Mwinyi kuwapa ajira wanaojitolea CCM

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiwa anazungumza katika moja ya tukio la chama hicho.

Unguja. Makamu Mwenyekiti wa CCM- Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi ameahidi kukomesha tabia ya kuwekwa kando vijana wanaojitolea ndani ya chama hicho pale zinapojitokeza fursa za ajira.

Rais Mwinyi alitoa kauli hiyo jana wakati akihitimisha ziara yake ya kutembelea mali za chama hicho na jumuiya zake katika Mkoa wa Mjinina kuwataka watendaji wote wanaohusika iwapo watahitaji vijana wa kuajiriwa wampelekee waliojitolea kwa muda mrefu ndani ya chama hicho.

“Vijana wengi wamejitolea katika chama kwa muda mrefu ninyi ni wapiganaji wakubwa sana, natambua kuwa kuna baadhi ya wakati tunapokuwa na fursa za ajira si nyie mnaopata.

“Safari hii tutahakikisha wale vijana waliojitolea ndio watakaopewa fursa. Nataka niwaelekeze hapa watendaji wote nikisema safari hii nileteeni majina ya vijana nileteeni majina ya vijana hawa,” alisema Mwinyi huku vijana hao wakimshangilia.

Alisema ana mipango ya kuzalisha ajira nyingi na kuwachukua vijana wengi, hivyo wasivunjike moyo.

Kuhusu miradi ya CCM, alisema ni lazima waangalie vema mali hizo na wawe na miradi mikubwa ya kukiendesha chama kiuchumi.

Alisema jumuiya zote za chama lazima ziwe na ofisi za kisasa na majengo yanayoendana na hadhi ya chama hicho katika ngazi zote.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, baada ya ziara amepata mtazamo mzuri kuhusu rasimali za chama hicho, hivyo watafanya mambo makubwa ya kukifanya chama kiwe na uwezo mkubwa kama vyama vingine duniani.

Huku akitolea mifano ya vyama vya kikomonisti (China) na ANC (Afrika Kusini) Dk Mwinyi alisema hakuna sababu ya kwanini CCM kisiwe na miradi kama hiyo maana wana rasimali za kutosha.Awali, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Musa Haji Mussa alisema jumuiya hiyo ina mipango na ndoto kubwa za kufanya uwekezaji wa miradi mbalimbali, anaamini ndoto hizo zitafikiwa kupitia kwake (Mwinyi).

Alisema wana ndoto kubwa za kutengeneza miradi mikubwa, ili jumuiya hiyo iwe na miradi mingi, hivyo wana imani na Dk Mwinyi atafanikisha kutekeleza ndoto zao.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini, Suleiman Tate alisema wanapata hofu eneo la mradi katika ofisi hiyo likapitiwa na mradi wa kujenga barabra za juu unaotarajiwa kujengwa Amani, hivyo kupoteza moja ya vitega uchumi

Hata hivyo, Dk Mwinyi alisema sula hilo wanapaswa waangalie sasa kuona michoro ya mradi huo unapopita ili waone kitakachofanyika.

Katika ziara hiyo Dk Mwinyi alitembelea maduka na sehemu ya vileo Amani, eneo la maduka Youth League darajani, sheli na eneo la umoja wa vijana Gymkana.