Rais Mwinyi awaonya ‘wanaoitukana’ CCM

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, akizungumza wakati wa mkutano wa ndani katika ziara ya kichama iliyofanyika Mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar.Picha Ikulu

Unguja. Fukuto ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) upande wa Zanzibar limezidi kufukuta baada ya makamu mwenyekiti wa chama hicho visiwani humo, Rais Hussein Ali Mwinyi kuagiza viongozi wa chama hicho kuwashughulikia wanachama “wanaokiuka maadili na kukitukana chama hicho pamoja na viongozi wake.”

Dk Mwinyi amesema wameibuka baadhi ya wanachama wanaovunja maadili ya chama hicho kwa makusudi lakini chama kinawaacha wakiendelea kutamba na kusubiriwa kuchukuliwa hatua wakati wa uchaguzi, jambo ambalo alisema linahatarisha uhai wa chama.

Licha ya Rais Mwinyi kutokutaja jina la mwanachama yoyote kwenye hotuba yake, kauli ambazo zimeibua mjadala na msukumo wa kutaka aliyezitoa aitwe kwenye kamati ya maadili ni za Balozi Ali Abeid Karume, mwanachama wake mashuhuri, ambazo zimekuwa mwiba kwa watawala na kwa chama hicho.

Mara kadhaa, mwanadiplomasia huyo ambaye ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume amekuwa akitoa kauli mbalimbali kwamba chama hicho kimekosa uhalali wa wananchi kuongoza visiwani humo.

Katika moja ya kauli hizo Balozi Karume amekituhumu chama chake kuingia madarakani kwa wizi wa kura, akidai CCM haijawahi kushinda uchaguzi wa urais Zanzibar, bali kwa wizi wa kura.

 Kauli hizo zimeibua mjadala ndani ya chama hicho huku viongozi wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar, Dk Muhammed Dimwa na Katibu wa Kamati Maalumu ya Idara ya Itikadi na Uenezi visiwani humo, Khamis Mbeto wakisema chama kimemsikia Balozi Karume na suala lake litashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za chama.

Wakati ikisubiriwa kuona hatua gani zitachukuliwa dhidi ya Balozi Karume juu ya kauli zake hizo, jana Rais Mwinyi akizungumza na viongozi wa CCM ngazi ya mashina hadi Mkoa wa Kusini Unguja na kutembelea miradi mbalimbali ya chama hicho, aligusia hatua za kuchukuliwa kwa wanachama wake wanaokiuka maadili.

"Wakati mwingine watu wanavunja maadili lakini wanatazamwa na kusubiriwa kwenye uchaguzi. Huo si utaratibu, tuanze sasa, wanaofanya hivyo washughulikiwe kwa mujibu wa utaratibu kuanzia sasa na ndiyo maana kuna kamati za maadili, zinatakiwa zifanye kazi yake," alielekeza Rais Mwinyi

Akionekana kukerwa zaidi, Rais Mwinyi alisema, "haiwezekani hata siku moja watu wanavunja maadili tunawaacha. Huo ugonjwa ukizidi kukua baadaye unakuwa mkubwa zaidi, kwa hiyo kamati hizi zifanye wajibu wake."

"Wapo viongozi wa CCM leo wanatukana chama chao tunawaacha, haiwezekani. Huyo anayejiita yeye mwanachama anakaa hadharani anasema maneno ambayo mtu yeyote mwanachama wa CCM hawezi kusema maneno hayo." alisema.

Balozi Karume hakupatikana alipotafutwa na gazeti hili jana kwa simu na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi haukujibiwa.

Hata hivyo, akizungumzia mipango wa makada wa CCM kutaka kumuita Juni mosi, Balozi Karume alisema hakuna aliyemfuata au kuelezwa lolote na amekuwa akitumia haki yake kueleza kile anachokiona.

Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Mwinyi, mwanachama wa chama hicho Amina Said Othman alisema wanaamini hakuna mwanachama anayeogopwa kuchukuliwa hatua iwapo atakwenda kinyume na miongozo na taratibu za chama.

Mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, Ameir Waziri alisema chama hakipaswi kuishia tu kuwaonya na kuwachukulia hatua makada hao, bali kuchunguza na kubaini mtandao wote uliopo nyuma ya wanachama wanaokigeuka na kukitukana hadharani.

Kauli ya Waziri inafanana na ile iliyotolewa wiki iliyopita na mchambuzi mwenzake wa masuala ya siasa visiwani humo, Ali Makame alipozungumza na gazeti hili kuhusu kauli za Balozi Karume akisema CCM ina nidhamu kutoka juu hadi chini, hivyo anapotokea mtu akafanya hivyo, tena akiwa kada mzoefu, ni wazi amekiuka taratibu za chama.

Alisema wakinyamazia suala hilo kuendelea na wengine wakawa wanakosoa bila kufuata utaratibu, inaweza kuleta athari kubwa ndani ya chama hicho.

Makame alitaja moja ya athari zinazoweza kujitokeza kuwa ni chama kupoteza mvuto na uaminifu kwa wanachama wake, hivyo kusababisha makundi mengine kuibuka na kuanza kukosoa wakijua hakuna hatua zitakazochukuliwa.

Alisema kujibizana naye itamfanya aonekane ni shujaa kwa sababu yeye kama amekosea na wengine (wanachama) hawapaswi kukosea kujibizana naye, isipokuwa kuchukua hatua kama ambavyo wamekuwa wakichukuliwa makada wengine wanapokengeuka.

"Suala la msingi tunayo rekodi ya wale makada ambao wamekosoa chama kinyume na utaratibu na wakachukuliwa hatua, tukimuacha hiki kitakuwa kirusi kibaya kwa CCM, maana nidhamu itaondoka na ikishaondoka CCM itapata athari," alisema Makame.

Juni mwaka jana, chama hicho kilimvua uanachama Kada na Mzee wa chama hicho Makao Makuu ya CCM Kisiwandui, Baraka Shamte.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kutuhumiwa na chama hicho kusambaza kipande cha sauti chenye maneno yaliyotafsriwa ni ya kumkashifu Rais Mwinyi na utawala wake.

Juni 13, 2022 CCM Mkoa wa Mjini kupitia kikao chake cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa huo ilipitisha azimio la kumvua uanachama Mzee Shamte kufuatia vitendo vyake vya ukiukaji wa maadili ndani ya chama.

Licha ya kuvuliwa uanachama kada huyo, alikumbana na sekeseke lingine ambapo alivamiwa na kikundi cha watu wasiojulikana na kumpiga na kumvunja mguu kisha akalazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Hata hivyo waliofanya tukio hilo hawakukamatwa licha ya polisi Mkoa wa Mjini kueleza wanawasaka waliofanya tukio hilo.

Baada ya muda, Mzee Shamte aliomba msamaha kwa chama hicho akidai alikosea kumdhihaki kiongozi huyo na alisemehewa lakini hakurudishwa kwenye nafasi yake ya uzee wa chama.


Ugomvi wabunge, wawakilishi

Katika maelezo yake, Rais Mwinyi alikwenda mbali zaidi akisema wapo wabunge na wawakilishi wanagombana lakini chama hakiongei chochote.

Alisema mbunge na mwakilishi wasipoelewana na kugombana wanategeneza makundi katika maeneo yao na makundi hayo yanakuwa hatari kwa chama, hivyo chama kinatakiwa nao kiwaite wajieleze na kisha hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

"Kila mara napata habari kwamba mbunge huyo kafanya hiki na mwakilishi huyu kafanya hivi, ndugu zangu haya tuyafanye sasa tusingoje uchaguzi, tuwashughulikie sasa," alisema.

Alisema iwapo wakiyafanya hayo chama chao kitakuwa imara na hakuna kitakachoharibika.

Alisema hakuna uhai katika chama kama hakuna umoja na mshikamano kwani kila unapokuwapo uchaguzi kinakuwa na makundi lakini baada ya hapo wanatakiwa kuyavunja na kuwa kitu kimoja.

“Tunachotakia kufanya sasa kuondoa tofauti zetu hili litatusaidia sana na tutapambana na watu wa nje si wa ndani, kwa hiyo niwaombe sana wenye makundi wayavunje tuwe wamoja na kuendeleza chama hili litatusaidia kushika dola katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025,” alisema.


Kifua mbele

Rais Mwinyi aliwaeleza wanachama hao kutembea kifua mbele akisema hakuna shaka kwamba chama kinatekeleza ilani na kwa kasi waliyonayo ikifika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 watakuwa wamekamilisha miradi iliyoahidiwa.

Alisema kwa sasa tayari zimejengwa shule za maghorofa, barabara zinajengwa, hospitali zinajengwa katika wilaya zote 11 huku kukiwa na miradi mingi ya maji na umeme inayotekelezwa kwa wakati mmoja.

Aliwataka viongozi hao wawe na mkakati maalumu wa kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake kuongeza idadi ya wanachama kwamba mtaji wa chama cha siasa ni watu

Pia alisema lazima chama kiwe na uchumi imara unaoendana na hadhi ya chama hicho kwani kina miradi mingi ambayo haijaendelezwa.

"Hiki chama kina muda mrefu na kimeshika dola muda mrefu, hivyo hatuna sababu kwa nini tusiwe na uchumi imara maana tuna ardhi na majego mengi," alisema.

Katika mkutano huo, Rais Mwinyi alisema umefika wakati chama hicho kuwalipa posho mabalozi wa mashina. Alisema watendaji hao wanajitolea kwa muda mrefu ndani ya chama hicho lakini hawapati chochote.

Alimuagiza Naibu Katibu Mkuu CCM-Zanzibar, Dk Muhammed Dimwa kuandaa utaratibu wapatiwe vitambulisho maalumu waanze kupewa posho.

"Wakati umefika sasa tuwape posho mabalozi hawa kwa sababu wanafanya kazi kubwa. Natoa maagizo sasa andaa utaratibu wawe na vitambulisho maalumu," alisema.

Alisema kumekuwapo na ugumu wa chama hicho kuwalipa mabalozi hao kwa sababu ya wingi wao maana wapo zaidi ya 5,000.

Awali, Dk Dimwa alisema chama hicho kinasimamia misingi mikuu na tunu za taifa kulinda maridhiano. Alisema kitaendelea kusimamia chama na Serikali yake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Muhammed Kawaida alisema vijana wataendelea kuwalinda, kuwatetea na kuwapigania viongozi wakuu wa chama hicho.