Njano na kijani zatawala Dar ,CCM kikizindua kampeni
Muktasari:
- Mgombea urais Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa wagombe 17 walioteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwania nafasi hiyo jana Jumatano Agosti 27, 2025 kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, mwaka huu.
Dar es Salaam. Ni kijani na njano! ndiyo hali halisi ilivyo katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, wanachama, wapenzi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliovalia sare za chama hicho wakiendelea na hekaheka za uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Katika jiji la Dar es Salaam hususani kwenye maeneo ya Mbezi Louis hadi Ubungo, kwenda mpaka Mwenge ni rangi za njano na kijani ndizo zimeshamiri, makada hao wakielekea viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe kwenye shamrashamra za uzinduzi wa kampeni za chama hicho zinazofanyika leo Alhamisi Agosti 28, 2025.
Mwananchi iliyokuwa kwenye mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, imeshuhudia funga kazi kwenye njia panda ya kwenda Kawe, ambako mamia ya wanachama wakiwa wameongozana kuelekea viwanja vya Tanganyika Packers, huku Polisi wa kutuliza ghasia (FFU), Polisi wa Usalama Barabarani na askari wa Jeshi la Wananchi baadhi wakiwa makini kuimarisha ulinzi na usalama huku wakiyaongoza magari na raia.
Katika eneo yalipojengwa maduka Lugalo Jeshini, daladala zinazopita njia hiyo kuelekea Kawe, zinaelekezwa kugeuzia hapo na hakuna inayoruhusiwa kufika Kawe mwisho ambako ndipo ulipo uwanja wa Tanganyika Packers.
Katika eneo zilipo flemu za maduka Lugalo ambako ndipo kituo cha daladala kuna wanajeshi wametawanyika sehemu tofauti tofauti, wengine wakiongoza magari yanayogeuzia hapo, wengine wakiongoza mamia ya wananchi wanaoshuka kwenye daladala hizo.
Mbali na wanajeshi hao, pia askari wa kutuliza ghasia ambao hawana silaha, wanaendelea kusimamia na kuhakikisha usalama wa mamia ya wafuasi na wapenzi wa chama hicho wanakuwa salama.
Askari wa usalama barabarani nao hawajabaki nyuma, wanaendelea na jukumu lao la kuhakikisha hakuna foleni ya magari ambayo mengi ni ya binafsi na ya umma yakiegeshwa mbali kidogo na vilipo viwanja vya Tanganyika Packers.
Hata hivyo, utaratibu huo unaonekana kuibua fursa kwa waendesha bodaboda ambao wanabeba abiria kwa Sh1,000 mpaka Sh2,000 kutoka Kawe Mwisho hadi eneo zilipo flemu za maduka kwenye fensi ya Lugalo ambako daladala zinaishia, kwa wale ambao wako Kawe kwa ratiba zingine na si kampeni za CCM.
Katika mitaa ya Kawe, kuanzia kituo cha Kanisani kuelekea hadi Tanganyika Packers katika nguzo za umeme, kumepambwa kwa bendera za CCM ambazo zinapepea kila upande.
Mamia ya wananchi wenye sare za chama hicho wanapishana wengine wakiingia na wengine wakitoka, wote wakiwa na shauku ya shamrashamra hizo za ufunguzi wa kampeni.
Katika mkutano huo, mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi watatambulishwa kwa Watanzania kabla ya kuendelea na kampeni katika mikoa mbalimbali nchini kuanzia kesho kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM.
Uwanja wafurika
Maelfu ya wapenzi, wafuasi na wanachama wa chama hicho wamejitokeza kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo.
Hadi kufikia saa 8:30 mchana katika viwanja vya Tanganyika Packers, unapofanyika mkutano huo wa ufunguzi ulikuwa umefurika maelfu ya wananchi.
Walinzi wanaosimamia usalama, ilipofika saa 7:16 mchana walizuia watu kuendelea kuingia kwa kutumia geti namba moja, wakieleza eneo hilo limejaa, wakitaka wananchi kutumia geti la pili, ambako nako mamia ya wananchi walikuwa wamefurika na wakati wowote palitarajiwa kujaa kutokana na idadi ya watu waliopo nje.
Pembeni mwa viwanja hivyo, maelfu ya wananchi pia wanaendelea na pilikapilika, wengine wakifanya biashara na wengine wakiendelea na shamrashamra za ufunguzi wa kampeni hizo.
Inaelezwa tangu saa 12 asubuhi wananchi walianza kuwasili katika viwanja hivyo.
Misafara ya viongozi imeanza kuwasili viwanjani hapo saa 7:41 mchana, ikipishana kwa dakika chache.
Hakuna daladala, fursa kwa bodaboda
Shamrashamra hizo zimegeuka kero kwa watumiaji wa usafiri wa umma kutoka Kawe kwenda kwenye maeneo mengine ya jiji.
Katika eneo la Kawe, kuanzia round about ya Kawe kama unatokea Mbezi Beach, kwenda hadi Ukwamani, kuanzia saa 6 mchana hadi sasa hakuna daladala inayoruhusiwa kuingia, isipokuwa zile zilizokodiwa kubeba watu wanaokwenda kwenye mkutano ambazo zikishashusha abiria zinapaki.
Mamia ya wananchi wanaotokea Kawe wanalazimika kutembea kwa miguu ili kusogea eneo ambako watafanikiwa kupata usafiri wa umma.
Katika mkutano huo, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi wanatambulishwa rasmi kwa Watanzania kabla ya kuendelea na kampeni katika mikoa mbalimbali nchini.