Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SAU yakomaa na kilimo

Mwenyekiti wa Chama cha Umma (SAU), Bertha Mpata, akikabidhi Ilani ya uchaguzi kwa mgombea urais wa chama hicho, Majalio Kyara na mgombea mwenza wake, Satia Bebwa, wakati wa uzinduzi wa kampeni za kitaifa uliofanyika leo Septemba 9,2025 viwanja vya Ukonga Mombasa, Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Chama cha Sauti ya Umma (SAU), kimezindua ilani yake ambayo imeainisha vipaumbele vitatu vinavyokwenda kutekelezwa

Dar es Salaam. Chama cha Sauti ya Umma (SAU), kimezindua rasmi kampeni zake za uchaguzi mkuu huku  mgombea urais kupitia chama hicho, Majalio Kyara akiahidi kusimamia kilimo hai ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Akizungumza katika uzinduzi huo leo Jumanne Septemba 9, 2025, katika Viwanja vya Ukonga Mombasa, Dar es Salaam Kyara amesema kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa,  hivyo kimepewa kipaumbele cha pekee katika ilani ya chama chao.

“Tunataka tukipe umuhimu kilimo kama damu ilivyo kwenye miili yetu, kwa kuwa kupitia kilimo tunaweza kutatua matatizo mengi yanayoikabili nchi. Tunataka wananchi wale chakula bora na siyo bora chakula. Hivyo, kilimo kisichotumia kemikali kitasaidia kujenga afya njema kwa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.

Kuhusu viwanda, Kyara amesema Tanzania imejaliwa kuwa na ardhi nzuri na rasilimali watu wenye nguvu, hivyo kuna kila sababu ya kuanzisha kongani za viwanda zitakazotumia malighafi za ndani.

“Kwa namna Mungu alivyotuumba, Tanzania inaweza kuilisha siyo tu nchi yetu, bali hata Afrika nzima,” amesema mgombea huyo wa urais.

Kukuza vipaji

Kyara amegusia changamoto ya ajira akiahidi kama atapatiwa ridhaa ya kuongoza Serikali, ataanzisha mfumo madhubuti wa kutambua na kukuza vipaji vya vijana kwa manufaa ya Taifa.

Ametoa mfano wa kijana aliyemaliza kidato cha sita na kujitolea kufundisha wenzake na zaidi ya wanafunzi 100 walipata alama ya ‘A.’

“Kijana huyo ni mfano wa kipaji cha kipekee kilichopewa na Mungu kwa ajili ya kusaidia wengine. Hivyo sisi tunakwenda kulea na kukuza vipaji kama hivyo kwa manufaa ya taifa,” amesisitiza.

Aidha, amesema chama chake kitahakikisha miradi mikubwa ya uwekezaji nchini inashirikisha Watanzania kwa umiliki wa hisa zisizopungua asilimia 30 ili wananchi wawe sehemu ya kunufaika na rasilimali zao.

“Huwezi kufanikisha maendeleo ya nchi yako bila uchumi kushikwa na wazawa. Tunakwenda kuimarisha mfumo wa uchumi unaowawezesha Watanzania kuwa wamiliki wa Taifa lao,” amesema.

Maadili na uadilifu

Kyara pia, amesisitiza umuhimu wa kurejesha misingi ya maadili na uadilifu serikalini, akisema Taifa linahitaji watumishi wenye hofu ya Mungu.

“Ukiwa na hofu ya Mungu ni wazi kutakuwa na upendo, haki na uadilifu. Hakutakuwa na dhuluma, bali kila mmoja atauliza namna anavyoweza kumhudumia Mtanzania kwa uaminifu,” ameeleza.

Mgombea mwenza wa chama hicho, Satia Bebwa amewaomba wananchi kuwachagua kwa miaka mitano ijayo kwa kuwa sera zao ni tofauti na za vyama vingine na zinaweza kutekelezeka kwa uhalisia.

Awali, Makamu Mwenyekiti Bara wa SAU, Johnson Bayo  alibainisha vipaumbele vitatu vya chama hicho kuwa ni pamoja na kilimo ambacho kitakwenda kuongeza uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara kwa kutumia mbinu bora.

Lakini pia ametaja teknolojia itakayosaidia kuongeza tija hususani katika mavuno.

Bayo amesema kipaumbele cha tatu katika ilani yao ni viwanda.

Amesema Serikali ya SAU itaanzisha viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao, kuzalisha pembejeo za kilimo ndani ya nchi na kuinua kipato cha wananchi.