CCM mpya ya Samia

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wajumbe wa mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho, jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Miongoni mwa mambo yanayoikabili safu mpya ya uongozi ni kukivusha chama katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Dodoma. Ni CCM ya mabadiliko ya kukiboresha chama, ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mkutano Mkuu kuridhia mapendekezo yaliyotolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Mkutano huo uliofanyika jana chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan, umehusisha mabadiliko ya katiba kwa kurejesha kofia mbili za uongozi, kuongeza wajumbe wa NEC wa kapu kutoka 30 kwa pande zote (Bara na Zanzibar) ambapo kila moja itatoa wajumbe 20.

Pia, mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia ndani ya CCM ni kuongeza wajumbe wa NEC wa kapu kutoka 30 hadi 40, makatibu wa mikoa 32 wamerejeshwa NEC, uteuzi kwa wajumbe wa NEC umeongezeka kutoka sita hadi 10.

Aidha, wajumbe wameongezeka na kufikia 1,934.

Mabadiliko mengine ni makatibu wenezi wa mikoa sasa kuajiriwa badala ya kuchaguliwa. Ikiwa na maana wataweza kupata watu wenye taaluma ya eneo hilo.

Wakati wa uenyekiti wa John Magufuli (aliyekuwa Rais wa awamu ya tano) wajumbe NEC walipungua kutoka 388 hadi 158, wajumbe wa Kamati Kuu walipungua kutoka 34 hadi 24.


CCM mpya ya Samia

Katika chaguzi zilizofanyika ndani ya chama hicho, wagombea wengi wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ambao ni zaidi ya milioni mbili tofauti na ilivyokuwa awali.

Idadi ya wagombea wa NEC pia iliongezeka ambapo waliojitokeza walikuwa 2,703, idadi ambayo haijawahi kutokea huko nyuma, huku waliopitishwa wakiwa 374.

Aprili 1, 2022 CCM iliitisha Mkutano Mkuu Maalumu kufanya marekebisho ya katiba yake kwa kuwapa majukumu wajumbe wa NEC, kuwarejesha kwenye NEC makatibu wa mikoa na kutoa fursa kwa kofia mbili kuwepo katika uongozi wa juu.

Hayo yalikuwa mabadiliko ya 17 ya ndani ya chama hicho kilichoanzishwa mwaka 1977.

Mabadiliko ya mwisho yaliyofanyika mwaka 2017 chini ya Rais John Magufuli yaliwapunguza wajumbe kwenye vikao vya juu vya chama kwa lengo la kupunguza gharama na sababu nyingine ambazo hazikuwekwa wazi.


Sababu za mabadiliko

Mabadiliko hayo yaliwarejesha kwenye NEC makatibu wa CCM wa mikoa na wale waliokuwa wanachaguliwa kupitia wilaya walioondolewa katika mabadiliko ya 2017.

Taarifa kutoka ndani ya CCM, zilibainisha kuondolewa kwa makatibu hao kulitengeneza udhaifu wa utekelezaji wa maagizo yanayotolewa na NEC, kwa kuwa baadhi ya wenyeviti walikuwa ama hawayafikishi kwa makatibu wao, huyafikisha kwa kuchelewa na au kwa tafsiri isiyo sahihi.

“Makatibu wa mikoa ambao ndio watendaji wa chama kwenye maeneo yao, mara kadhaa wameshindwa kutekeleza maagizo ya NEC na kudhoofisha shughuli za chama kwa kuwa hawakuyapata kwa usahihi au hayakufika kabisa, kilisema chanzo cha Mwananchi.

Mabadiliko mengine yaliyofanyika ni kuongeza wajumbe waliokuwa na kofia mbili kama vile wabunge au mawaziri na wajumbe wa NEC.

Nafasi nyingine ni kuwatambua makatibu wa jumuiya kuwa wajumbe wa halmashauri kuu, nafasi ambazo hazikuwepo awali na wajumbe walipitisha mabadiliko hayo kwa kura za ndiyo.


Mitazamo tofauti

Mabadiliko hayo yamekuwa na mitazamo tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali, ambapo Wakili Alute Mughwai alisema kila jambo linalofanyika ndani ya chama hicho lina mtazamo wa kukipeleka mbele, ingawa kunahitajika mjadala wa tathimini.

Mughwai, ambaye ni kaka yake na Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu alisema kuongeza idadi ya wanachama kuwa viongozi inakuwa na sura mbili ama ya kuongeza jeshi kwenye vita ya kisiasa, lakini kama hawatakuwa na ubora ni mzigo.

Wakili huyo aliomba uwepo mjadala mpana ndani ya CCM kuhusu faida zitakazotokana na wingi wa wajumbe na kama wangebaki wachache kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa awamu ya tano.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John’s Fredrick Golden, alisema umoja na mshikamano ndani ya chama hicho ndiyo nguzo, lakini akatahadharisha viongozi ambao wamekuwa wasemaji nje ya vikao rasmi kwamba wanakiumiza chama.

Golden alisema kukosoana siyo jambo baya, lakini inategemea linakosolewa mahali gani na kwa wakati upi ili watu watambue ukweli na hivyo akataka uwepo umakini mkubwa wakati wa kuchagua viongozi, maana wingi wao unaweza kuwa tatizo.

“Wakitaka kusema mambo yao wakutane ndani ya vikao ambako kuna nafasi ya kusema na kukosoa, siyo kukurupuka na kusema mambo akiwa nje, huo siyo utaratibu, kwani wanakigawa chama,” alisema Golden.

Mchambuzi masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Kahangwa alisema, “yawezekana katika vikao vyake vya kawaida vya CCM, imeona kuna haja ya mabadiliko na hadi wanafikia hivyo, wameweza kuwashawisha wajumbe juu ya umuhimu wa mabadiliko hayo.

“Ukiongeza wajumbe inakuwa ni gharama, bila shaka CCM imepima na kuona inaweza kumudu gharama na majukumu yao yanaweza kuongezeka. Kama itawaelemea,” alisema.

Akijibu swali aliloulizwa mabadiliko hayo ni kuundwa kwa CCM mpya, Mhadhiri huyo wa UDSM alisema majibu ya moja kwa moja wanayo CCM wenyewe, “lakini Mzee Mwinyi aliwahi kusema kila zama na kitabu chake, sasa yawezekana kama ni CCM ya Samia ni kitabu chake.”

…wakosoaji

Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano mkuu wa 10 uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma alisema wanaokosoa Serikali yake katika utekelezaji wa Ilani, wanapaswa kumtazama katika bajeti mbili.

Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho kumekuwa na ukosoaji wa wanachama kutoka ndani ya CCM na nje ya chama hicho kuhusu kinachoendelea ndani ya Serikali ya awamu ya sita.

Hata hivyo, hakuzitaja moja kwa moja bajeti ambazo aliomba kupimwa nazo, licha ya kuwa katika uongozi wake bajeti ya kwanza ni ile ya 2021/22 na 2022/23 ambayo ipo kwenye utekelezaji, huku akichukulia kota ya mwisho katika bajeti ya 2020/21.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua Mkutano mkuu wa 10 wa CCM Jijini Dodoma ambapo alikiri kuwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unatazama kipindi cha miaka mitano, lakini kwake yeye na wenzake anaomba wapimwe katika bajeti ya miaka miwili.

Kiongozi huyo aliingia madarakani Machi 19, mwaka jana baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Serikali ya awamu ya tano, John Magufuli aliyefariki Machi 17 2021, jijini Dar es Salaam.

Tangu aliposhika kijiti cha uongozi, amekutana na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya viongozi wenzake, jambo linalotajwa kuwepo na mgawanyiko wa ndani ya chama licha ya CCM kutokubaliana na kauli hiyo.

Akiwa na miezi 10 madarakani, Rais Samia alitofautiana na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alizungumzia suala la ukopaji madeni makubwa huku akienda mbali zaidi kuwa iko siku nchi itauzwa.

Kauli ya Ndugai ilionekana kutomfurahisha Rais Samia na wanachama wengine ndani ya chama hicho hata wakapelekea kuwepo kwa shinikizo la kutaka kiongozi huyo wa mhimili ajiuzulu na akafanya hivyo.

Maoni ya Ndugai yalitafsiriwa kama usaliti ndani ya chama na kiongozi huyo ambaye aliingia na kauli ya Kazi Iendelee ikiwa na maana ya kuendeleza miradi mikubwa iliyoanzishwa na mtangulizi wake, John Magufuli.

Mbali na Ndugai, aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali hivi karibuni aliingia kwenye mgogoro ambao bado unafukuta baada ya kuwafunga midomo wanaotumia kauli ya kumsifia Rais kuwa ameupiga mwingi.

Katika baadhi ya maeneo, Dk Bashiru alizungumzia kauli ya ‘kuupiga mwingi’ akisema haina afya kwa mustakabali wa kujenga siasa au kumsaidia Rais, licha ya kushindwa kueleza wafanye nini kumsifia.

Wengine ambao wamekuwa wakitoa kauli za kukosoa kwenye mitandao ni mbunge wa Nzega Vijiji, Dk Hamisi Kigwangala na mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina ambao hata hivyo hawatajwi kumkosoa moja kwa moja, bali huwakosoa wateule wake.


Atoa ruksa

Juzi Rais Samia hakuzuia kuhusu ukosoaji, lakini alichotaka ni wanaotoa kauli hizo kujikita kwenye utekelezaji wa alichokisimamia kwenye uongozi wake.

Akihutubia jana wajumbe 1,928 na wageni wengine, kiongozi huyo alisema utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ambao ndiyo mkataba baina yao na wananchi unakwenda vizuri kwa pande mbili za muungano na kuahidi kuendeleza umoja na mshikamano ili waweze kuisimamia vema miradi.

Lakini, kiongozi huyo alibainisha bila mshikamano na umoja wa ndani ya chama hicho, utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na usimamizi wa miradi ndani ya Serikali utakuwa ni mgumu, hivyo ni wajibu wa kila mwanachama kusimama kwa nguvu moja katika jambo hilo.

Kutokana na hilo, Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema imeonyesha jinsi ambavyo viongozi hawapendi kukosolewa.

“Hakuna kiongozi anayepokea ukosoaji kwa moyo mweupe. Tangu Mwalimu (Julius) Nyerere alikuwa akikosolewa na nadhani mtu aliyevumilia zaidi kukosolewa alikuwa ni Mwinyi (Rais Ali Hassan), alikosolewa mpaka na wastaafu.

“Hata (Rais mstaafu Jakaya) Kikwete naye alivumilia ukosoaji, lakini Mkapa (Rais mstaafu Benjamin) na (Rais) John Magufuli hawakupenda kabisa kukosolewa,” alisema.

Kuhusu Rais Samia, alisema licha ya awali kuwahamasisha watu waongee, ameonekana kutovumilia.

“Kwa hiyo tafsiri ninayoipata hapa ni kwamba Rais Samia naye kama kiongozi inawezekana hapokei ukosoaji vizuri,” alisema.