Paresso: Huyu ndiye Samia wa miaka mitano ijayo
Muktasari:
- Cecilia Paresso ni miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaozunguka mikoa mbalimbali kusaka kura kwa wagombea wa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi wa Oktoba 29,2025.
Mageuzi ya kiuchumi yaliyotokana na ubunifu na utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati nchini Tanzania, yanatajwa kuwa miongoni mwa sababu kwa Watanzania kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wagombea wake, akiwemo Samia Suluhu Hassan anayewania urais.
Kukamilika kwa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Daraja la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza, Reli ya Kisasa (SGR) na miradi ya ujenzi wa barabara, imeelezwa kuwa ni turufu kwa Samia katika harakati za kunadi sera zake na kuomba kura kwa wananchi.
Hayo yameelezwa jana Alhamisi Oktoba 9, 2025 na aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, Cecilia Paresso wakati akizungumza kwenye mkutano wa kumnadi mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Jimbo la Rufiji, mkoani Pwani, Paresso amesema Samia amefanya kazi kubwa ya kuleta mageuzi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya na elimu, hivyo anastahili kupewa kipindi cha miaka mitano kingine.
Amesema mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Samia katika kipindi cha miaka minne tangu kuingia madarakani, ni ushahidi tosha wa uongozi wa busara, maono na uchapakazi.
“Katika kipindi cha miaka minne, Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuboresha huduma za afya nchini. Amejenga zahanati katika maeneo mengi, vituo vya afya, hospitali za wilaya, na kuendeleza hospitali za rufaa pamoja na za kanda. Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan tunayemhitaji miaka mitano ijayo,” amesema Paresso.
Kuhusu sekta ya elimu, Paresso amesema Samia ametoa kipaumbele katika maboresho ya mitaala na sera ya elimu, akisisitiza usawa wa fursa kwa watoto wote bila ubaguzi.
“Katika kipindi chake, ameboresha mitaala ya ufundishaji, amefanya marekebisho ya sera ya elimu ili kila mtoto apate fursa ya kusoma bila vikwazo.
“Amehakikisha wasichana waliopata ujauzito wanarejea shuleni na elimu bila ada imeendelea hadi kidato cha sita. Huyu ndiye Samia tunayemhitaji miaka mitano ijayo,” ameongeza.
Paresso aliwahimiza wananchi wa Rufiji na Watanzania kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono mgombea huyo. Katika mkutano huo, Paresso alimnadi mgombea ubunge wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa pamoja na madiwani wa kata mbalimbali wilayani humo.
Dk Nchimbi yuko mkoani Pwani kunadi sera za CCM, kuwaombea kura wabunge na madiwani wa chama hicho baada ya kuhitimisha mikutano kwenye visiwa vya Unguja na Pemba.