Rais Mwinyi apokea ripoti ya CAG, aagiza ipelekwe barazani

Rais Hussein Mwinyi akipokea vitabu vya ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Dk Othman Abbas Ali Ikulu Zanzibar.

Unguja. Rais Hussein Mwinyi amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2022/23 Ikulu, Zanzibar.

Akipokea ripoti hiyo Rais Dk Mwinyi amemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman kuiwasilisha katika Baraza la Wawakilishi.

Akizungumza baada ya kukabidhi ripoti hiyo kwa Rais Dk Mwinyi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Dk Othman Abass Ali,  alisema wamewasilisha ripoti saba ikiwemo ya Serikali Kuu (Mawizara na taasisi zote), Mashirika na Taasisi zinazojitegemea.

"Ripoti ya Idara Maalum na taasisi zake, ripoti ya mifumo yote ya Tehema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ripoti ya mashirika ya umma, na ripoti ya ufanisi ya miradi ya maendeleo iliyofadhiliwa na fedha za Uviko 19," alisema

Amesema ripoti hizo zipo za aina mbili ikiwemo miradi ya maendeleo ya wahisani pamoja na ya Serikali pamoja na ripoti za kiufundi.

“Tunapojenga tunatakiwa kufanya ukaguzi wa thamani ye fedha, tumefanya ukaguzi huu kwa sekta za afya na elimu kwa skuli zote 12 zilizojengwa” alieleza CAG.

Pia amesema walifanya ukaguzi kwa Shule ya Bweleo ambayo Serikali iliinunua na shule zote zilizofanyiwa matengenezo ikiwemo vyoo vya shule hizo na kuonesha yote yaliyobainika kwenye ukaguzi huo.

Kifungu cha 112 (5) kinamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali awasilishe taarifa yote aliyoikagua na aikabidhi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa hatua nyengine.