Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Salum Mwalimu yamemkuta Chaumma, hawamtaki

Muktasari:

  • Mambo yamekwenda vibaya kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, baada ya baadhi ya makada wa chama hicho kutokuwa na imani naye.



Dar es Salaam. Baadhi ya wajumbe wa sekretarieti na Kamati Kuu ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), wamepiga kura ya kutokuwa na imani na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, kwa madai kuwa, amekuwa akijiamulia mambo.

Waraka uliotiwa saini na orodha ya wajumbe waliopiga kura ya kutokuwa na imani na Mwalimu, umewasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kinachoendelea leo Jumatatu Juni 29, 2026, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mwananchi kwa nyakati tofauti limemtafuta Mwalimu ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 alikuwa mgombea urais, hakupatikana kwani simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa.


Waliosaini kumkataa

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chaumma ambaye ni mmoja wa waliotia saini waraka wa kutokuwa na imani naye, Aisha Madoga, amekiri kusaini waraka huo, akisema sababu ni mwenendo usioridhisha wa Mwalimu.

Miongoni mwa matendo ambayo hawaridhishwi nayo, amesema ni tabia ya kupindisha maudhui ya misimamo na mapendekezo ya vikao vya juu vya chama hicho, akiegemea upande wa Serikali.

“Ujue vikao vya Chaumma havikuwahi kuipongeza Tume ya Uchunguzi wa Ghasia za Oktoba 29, lakini yeye akatoka kwenye vyombo vya habari anasema vitu tofauti na tulivyokubaliana. Kila mambo anachosema si msimamo wa chama,” amesema.

Alipoulizwa ni mambo yepi hasa aliyozungumza kinyume na yaliyokubaliwa, amesema ni suala la kuipongeza Tume ya Uchunguzi wa Ghasia za Oktoba 29.

“Ujue kamati kuu ililaani matukio ya Oktoba 29, lakini yeye akienda kwenye vyombo vya habari anaongea tofauti. Sisi siyo wakala wa Serikali yeye anaongea kwa niaba ya chama na anaongea maoni yake binafsi,” amesema.

Amesisitiza wameamua kufanya hivyo kwa kuwa hawaridhishwi na matendo yake, vinauchafua uongozi na chama hicho kwa ujumla.

“Kama kuna maslahi anayapata ni yeye, sisi tunachotaka misimamo tunayotoa mbele ya vyombo vya habari ikatamkwe kama ilivyo, sio kupindisha kabisa mambo,” amesema.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mambo ya Uchaguzi wa chama hicho, Kangeta Kangeta, naye amekiri kutia saini waraka huo bila kufafanua kwa kina.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkurugenzi wa Uchumi, Fedha na Mipango wa Chaumma, Catherine Ruge, amesema hakuwepo kwenye kikao, lakini angekuwepo, angekuwa miongoni mwa waliopiga kura ya kutokuwa na imani na Mwalimu.

Amesema hamuungi mkono Mwalimu kwa sababu amekuwa akijiamria mambo na kutoa taarifa zinazoenda kinyume na misimamo ya chama.

Pia, amesema kiongozi huyo amekuwa akiwazuia wanachama kutofautiana mitazamo na misimamo na Serikali, mambo ambayo si kinyume na dhamira zao za kujiunga na chama hicho.

“Sisi tuliondoka Chadema kwa sababu hakukubaliana mambo fulani, tumeenda Chaumma tukijua kabisa kuwa tutabaki na misimamo yetu na tutakuwa na nguvu ya kutoa maoni hata kama hayatafanyiwa kazi na Serikali,” amesema.

Amesisitiza Mwalimu bila vikao amekuwa akijiamulia kwenda kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mambo ambayo ni kinyume na misimamo ya chama hicho.


Wengi hawamtaki

Kwa mujibu wa moja ya chanzo cha kuaminika ndani ya chama hicho kimesema ni kweli baadhi ya wajumbe wamewasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Katibu Mkuu, Salum Mwalimu, wakieleza kutoridhishwa na mwenendo wake wa uongozi.

Amesema wajumbe wengi wana msimamo wa kutomtaka Mwalimu aendelee kushika wadhifa huo, wakidai amekuwa akifanya maamuzi binafsi bila kuzingatia misimamo ya chama.

Kwa mujibu wake, hali hiyo imejidhihirisha kuanzia nje na hata wakati wa kikao husika, ambapo wajumbe wengi walionyesha kutokuwa tayari kuendelea kumuunga mkono.

Amesema Mwalimu amekuwa akilalamikiwa kwa muda mrefu kwa madai ya kukihujumu chama, pamoja na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za taasisi, hata baadhi ya wananchi wamekuwa wakieleza kutoridhishwa na aina ya uongozi uliopo, wakidai Katibu Mkuu amekuwa akiharibu taswira ya chama.

"Wajumbe wengi wameazimia kumuondoa, na mwishoni wanataka mkutano wa Halmashauri Kuu uliopangwa kesho ukapige kura ya kutokuwa na imani naye na uamuzi huo ukaungwa mkono. Kwa sasa, matarajio ya wengi ni kwamba nafasi hiyo inaweza kujazwa na Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama, Benson Kigaila," amesema.

Hata hivyo, vyanzo vya ndani ya kikao vinaeleza Mwalimu aliondoka kikaoni hapo kabla hakijaisha na hivyo Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila akapewa usukani wa kukiongoza.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Kigaila alijibu yupo kikaoni hivyo asingeweza kuzungumza. Hata mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe, naye alipokea lakini hakusikika akizungumza.

Vyanzo vya ndani vinaeleza ikiwa Mwalimu atawekwa kando, nafasi hiyo huenda ikaangukia kwa Kigaila.