Samia: Wanaowatisha wasithubutu, tokeni mkapige kura
Muktasari:
- Mgombea huyo ameonya wanaotisha watu ili wasijitokeze Oktoba 29, 2025 siku ya Uchaguzi Mkuu na kueleza kuwa wamejipanga vizuri, wananchi wasiogope wajitokeze kwenda kupiga kura.
Simiyu. Mgombea Urais wa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewatoa hofu Watanzania akiwataka wajitokeze kupiga kura Oktoba 29, 2025 huku akiwaonya wanaotisha watu.
Samia ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa onyo hilo leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Bariadi Mjini mkoani Simiyu.
"Niwatoe hofu kuna watu wanatishatisha ili kuwafanya watu wasitoke Oktoba 29, nataka kuwaambia ninayezungumza hapa ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii, nataka kuwaambia wasithubutu kibati tu kikipasuka sisi tuko nao," amesisitiza.
"Tumejipanga vizuri tokeni kapigeni kura rudini nyumbani mkapumzike hakuna hofu, hakuna kuogopa tokeni mkapige kura," amesema na kuongeza...
"CCM tumedhamiria kufanya kazi, tumefanya kazi mmeiona na tunajiamini kwamba tutaweza tena kufanya kazi kipindi cha pili cha awamu ya sita kazi ya kuonekana, niombe mtuchague CCM," amesema.
"Niwatoe hofu kuna watu wanatishatisha ili kuwafanya watu wasitoke Oktoba 29, nataka kuwaambia ninayezungumza hapa ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii, nataka kuwaambia wasithubutu kibati tu kikipasuka sisi tuko nao tumejipanga vizuri tokeni kapigeni kura rudini nyumbani mkapumzike hakuna hofu, hakuna kuogopa tokeni mkapige kura," amesema.
Aidha amesema kupitia reli ya kisasa ya SGR inayojengwa jijini Mwanza itapita Simiyu katika baadhi ya maeneo na kuwa itakuwa na vituo vya kushusha na kupakia abiria hivyo ni fursa za kiuchumi kwa vijana," amesema Samia.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa Jimbo la Nzega, Hussein Bashe amewaomba wananchi kukichagua chama hicho ili waendelee kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kwa wakulima.
"Wakulima wa hapa Simiyu, pamba ilikuwa Sh500 na ilikuwa hainunuliwi katika msimu wa mwaka 2020/2. Mwaka huu pamoja na kuanguka bei ya soko la dunia wakulima wameuza Sh1,200 na hawajakatwa. Katika kipindi cha miaka minne mkoa umekuwa na viwanda vinne vya kuchakata pamba," amesema.
Mwenyekiti wa Wafugaji Tanzania, Mrida Mshota amesema katika kipindi cha miaka minne wafugaji wote nchini wamepatiwa chanjo ya mifugo ya thamani ya Sh69 bilioni na kuhakikisha mifugo yote nchini inachanjwa.
Mwenyekiti huyo amesema mikoa mitatu inayoongoza kuwa na mifugo mingi nchini ni Arusha, Kagera na Simiyu ambapo kwa mkoa wa Simiyu una ng'ombe milioni 2.53 na katika miaka minne ya Samia maofisa ugani 80, pikipiki 77 zimepelekwa mkoani humo kwa ajili ya kusaidia wafugaji.
"Awali tulikuwa tunakamatiwa mifugo inapigwa minada ila tangu mwaka 2021 hatuna kesi ya mifugo kukamarwa hifadhini, wafugaji Kanda ya Ziwa na Tanzania mwaka huu wanakuchagua kwa kura nyingi na hatuangalii kelele zinazopigwa na wachache, hatutakubali mambo ya kihuni katika nchi yetu," amesema.
Aidha katika mkutano huo, wanachama 30 kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na aliyekuwa Katibu wa Bavicha Wilaya ya Bariadi, Bwinini Masunga wamehamia CCM.
"Kutokana na mazuri aliyofanya Rais Samia mimi kama kijana nimeona hakuna haja ya kuumizana kwenye maandamano, naomba vijana tunaojitambua tuwe wamoja, taifa lolote linalofanya mabadiliko ya kimaendeleo linategemea nguvu ya vijana," amesema.