Rais Mwinyi kupokelewa kishujaa Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Muktasari:

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alichaguliwa na mkutano mkuu wa chama hicho Desemba 7, 2022 kuwa makamu mwenyekiti wa CCM – Zanzibar kwa kupata kura 1912 kati ya kura 1915 zilizopigwa baada ya mtangulizi wake, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kumaliza kipindi chake cha miaka 10.

Zanzibar. Siku chache baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM taifa kumchagua Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar, ameandaliwa mapokezi makubwa na wanachama Desemba 11, 2022 kisiwani humo.

Dk Mwinyi alichaguliwa na mkutano mkuu wa chama hicho Desemba 7, 2022 kwa kupata kura 1912 kati ya kura 1915 zilizopigwa baada ya mtangulizi wake, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kumaliza kipindi chake cha miaka 10.

Katika mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili; Desemba 7 na 8 jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM Taifa huku Abdulrahman Kinana akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.

Akizungumza kuhusu mapokezi hayo na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya CCM, Kisiwandui mjini Unguja leo Ijumaa Desemba 9, 2022, katibu wa itikadi na uenezi wa kamati maalumu ya CCM Zanzibar, Catherine Nao amesema Dk Mwinyi atapokewa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume saa 8:00 asubuhi.

“Msafara wake utapita Kiembesamaki, Mazizini kupitia Kilimani chini, Magereza, Kariakoo, Kisonge hadi Ofisi kuu ya Chama cha Mapinduzi Kisiwandui,” amesema

Kwa Mujibu wa Nao, baada ya kufika Kisiwandui, atapokewa na Sekretarieti na wazee wa CCM, ataingia kusaini kitabu kwenye ofisi yake kisha kwenda kwenye kaburi la muasisi wa Mapinduzi na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume ambalo lipo kwenye viwanja vya ofisi hizo.

Akieleza sababu za kufanya mapokezi makubwa kiasi hicho, Nao amesema mbali ya kwamba Dk Mwinyi anaingia awamu ya kwanza ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, bali wajumbe wameonyesha imani kubwa kwake.

Mbali na sababu hizo, pia amesema huo ni mkakati maalumu wa kujipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 “tunaamini anakuja kufanya kazi kwenye chama na kuiongoza CCM Zanzibar, kuweka mipango thabiti na kutengeneza sekretarieti kuelekea mwaka huo.”

Naye mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM wilaya ya Mjini na wilaya ya Amani, Rashid Simai Msaraka amesema kwa Zanzibar ni mara ya kwanza kufanya mapokezi ya makamu mwenyekiti wa CCM aliyezaliwa baada ya mapinduzi.

Msaraka ambaye pia ndiye mkuu wa wilaya ya Mjini, amesema wamejipanga kufanya mapokezi hayo ya aina yake huku akiwaomba wananchi wote wajitokeze katika viunga vyote atakapopita kumpokea.