Prime
Mwalimu ajiweka kando Chaumma, aomba uchunguzi
Muktasari:
- Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya chama hicho, miongoni mwa tuhuma zinazomkabili kiasi cha kuomba kujiweka kando kwa muda kupisha achunguzwe ni madai ya matumizi mabaya ya ofisi ikiwamo kujimilikisha mashangingi ya chama hicho
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amemuandikia barua mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe, akiomba kuundwa kwa tume ya kuchunguza tuhuma zinazomkabili zilizodaiwa kutolewa na wajumbe wa kamati kuu.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya chama hicho, miongoni mwa tuhuma zinazomkabili kiasi cha kuomba kujiweka kando kwa muda kupisha achunguzwe ni madai ya matumizi mabaya ya ofisi.
Katika tuhuma hiyo, Mwalimu anadaiwa kujimilikisha magari ya kifahari mashangingi mawili yaliyodaiwa kutolewa na mmoja wa wadau kwa ajili ya kukisaidia chama. Mashangingi hayo yaliyotumika kwenye kampeni za uchaguzi mkuu 2025 inadaiwa moja amejimilikisha na lingine ameliuza.
Jana, taarifa zilizozua mjadala mkubwa mitandaoni zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chaumma walipiga kura ya kutokuwa na imani na Mwalimu, wakimtuhumu kwa kufanya uamuzi binafsi bila kufuata taratibu za chama.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, waraka uliosainiwa na wajumbe hao uliwasilishwa katika kikao cha kamati kuu kilichofanyika jana na kuhitimishwa saa tano usiku.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la kuandaa hoja zitakazowasilishwa mbele ya Halmashauri Kuu, itakayotoa uamuzi wa mwisho kwa kupiga kura ya ndiyo au hapana kuhusu hoja zote zitakazowasilishwa.
Sababu zingine zilizochangia wajumbe kumkalia kooni na kupiga kura ya kutokuwa na imani naye ni madai kwamba amekuwa akifanya uamuzi binafsi na kutoa maoni yake kama misimamo rasmi ya chama bila kuyapitisha katika vikao husika.
Miongoni mwa maoni yanayodaiwa kutokuwa msimamo rasmi wa Chaumma ni pamoja na kuipongeza na kuisifia Tume ya Uchunguzi wa Ghasia za Oktoba 29, 2025. Msimamo huo unadaiwa kuwagawa wanachama wa chama hicho katika makundi mawili.
Sababu nyingine inayotajwa ni madai ya ubadhirifu wa fedha. Hoja hiyo iliwahi kujadiliwa katika kikao kati ya viongozi wa chama na makatibu wa mikoa mapema mwaka huu, ambapo kulikuwa na madai ya matumizi yasiyoeleweka ya fedha zilizotengwa kwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Katika barua ya Mwalimu aliyoiwasilisha leo, Juni 30, 2026, kwa Mwenyekiti wa Chaumma Hashim Rungwe, Mwalimu amesema:
"Nakuandikia barua hii kama rejea rasmi ya ombi langu nililowasilisha mbele ya kikao cha kamati kuu kilichofanyika Juni 29, 2026, jijini Dar es Salaam, kuhusu kamati kuu kuunda timu ya kuchunguza tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wajumbe dhidi yangu. Kama nilivyotamka katika kikao hicho, niko tayari kujibu tuhuma zozote zitakazothibitika na kuwajibika ipasavyo."
Ameongeza kuwa, kwa masilahi ya uchunguzi huo, atajiondoa kwa muda katika majukumu yake ya ofisi ili kutoa nafasi ya uchunguzi huru hadi suala hilo litakapokamilika.
"Iwapo utaridhia, nakaimisha nafasi ya Katibu Mkuu kwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Mheshimiwa Benson Kigaila," amesema Mwalimu.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara, Benson Kigaila amesema hatima ya Mwalimu kuhusu kukataliwa au kutokataliwa na wajumbe itafahamika baada ya mchakato wa ndani wa chama kukamilika.
Mwananchi ilizungumza na Kigaila, ambaye jana hakuweza kuzungumza kutokana na kuongoza kikao cha kamati kuu baada ya Mwalimu kudaiwa kuingia mitini kwenye kikao hicho kufuatia kujitetea dhidi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Akizungumzia suala hilo, Kigaila amesema mchakato bado haujakamilika, hivyo si sahihi kutoa hitimisho kabla Halmashauri Kuu haijafanya uamuzi wake.
"Hoja unayoieleza bado ipo kwenye vikao vya chama na mchakato wake haujakamilika. Si busara kuizungumzia kwa undani kwa sababu Halmashauri Kuu, ambayo ndiyo yenye uamuzi wa mwisho, bado haijapiga kura ya kuridhia au kukataa," amesema.
Amesema kutokana na uzito wa uamuzi wa Halmashauri Kuu, matokeo ya mchakato huo yatawekwa hadharani baada ya kikao hicho kumalizika jioni ya leo.
"Jioni ya leo baada ya kikao cha Halmashauri Kuu tutasema kama Mwalimu amekataliwa au hajakataliwa, ikiwa amekataliwa tutakuja na suluhu Kwa sasa, tuache mchakato wa ndani wa chama uendelee na tuheshimu taratibu zake," amesema.
Alipoulizwa kuhusu taarifa zinazomtaja kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kurithi wadhifa wa katibu mkuu endapo Mwalimu ataondolewa, Kigaila amekataa kuzungumzia suala hilo.
"Siwezi kusema chochote kwa sasa. Mchakato wa vikao vya ndani bado haujakamilika. Naomba tuheshimu taratibu za chama; ukweli wote utajulikana baada ya mchakato kukamilika," amesema Kigaila.
Mwananchi inaendelea kumsaka Mwalimu kuhusu ukweli ya mdai ya kukataliwa kwake kila akitafutwa kwa simu haipatikani.