Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Masisi kutetea kiti chake uchaguzi mkuu Botswana

Uchaguzi mkuu wa Botswana umefanyika Jumatano Oktoba 30, 2024 ambapo wananchi walipiga kura kuamua muundo wa Bunge la 13 la nchi hiyo pamoja na mabaraza ya mitaa kote nchini humo.

Katika uchaguzi huo, jumla ya viti 61 vya Bunge na viti 609 vya mabaraza ya mitaa vinashindaniwa, vyote vikichaguliwa kwa mfumo wa kwanza kushinda.

Wananchi wa Botswana wamepiga kura kuwachagua wabunge, ambao nao watamchagua Rais wa taifa hilo linalosifika kwa kuwa na uchumi imara barani Afrika.

Shughuli ya kujumlisha matokeo na kutangaza washindi katika ngazi ya majimbo inaendelea nchini humo huku chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) kikitarajiwa kushinda viti vingi kwenye uchaguzi huo.

Tangu uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa upigaji kura kwa wote mwaka 1965, BDP kimekuwa na wingi wa viti bungeni bila kukatizwa, na hivyo kimeongoza peke yake kwa miaka 58, hali inayofanya Botswana kuwa nchi yenye mfumo wa chama kimoja chenye nguvu.


Mokgweetsi Masisi

Rais Mokgweetsi Masisi anapewa nafasi kubwa ya kushinda muhula wa pili dhidi ya wapinzani watatu katika taifa hilo ambalo chama chake cha BDP kimeongoza tangu lilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1966. Wapigakura watachagua wabunge wa Bunge la Taifa, ambao nao watamchagua Rais.

Masisi amekuwa Rais tangu mwaka 2018 alipoingia madarakani baada ya kuhudumu kama Makamu wa Rais chini ya mtangulizi wake, Ian Khama. Aliendelea kuwa Rais baada ya chama chake cha BDP kushinda uchaguzi wa mwaka 2019.

Akiwa na umri wa miaka 63, Masisi ni mwalimu wa zamani aliyewahi kufanya kazi katika shirika la watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef), kabla ya kuingia katika siasa. Katika muhula wake wa kwanza, alikabiliana na changamoto ya ukosefu mkubwa wa ajira na ukuaji mdogo wa uchumi kutokana na kupungua kwa mahitaji ya almasi duniani, ambayo Botswana inategemea kiuchumi.

Mwaka jana, Masisi aliungwa mkono baada ya kujadiliana kuhusu mkataba mpya wa mauzo na De Beers unaoipa nchi yake sehemu kubwa zaidi ya utajiri wa almasi, ingawa wapinzani wanasema hajafanya vya kutosha kubadilisha uchumi na kuunda ajira.

Ameingia kwenye mgogoro na Khama, anayemtuhumu kwa kuendesha utawala wa mabavu na kusaidia chama cha upinzani.


Duma Boko

Mgombea mwingine wa kiti cha urais, Duma Boko, mwenye umri wa miaka 54, ni mwanasheria anayegombea kwa mara ya tatu kama kiongozi wa chama cha Umbrella for Democratic Change (UDC), muungano wa upinzani ambao ulishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2019 na umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa BDP.

Katika ilani ya chama chake, Boko anapendekeza kuongeza nafasi ya Serikali katika uchumi ili kufikia maendeleo ya kijamii na ukuaji endelevu.

Chama cha Boko kilipinga matokeo ya uchaguzi uliopita katika Mahakama Kuu ya nchi hiyo kikidai kuwa ulikuwa ulaghai. Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo.


Dumelang Saleshando

Dumelang Saleshando, mwenye umri wa miaka 53, ni kiongozi wa chama cha Botswana Congress Party (BCP). Chama hicho kilianzishwa mwaka 1998 na kimekuwa kikipata kati ya asilimia 10 na 20 ya kura katika chaguzi zilizopita.

Saleshando alichukua uongozi kutoka kwa baba yake mwaka 2010. Chama hicho kinajitambulisha kama chenye misingi ya demokrasia ya kijamii na kinafanya kampeni kwa kauli mbiu ya “Okoa Botswana”.


Mephato Reatile

Mgombea mwingine ni Mephato Reatile ambaye ni kiongozi wa chama cha Botswana Patriotic Front (BPF), chama kilichoanzishwa mwaka 2019 na wanachama wa chama tawala waliojiondoa kumfuata Khama baada ya kuondoka kutokana na mgogoro wake na Masisi.

Khama, ambaye baba yake, Seretse Khama alikuwa Rais wa kwanza wa Botswana, amerudi kutoka uhamishoni alikokuwa kwa miaka mitatu ili kukisaidia BPF katika uchaguzi huu. Chama hicho kilipata takribani asilimia nne ya kura mwaka 2019.

Uchaguzi uliofanyika Oktoba 23, 2019 ulikiwezesha chama cha BDP kuendelea kuwa na wingi wa viti bungeni kwa mara ya 12 mfululizo, kikijipatia asilimia 53 ya kura na viti 38 kati ya 57, kikiwa na kiti kimoja zaidi ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2014.

UDC kilipata asilimia 36 ya kura na viti 15, viti viwili pungufu ikilinganishwa na matokeo yake ya mwaka 2014.

Uchaguzi huo ulileta mabadiliko makubwa ya kisiasa katika taswira ya siasa za Botswana. Hii ni kutokana na mabadiliko makubwa ya wapinzani kuungwa mkono katika Wilaya ya Kati (Central District) ambayo ilikuwa ikikiunga mkono BDP kwa wastani wa asilimia 75 ya kura tangu chaguzi za kwanza wa mwaka 1965.

Hali hiyo ilitokana na Rais wa zamani, Ian Khama, kukiunga mkono chama kipya cha BPF na wagombea wa UDC, pale ambapo BPF haikuwa na wagombea wake.

UDC na BPF walishinda viti 11 kati ya 17 vya wilaya hiyo, na hiyo ilikuwa mara ya kwanza katika historia kwa chama tofauti na BDP kushinda kiti katika wilaya hiyo.


Historia ya chaguzi Botswana

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2019, kulikuwa na vyama vitatu vya upinzani katika Bunge la Taifa—UDC, BPF na Alliance for Progressives (AP). Agosti 2022, BPF ilijiunga na muungano wa UDC, ikiunganisha vyama vyote vya upinzani vilivyopo bungeni isipokuwa AP.

Chama cha BCP, ambacho ni mshirika mkubwa wa UDC tangu mwaka 2017, kilionyesha nia ya kujiondoa katika muungano wa UDC kutokana na migogoro kati ya kiongozi wa BCP, Dumelang Saleshando na kiongozi wa UDC, Duma Boko.

Saleshando aliacha kuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni baada ya kundi la wabunge wa UDC, likiwa na wabunge watano waliotoka BCP, kupiga kura ya kumwondoa kwenye nafasi hiyo Julai 2022.

BCP ilipendekeza kuunda muungano wa uchaguzi na AP pamoja na Chama cha Wafanyakazi cha Botswana (Botswana Labour Party), chama kidogo kilichojitenga kutoka Botswana National Front.

Hata hivyo, AP ilijiondoa kwenye mazungumzo ya muungano kutokana na kutokubaliana na BCP, hasa kuhusu mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi, na badala yake iliamua kujiunga na UDC.

Mei 2023, kamati kuu ya BCP iliamua kwa kauli moja kushiriki uchaguzi wa mwaka huu bila kushirikiana na muungano wa UDC. Chama kilitaja sababu za kujiondoa kuwa ni kutokuwapo kwa demokrasia ya ndani ndani ya UDC na hatari kwa kiongozi wao wa chama kuwa chini ya ushawishi wa “maslahi binafsi.”

Baada ya kikao cha viongozi wa BPF, Aprili huu, chama hicho kiliamua kujiondoa kwenye muungano wa UDC, kikichagua kutumia “mfumo wa makubaliano” ambao ungehusisha BPF kutosimamisha wagombea katika majimbo yasiyoweza kushinda na UDC kutofanya hivyo pia katika majimbo ambayo BPF inaweza kushinda. Hata hivyo, pendekezo hili lilikataliwa na uongozi wa UDC.


Mustakabali wa taifa

Tangu Botswana ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1966, imekuwa chini ya utawala wa chama kimoja, BDP, ambacho kimeiongoza nchi kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi na kisiasa.

Botswana imefanikiwa kutumia vizuri rasilimali zake, hususan almasi na kuendeleza uchumi unaofikia viwango vya juu zaidi barani Afrika.

Hata hivyo, changamoto zimeibuka katika miongo ya karibuni ikiwemo ukosefu wa ajira, utegemezi mkubwa wa uchumi wa almasi na tofauti za kisiasa ndani ya chama cha BDP ambazo zimechochea migogoro na kuibuka kwa vyama vya upinzani.

Kwa muda mrefu, Botswana imekabiliwa na changamoto za kiuchumi, hususan kutokana na utegemezi mkubwa wa mapato ya serikali kwenye almasi. Ingawa nchi hiyo imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi kupitia sekta ya madini, kupungua kwa mahitaji ya almasi duniani na mabadiliko ya bei katika soko la kimataifa kumewapa viongozi wa Botswana changamoto za kutafuta njia mpya za kuinua uchumi.

Masuala mengine muhimu katika ajenda za uchaguzi huo ni pamoja na ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana, pamoja na upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu na miundombinu. UDC inakusudia kuongeza nafasi ya serikali katika kuimarisha uchumi na kutoa huduma za kijamii kwa lengo la maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, BDP imejielekeza katika kuboresha mazingira ya uwekezaji wa sekta binafsi ili kuchochea ukuaji wa ajira na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi.


Mustakabali wa kisiasa na kiuchumi

Uchaguzi wa mwaka 2024 unachukuliwa kuwa ni kipimo cha uimara wa demokrasia ya Botswana na mwelekeo wa nchi hii katika miaka ijayo.

Ikiwa BDP itaendelea kushikilia madaraka, Rais Masisi anakabiliwa na changamoto ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi ambayo yataondoa utegemezi wa almasi na kuwapa vijana nafasi zaidi za ajira.

Masisi na chama chake wanatarajiwa kuendeleza juhudi za kuvutia uwekezaji wa ndani na nje pamoja na kufikia mipango mipya ya kiuchumi ambayo itajikita zaidi katika sekta za viwanda, kilimo na utalii.

Kwa upande mwingine, iwapo UDC itafanikiwa kushinda, Botswana inaweza kuona mabadiliko makubwa katika sera za kiuchumi na kijamii. Duma Boko na muungano wa UDC wanapendekeza kuongeza nafasi ya serikali katika uchumi ili kukuza maendeleo ya kijamii na kuleta usawa wa kiuchumi katika jamii.

Mpango huu unaungwa mkono na baadhi ya wananchi wanaohisi kuwa BDP imekosa kuwajumuisha vya kutosha katika uchumi na kwamba raslimali za nchi hazijanufaisha kila Mtswana.

Leo itakuwa siku muhimu kwa Botswana, ambapo wapiga kura watakuwa na nafasi ya kuamua juu ya mustakabali wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yao.

Chaguzi za awali nchini humo zimekuwa za amani na zilizojaa matumaini ya demokrasia, na kuna matumaini kuwa uchaguzi huu pia utaendeshwa kwa uwazi na usalama. Iwe BDP au UDC itashinda, Botswana inakabiliwa na jukumu kubwa la kukabiliana na changamoto za kiuchumi, kuboresha maisha ya wananchi, na kudumisha sifa yake kama kielelezo cha utawala wa kidemokrasia na utulivu barani Afrika.

Kwa hivyo, uchaguzi wa mwaka 2024 si tu ni mpambano wa kisiasa baina ya vyama vya siasa bali pia ni jaribio la taifa hili kutathmini na kutafuta njia bora zaidi za kujiendesha kisiasa na kiuchumi kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.