Siri muungano wa wapinzani kung’oa vyama tawala Afrika
Muungano wa vyama vya upinzani umekuwa ni silaha ya kukabiliana na vyama vikongwe ambavyo vimeyatawala mataifa yao kwa muda mrefu tangu wakati wa harakati za ukombozi hadi zama hizi za ulimwengu wa kisasa.
Baadhi ya mataifa ya Afrika yameonyesha mfano bora kwa wapinzani kuungana na kufanikiwa kushika dola na kuviondoa madarakani vyama tawala ambavyo vimekuwa madarakani kwa miongo kadhaa.
Hivi karibuni, tumeshuhudia namna wapinzani nchini Botswana walivyoungana na kufanikiwa kukiondoa madarakani chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1966.
Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 30, muungano wa vyama vya upinzani wa Umbrella for Democratic Change (UDC), umeongoza kwa wingi wa viti bungeni na hivyo mgombea wake, Duma Boko, kuwa Rais mpya wa nchi hiyo.
Huko Kenya, kwenye uchaguzi wa mwaka 2022, muungano wa Kenya Kwanza kupitia mgombea wake, William Ruto ulishinda uchaguzi dhidi ya muungano wa Azimio la Umoja ambao mgombea wake, Raila Odinga aliuwa akiungwa mkono na Rais wa wakati huo.
Kadhalika, huko Senegal, mgombea binafsi, Bassirou Faye ambaye alipata nafasi hiyo baada ya kiongozi wa chama cha PASTEF, Ousman Sonko kutoteuliwa kugombea urais kwenye uchaguzi wa Aprili, mwaka huu.
Hata hivyo, Sonko ambaye alitarajiwa kuwa mgombea urais kupitia chama hicho, alimuunga mkono Faye na kufanikiwa kukishinda chama tawala cha Alliance for the Republic (APR) chini ya Rais Macky Sall.
Nchini Tanzania, sheria hairuhusu vyama kuungana, hata hivyo, ushirikiano uliofanyika kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya kuanzishwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), upinzani walipata ushindi mkubwa.
Idadi ya wabunge iliongezeka, kura za mgombea urais aliyeungwa mkono na vyama vingine, Edward Lowassa ziliongezeka hadi kufikia milioni sita na zaidi ya halmashauri 20 ziliongozwa na upinzani, jambo ambalo halikuwepo huko nyuma.
Hata hivyo, wadau wanabainisha ugumu wa vyama vya upinzani kuungana Tanzania wakitaja zuio la kisheria na ubinafsi wa baadhi ya vyama vya siasa. Hata hivyo, wote wanakubaliana kuhusu umuhimu huo.
Mtazamo wa Chadema
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu, wakati akizungumza kwenye kipindi kimoja kinachorushwa na televisheni ya Star Tv, alisema kuungana ni jambo jema, lakini changamoto ni vyama vingine vya upinzani havina uwezo wa kuweka wagombea maeneo mengi nchini.
“Kama vyama vya upinzani vipo kuangalia maeneo ya kuunganisha nguvu si jambo baya, tatizo kuna vyama 19 vilivyosajiliwa, lakini ukiangalia vyenye uwezo wa kuweka wagombea nchi nzima havizidi vinne, CCM na Chadema vina uhakika wa kuweka wagombea kila mahali,” alisema.
“Utakuwa na uhakika ACT Wazalendo wanaweza kuweka wagombea Zanzibar baada ya hapo wengine wako wapi, tuzungumze ukweli, kusema ukweli maeneo ya kuunganisha nguvu ni kidogo,” alisema.
Alieleza kuwa sehemu kubwa ya nchi vyama vinavyoweza kusimamisha wagombea ni CCM na Chadema, huku akieleza wataunganisha na nani wakati hakuna chama kingine cha upinzani kinachojitokeza.
“Hawapo kwenye mikutano na uchaguzi, tutaunganisha nguvu na nani, tatizo vyama vingine haviweki wagombea katika maeneo lakini vinaishi kwenye orodha ya daftari la Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema.
ACT Wazalendo
Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alipendekeza umuhimu wa vyama vya upinzani kuungana katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025 ili kukishinda Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kujenga msingi wa hoja hiyo, alishauri vyama hivyo kuketi pamoja na kuja na mchoro utakaowasaidia kuibuka kidedea kwenye uchaguzi kama walivyofanya mwaka 2015.
Zitto alisema hayo Septemba 25, 2024 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Mbozi mkoani Songwe, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya chama hicho iliyokuwa inalenga maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
“Mkoa wa wenu wa Songwe, mwaka 2025 uligawana nusu kwa nusu kati ya upinzani na CCM, sasa hivi hapa Songwe, vyama vya upinzani tukaeni pamoja tuchore mchoro, tugawane majimbo ili tuinyime CCM kura ya mkoa huu.
“Haya mambo ya kujiingilia kila chama kivyake katika uchaguzi au kujiona bora kuliko mwingine, kujiona bora kuliko mwingine hayatusaidii lolote, badala yake CCM inafaidika,” alisema Zitto.
Zitto alipendekeza sehemu ambayo ACT Wazalendo inaungwa mkono zaidi, basi vyama vingine vya upinzani visiweke mgombea katika eneo hilo ili kuwaondoa CCM madarakani kuanzia ngazi za chini.
“Hii ndiyo kazi tunayoweza kuifanya, sisi hatuwezi kuwa watu wa kurudia mambo yaleyale, kila uchaguzi tunafanya vilevile, vyama kuingia kivyakevyake tukidhulumiwa tunaitisha mikutano na wanahabari tunalalamika, uchaguzi ukiitishwa tunaenda kupambana na walewale.
“Tuacheni ujinga, tukaeni chini tuisafishe CCM na inawezekana, ila hatujifunzi, badala yake tunaongoza kwa kupigana vita wenyewe kwa wenyewe, mambo ya kijinga kabisa,” alisema.
Sakaya afunguka
Akizungumzia muungano wa vyama vya upinzani nchini, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya anasema mara zote ikija hoja ya kuungana, wanaiunga mkono lakini vyama vingine vimekuwa vikikwamisha, huku akikitupia lawama Chadema.
“Chadema wakiungana na CCM wataendana vizuri, kwa sababu vyama vingine hatuthaminiwi, tunaitwa vyama njaa njaa, tupo kwenye vyama vya Msajili wa vyama lakini kwenye mikutano hatupo,” anasema.
Anasema wakiungana na CCM wataendana kwa sababu wamekuwa wakijifungia kufanya vikao vyao vya siri, wakijiona wana mkataba na ajenda nao na vyama vingine vikitazama.
“Chadema wanatumika, kama hatujaangalia maslahi ya wananchi hata tukiungana ni bure na bahati mbaya tunaoungana nao hawako pamoja na sisi, wanaogelea kwenye boti nyingine wanajiona ni chama kikubwa na wanapendwa,” anasema.
Anasema Chadema wanajiona wako mbele siku zote kuliko vyama vingine vya upinzani na kufanya vikao vyao huku akieleza vyama vingi Tanzania vinatanguliza ubinafsi zaidi kuliko kujali changamoto za watu.
“Hatutaki kuunganisha nguvu kukabiliana na adui, tukitaka kuungana wanaingilia, tumeikosa nchi hii 2015 na inaweza kuchukua karne tena, ni Chadema waliharibu, wananchi walikuwa tayari kumleta mgombea mwingine na kumuacha tuliyemuandaa,” anasema Sakaya.
Mwanasiasa huyo anasema vyama vimejawa na ubinafsi kiasi kwamba wanapikwa kwa mafuta yao huku akieleza wamekosa ajenda ya dhati ya kuiondoa CCM madarakani.
“Walikaa vikao na kula sambusa lakini hakuna cha maana walichofanya. Tuna udhaifu na CCM wanajua wakituita wanatupa sambusa na kula kiyoyozi tumemaliza biashara, tunakamatwa na vitu vidogo sana, tumejawa na umimi badala ya utaifa,” anasema.
Dk Slaa afichua tatizo
Kada wa zamani wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa anasema changamoto ya vyama vya upinzani nchini maneno ni mengi kuliko matendo, huku akieleza jamii inataka mabadiliko.
“Mwanasiasa mzuri anajua hakutakiwa kuja na hoja ya kuungana, alitakiwa kuja kutuonyesha hatua walizochukua, kama hawajaonyesha mimi siwaelewi, mwanasiasa yeyote makini hatakiwi kuja kutuonyesha anachofikiri,” anasema.
Dk Slaa, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, anasema wanachotegemea Watanzania waonyeshwe hatua zilizochukuliwa na wamefikia wapi katika mchakato huo.
“Tulitegemea kama kuna vyama vimeonyesha nia watuambie wamefikia hatua fulani na wananchi tuwaunge mkono,lakini muda huu tupo katikati ya Uchaguzi wa serikali za mitaa na wakipoteza kuungana kutakuwa na maana gani,” anasema.
Anasema vyama hivyo vinatakiwa kuonyesha matunda na matendo,huku akieleza watu wanahitaji kuona mabadiliko na hadi sasa wamechelewa kufanya kazi hiyo.
“Tanzania tunakwama kwa sababu maneno ni mengi kuliko matendo kwenye vyama vya siasa, siasa ni matendo,” anasema.
Wanazuoni wafafanua
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema kuungana ni njia nzuri ya kuchukua madaraka huku akitolea mfano hata mwaka 2015 vyama vya upinzani vilikaribia kuchukua madaraka.
“Tatizo Tanzania bado mradi wa kuunganisha vyama mfumo wake haujakaa sawa lakini jambo lenye manufaa, kama Kenya umeshakuwa utaratibu wao wa maisha katika kuendesha siasa,” anasema.
Dk Loisulie anasema jambo lingine kikwazo kwa Tanzania ni aina ya siasa ambapo chama tawala kimejiimarisha zaidi na wanasiasa wenye nguvu wote wanatoka CCM na duru za kisasa zinaeleza kuwa kuna wengine wanatumwa kwenda upinzani kuvuruga.
“Ukawa mwaka 2015, Lowassa angeendelea kubaki tungeanza kuona matunda lakini kilichotokea, hakuipa nguvu ilikuwa kuitaka nafasi ya urais, itikadi bado haijawa na nguvu, watu wakitiswa kidogo wanabadilika,” anasema.
Anasema kuna viongozi waliokuwa wanategemewa upinzani kama Mchungaji Peter Msigwa amehama na sahizi amekuwa akiponda upande aliotoka huku akieleza mtandao wa CCM bado ni tishio na wananufaika nao.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Revocutus Kabobe, anasema vyama vya siasa vya Tanzania kukosa ajenda ya pamoja ni sababu ya kushindwa kuungana.
“Vyama vya upinzani vya mataifa mengine vinafanikiwa kwa kuwa na ajenda, kuiondoa CCM madarakani haiwezi kuwa ajenda ya kuweza kuuza kwa wananchi, kumbuka 2015 kulikuwa na Ukawa na waliunganishwa na Katiba ya wananchi,” anasema.
Anasema kulingana na uzoefu wake, haoni kama vyama vya upinzani nchini vinaweza kuwa na ajenda ya pamoja ya kuweza kuunganisha vyama kuingia kwenye uchaguzi.
“Ajenda si kuondoa chama tawala, mkiondoa na mkishakiondoa mnafanyaje, labda ajenda itokee kesho, lakini hadi sasa matumaini ya kuungana ni madogo na ukizingatia sera yetu hairuhusu vyama kuungana,” anasema.
Dk Kabobe anasema sera ya nchi vyama vikiungana vinapoteza utambulisho wake, tofauti na Kenya wakiungana lakini vyama vyao vya msingi vinaendelea.
“Sheria yetu hata ingeruhusu sioni ajenda inayoweza kuwaunganisha pamoja, tofauti na kusema CCM imekaa muda mrefu tuiondoe, kikubwa vyama vya upinzani vije na ajenda inayogusa maslahi ya wananchi,” anasema.