo tofauti kwamba kuna uadui. Waone wanaongea mambo ya nchi yao kwa amani," amesema.

Akitoa mfano, Dk Nchimbi amesema anatamani kufika wakati ambapo hata akionekana akizungumza na mwanaharakati Maria Sarungi, jambo hilo litafsiriwe kama sehemu ya mjadala wa kujenga taifa na si uhasama wa kisiasa.

"Nikiwa nimekaa na Maria Sarungi, watu waseme wanaongea mambo ya nchi yao. Hamna uhasama, hamna uadui. Hiyo ndiyo aina ya taifa natamani tulijenge," amesema.

Pia ametoa wito kwa Watanzania kutumia nafasi walizonazo kurejesha umoja na mshikamano wa taifa, huku wakisimamia haki kama msingi wa amani na maendeleo.

"Nimuombe kila Mtanzania atumie kila nafasi aliyonayo kurudisha umoja, kurudisha mshikamano, lakini pia kusimamia haki kama msingi wa amani," amesema.