Shauri kiongozi wa Chadema Geita, lapigwa kalenda
Muktasari:
- Jaji Projestus Kahyoza anayesikiliza kesi hiyo, ametoa amri ya kiongozi huyo kufikishwa mahakamani Jumatatu Julai 20, 2026 saa 6:00 mchana bila kukosa.
Geita. Shauri la Mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Geita, Neema Chozaire lililotarajiwa kusikilizwa leo kwa mara ya kwanza, limekwama baada ya Jeshi la Polisi kushindwa kumfikisha mahakamani kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mawakili wa Serikali kuwa Arusha kwenye mkutano wao.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 14, 2026, wakili wa utetezi, Beatus Emmanuel amesema kutokana na mleta maombi (Chozaire) kutofikishwa mahakamani, Jaji Projestus Kahyoza anayesikiliza kesi hiyo, ametoa amri ya kiongozi huyo kufikishwa mahakamani Jumatatu Julai 20, 2026 saa 6:00 mchana bila kukosa.
Baadhi ya viongozi wa Chadema wakiwa mahakamani wakisubili mwenyekiti wa Chadema jimbo la Geita,Neema Chozaire kuletwa mahakamani,ambapo hata hivyo haikuwezekana baada ya mawakili upande wa utetezi kutofika mahakamani.
“Pamoja na kupeleka wito wa Mahakama wa kutaka mtuhumiwa mwenyewe aje kwa sababu ana kesi mahakamani, mtuhumiwa hajaletwa, kwa hiyo Mahakama kwa misingi kama hiyo haiwezi kusikiliza maombi ya pande mbili pale ambapo upande mmoja umejibu lakini haujaja mahakamani, pia mwombaji wa shauri la jinai hajaja,” amesema.
Leo, Julai 14, 2026 saa 3:30 asubuhi, shauri namba 15077 la mwaka 2026, lililofunguliwa na Chadema Julai 8, 2026 wakiongozwa na Wakili Beatus kupitia hati ya dharura katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, chini ya Naibu Msajili wa Mahakama, Jaji Projestus Kahyoza, limekwama kuendelea baada ya upande wa wajibu maombi kutofika mahakamani.
Chadema kwenye shauri hilo inashinikiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Mwanasheria wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kufika mahakamani na kueleza kwa nini kiongozi huyo anashikiliwa bila kufikishwa mahakamani wala kupewa dhamana.
Wakili wa utetezi anayemtetea Mwenyekiti wa Chadema jimbo la Geita, Neema Chozaire akizungumzia mwenendo wa shauri la kiongozi huyo anayeshikiliwa na polisi tangu Juni 29, 2026.
Wengine walioitwa mahakamani ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC) na Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO).
“Hawa ni watu ambao lazima waunganishwe kwa sababu ndiyo washauri wakuu wa kisheria wa Serikali na jambo tulikuwa tunataka lihojiwe au liamriwe na Mahakama kwamba sheria imetekelezwa kwa kukaa na mtuhumiwa kwa zaidi ya muda uliowekwa kisheria wa saa 24.”
“Pamoja na kupelekwa wito huo, wahusika wote na wakasaini kwa majina mbalimbali, lakini hawajafika mahakamani,”amesema.
Naye, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obadi amesema kitendo cha kutofikishwa mahakamani kwa kiongozi huyo ni ukiukwaji wa sheria za nchi, akiliangushia lawama Jeshi la Polisi huku akitaja juu ya hofu ya viongozi hao pamoja na familia kuhusu hali yake.
Viongozi wa Chadema waliofika Mahakama kuu,masjala ndogo ya Geita, wakiondoka mahakamani baada ya shauri hilo kupangiwa tarehe nyingine.
“Tuna taarifa kwamba Chozaire wakati wanamkamata na baada ya kumkamata alipigwa sana kiasi kwamba hakuweza hata kutembea vizuri. Pia sisi viongozi wenzake, familia pamoja na mawakili wake wananyimwa haki ya kumuona, kila tulipokwenda kumuona hawasemi yuko kituo gani, hawatuambii ana hali gani,”amesema.