Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saini ya Mnangagwa kurefusha muda wa urais mjadala Zimbabwe

Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.

Muktasari:

  • Upinzani nchini Zimbabwe umeapa kupinga sheria mpya iliyosainiwa na Rais Emmerson Mnangagwa inayoongeza muda wa utawala na kuhamisha mamlaka ya kumchagua rais kwa Bunge, ukidai kuwa inakiuka Katiba.

Dar es Salaam. Mvutano wa kisiasa umeongezeka nchini Zimbabwe baada ya Rais Emmerson Mnangagwa kusaini sheria ya marekebisho ya Katiba inayoongeza muda wa utawala wa viongozi wa sasa na kubadili utaratibu wa kumpata mkuu wa nchi, hatua iliyozua upinzani kutoka kwa vyama vya upinzani vinavyodai kuwa inahatarisha misingi ya demokrasia.

Sheria hiyo ilisainiwa Julai 7, 2026, baada ya kupitishwa na Bunge linalodhibitiwa na chama tawala cha Zanu-PF.

Marekebisho hayo yameibua maandalizi ya maandamano na hatua za kisheria, huku muungano mpya wa upinzani wa People's Coalition ukitangaza kutumia njia zote za kikatiba kupinga mabadiliko hayo.

Wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wa haki za binadamu wanasema marekebisho hayo yanaweza kuimarisha zaidi ushawishi wa chama tawala na kupunguza ushindani wa kisiasa, wakati Serikali ikiyatetea kuwa yanalenga kuimarisha utulivu wa kisiasa na mwendelezo wa uongozi nchini humo.

Mawakili wa muungano huo wamesema wanajiandaa kufungua kesi katika Mahakama ya Katiba wakidai mchakato wa kufanya marekebisho hayo haukufuata matakwa ya Katiba.

"Wakati muswada sasa umekuwa sheria, hilo halimaanishi kuwa ni halali au hauwezi kupingwa. Tunaamini mchakato uliotumika kubadili Katiba haukufuata sheria," amesema wakili wa haki za binadamu, Doug Coltart.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyofanywa na sheria hiyo mpya ni kuongeza muda wa muhula wa rais na wabunge kutoka miaka mitano hadi saba.

Hatua hiyo inampa Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83, fursa ya kuendelea madarakani kwa miaka miwili zaidi baada ya muhula wake wa sasa kumalizika mwaka 2028.

Marekebisho hayo pia yameondoa utaratibu wa wananchi kumchagua rais kwa kura ya moja kwa moja na badala yake yanatoa mamlaka kwa Bunge kumteua rais, mfumo ambao haujawahi kutumika nchini humo tangu mwaka 1987.

Upinzani umesema hatua hiyo inakiuka Katiba na kudhoofisha misingi ya demokrasia, huku ukidai mashirika ya kimataifa, yakiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, yanafahamu kinachoendelea nchini humo.

Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa chama tawala wamepongeza sheria hiyo wakisema italeta utulivu wa kisiasa na kuhakikisha sera za maendeleo zinaendelea bila kuyumbishwa na uchaguzi wa mara kwa mara.

Mnangagwa aliingia madarakani mwaka 2017 baada ya jeshi kumwondoa madarakani aliyekuwa Rais Robert Mugabe, aliyekuwa ameiongoza Zimbabwe kwa miaka 37.

Serikali yake imekuwa ikisisitiza kuwa marekebisho hayo yanalenga kuimarisha uthabiti wa kisiasa, lakini wakosoaji wanaona ni mkakati wa kuendeleza utawala wa Zanu-PF na kupunguza ushindani wa kidemokrasia nchini humo.

Mvutano huu unaibuka huku mashirika ya haki za binadamu ya ndani na kimataifa, pamoja na wanaharakati na wachambuzi wa siasa, wakionya kuwa hatua hiyo inaweza kuchochea mgawanyiko katika Taifa hilo.

Mjadala wa muswada huo ulianza rasmi Februari mwaka huu baada ya kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali kama Muswada wa Marekebisho ya Katiba Na. 3 wa mwaka 2026.

Hata hivyo, mchakato huo uliendelea hadi ulipopitishwa na Bunge la Seneti Jumatano, Juni 24, 2026, kwa kura 75 za ndiyo dhidi ya nne za hapana, baada ya kupitishwa pia na Bunge la Taifa Juni 18 kwa kura 216 dhidi ya 42, zaidi ya theluthi mbili zinazohitajika kufanya marekebisho ya Katiba.