Prime
Pumzika salama Jenerali David Musuguri
Mpendwa Jenerali David Bugozi Waryoba Musuguri Nzangho aka Chakaza (RIP).
Kwanza, nakupigia saluti ya mwisho kama mgeshi aliyelala. Pili, niseme wazi. Najua hutapokea wala kujibu saluti yangu kama kiongozi na mkuu wa mafyatu. Nenda salama salimini ukijua kuwa mafyatu watakumiss sana. Ulikuwa fyatu wa kupigiwa mfano.
Siombolezi bali nasherehekea kuondoka kwako. Old soldiers never die, they simply fade away. Baada ya kushughulika kwa miaka 104 na ushei, kwani ulibakisha miezi miwili tu kupiga 105. Si haba. Sasa rasmi umelala milele. Nenda shujaa mwenye sifa zilizotukuka ndani na nje ya kaya. Ulifanya mengi kwa kaya na Mungu akulipe huko uendako. Amina. Najua hutanisikia. Lakini acha nikupe send off na maua ya kifyatu.
Kwanza, ulikuwa fyatu mwenzangu uliyemfyatua na kumchakaza nduli Idi Amin na kuwakomboa Waganda. Kila niendapo UG, huwa najisikia fahari niitwapo mkombozi. Wengine hunisonya kwa sababu tulimfyatua nduli tukafyatua M7 ambaye, kwa takriban miaka 40, amekuwa akitembeza undava yeye na familia na marafiki zake. Sorry bro. Siku hizi siruhusiwi kuongea siasa. Hivyo, naomba unisamehe nisikumegee ujiko mwingi tunaoupata tokana na kazi yako.
Pili, kwa wasiokujua Jenerali na mkuu wa mageshi mstaafu, hasa vijana wa kileo, ni kwamba ulikuwa mwanajeshi tangu ujanani. Ulijiandikisha geshini mwaka 1942 ukiwa na umri wa miaka 20. Hii ni baada ya maza wako kunyotolewa roho kwa tuhuma za kijinga zisizokuwa na kichwa wala miguu za uchawi. Hivyo, ukiwa na vijana wenzako akina Mugendi Nyamatwema na Mkono wa Nzenzere, mliamua kujiandikisha geshini ili mkachichue na baadaye kuitumikia kaya.
Tatu, kwa mujibu wa historia yako ambayo sisi tunaokujua tunaijua, ulizaliwa Januari 4, 1920 huko Butiama alikozaliwa marehemu Baba wa Taifa. Hivyo, hamkuwa marafiki tu bali wa poti kama akina mura wapendavyo kuitana, yaani wa kunyumba au wa nyumbani.
Baada ya kujiandikisha, siyo kujiunga jeshini, ulipelekwa Madagascar na kupata mafunzo ya kigeshi kabla ya kwenda sehemu nyingine tena ukiwa chini ya KEA au King’s African Rifles (KAR) wakati wa mkoloni wa kiinglishi. Baadaye, ulipelekwa Nairoberry pale Kahawa Barracks ulipokutana na nduli na kumfundisha ugeshi.
Kwa wasiojua, nduli aliposikia kuwa mmojawapo wa makamanda waliokuwa wametumwa na kaya kumfyatua ulikuwa mwalimu wake, alichukua helikopta na kutoroka haraka ili asipate cha moto na kipigo cha mbwa kachoka kutoka kwa Jenerali Chakaza. Maana alijua shughuli yako, Jenerali ambaye kweli ulionyesha vitendo kwa kuikomboa UG ndani ya muda mfupi tofauti na wengi walivyotegemea.
Katika uhai wako, nakumbuka ulipata masomo mbalimbali nchini China na Kanada na mbali na kuwakilisha Afrika Mashariki London, Uingereza kwenye gwaride la Malkia mwaka 1957 mbali na kupigana vita nchini Burma, India na Ujepu ambako ulijeruhiwa paja na kupona na kuendelea kudunda kigeshi.
Jenerali, kama lilivyokuwa jina lako, ulichakaza lakini hukuchakaa. Kwani, ni wachache wanaoweza kupiga miaka 100 na ushei halafu wakafyatuka wakiwa na hali nzuri kama ulivyokuwa. Mwenyezi Mungu amelipa ujasiri na wema wako kwa kaya yetu.
Naomba, ufikapo huko uendako, wasalimie rafiki na ndugu yako Bwana mdogo wako lakini bosi wako, Julius Kambarage Nyerere, Eddie Soikoine, Rashid Kawawa, Ali Hassan Mwinyi, Hussein Shekilango, majenerali Abdallah Twalipo, Tumainiel Kiwelu, Ernest Mwita Kyaro, Mti Mkavu Silas Mayunga na wengine wengi, bila kusahau wasoja wetu waliodedishwa kule Uganda wakipigania ukombozi wa kaya yetu.
Habari njema ni kwamba CDF wetu wa kwanza, Jenerali Mrisho Sam Hagai Sarakikya bado anadunda tena kama yanki na mgeshi asiye na mfano. Mungu amuongezee miaka kama wewe. Amina. Saluti yake kamanda.
Kwa vijana wa sasa wasiokujua, natumia fursa hii kuwafyatuliwa ukweli juu ya kutukuka kwa urathi wako. Ulikuwa mkuu wa mageshi yetu ambaye aliteuliwa wiki moja baada ya kurejea toka kumfyatua nduli.
Ukakamavu na weledi wako wa medani ya kivita ulisababisha kaya kumfyatua huyu mjivuni aliyekuwa na domo kubwa kiasi cha kuwanyanyasa na kuwatisha maadui zake lakini asifue dafu kwako. Pia, ulikuwa kiongozi usiyejivuna wala kuwatumikisha wenzake zaidi ya kuwatumikia na kuwa tayari kujitoa kafara kwa ajili ya wengine.
Umeacha turathi ya kuigwa na kupigiwa mfano kama msoja na mwanakaya fyatu, ingawa siku hizi ni wachache wanaoweza kukuiga kutokana na uongozi kugeuka uongo na usasi wa ngawira. Hayo tuache nisije nikafyatuliwa bure. Kimsingi, nidhamu yako iwe kijeshi au hata baada ya kustaafu havitasahaulika. Ulitumikia kaya kwa ari na mori wa hali ya juu.
Nasikitika sitahudhuria mazishi yako kwa vile niko mbali kwenye misheni ya kuokoa kaya toka kwenye ufisi na ufisadi. Sitafaidi sauti za mizinga ikilipuliwa kuonyesha kuwa shujaa umeondoka kishujaa na kuagwa na mafyatu na mashujaa wenzako.
Kutokana na kutokuwa na muda wa kutosha, acha nikuage fyatu mwenzangu. RIP David Bugozi Musuguri, shughuli umeimaliza na vita umeshinda.