Mbaroni kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, anaswa akitaka kunywa sumu

Kibaha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Isaya Kastam mkazi wa Kwa Mfipa Kibaha kwa tuhuma za mauaji ya mpenzi wake, Faraja Chafu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 8, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema kuwa tukio hilo limetokea Julai 7 saa tatu usiku Kibaha.
Polisi imedai kwamba mtuhumiwa alimshambulia mpenzi wake anayefahamika kwa jina Faraja Chafu Mkazi wa Kwa Mfipa kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za wake na kumsababishia majeraha.
Amesema kuwa chanzo cha kumshambulia mpenzi wake huyo ambaye ni marehemu kwa sasa, ni wivu wa mapenzi baada ya kutoelewana na kwamba alifariki wakati akiwahishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwa ajili ya matibabu.

"Baada ya kumshambulia kwa kisu mtuhumiwa alitoroka lakini baadaye alipatikana maeneo ya Kigamboni jijini Dar Salaam baada ya kujaribu kunywa kitu kinachodhaniwa kuwa ni sumu ili ajiue," amesema.
Amesema kuwa mtuhumiwa huyo anaendelea kupatiwa matibabu na atakapopata nafuu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi kwa ajili ya uchunguzi.
Mjumbe wa Mtaa huo, Yusufu Kalala amesema kuwa marehemu emzi za uhai wake ameishi kwa miaka mingi katika eneo hilo na kwamba maisha yao wamekuwa wakitengana na kurudiana.
"Wamekuwa wakitengana na kurudiana lakini tukio hili ni kubwa na limetushangaza wote," amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Nasra Madenge amesema kuwa taarifa hiyo imewashangaza na kuwahuzunisha kwa kuwa ni tukio la kikatili.
"Tunaendelea na mipango mbalimbali tukishirikiana na wanandugu ili kuhakikisha marehemu anazikwa au anasafirishwa," amesema.
Wakati huohuo Kamanda huyo wa Polisi ameaema watu 11 wamejeruhiwa baada ya basi la abiria kupinduka maeneo ya Mdaula Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni baada ya dereva wa basi la abiria kutaka kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari.
"Ajali imetokea leo Jumanne saa tano asubuhi ikihusisha basi kampuni ya Kidinilo lililokuwa likitokea Kilosa kuelekea jijini Dar es Salaam lilipinduka na kuingia kwenye mfereji," amesema.

Amesema kuwa kati ya majeruhi hao saba wamelazwa Kituo cha Afya Chalinze na watatu wamelazwa Hospitali ya Msoga wakiendelea na matibabu.
Amesema kuwa wanaendelea kumtafuta dereva wa basi hilo ambaye alitoroka baada ya ajali hiyo.