Prime
KESI YA MAUAJI YA MUUZA MADINI MTWARA: Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa- 8

Muktasari:
- Hii ni simulizi ya hukumu ya kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili askari saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, katika hukumu yake aliyoitoa Juni 23,2025, Jaji Hamidu Mwanga, aliwahukumu polisi wawili adhabu ya kifo
Dar es Salaam. Katika mfululizo wa mapitio ya hukumu ya kesi hii ya mauaji ya kukusudia iliyokuwa ikiwakabili maofisa wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, leo tunaangazia Mahakama ilivyochambua ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wa washtakiwa.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara) na Nicholous Kisinza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Marco Chigingozi, Mkaguzi Msaidizi, John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi ) na Salim Mbalu alikuwa Koplo.
Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara.
Katika sehemu iliyopita tulifikia hitimisho la hoja za Jamhuri iliyofunga pazia la hoja za mwisho za mawakili wa pande zote za namna ushahidi wao ulivyojibu viini vya hatia kwa washtakiwa na kubainisha udhaifu wa utetezi wao.
Hitimisho hilo la hoja za mwisho za Jamhuri, sasa linatoa fursa kwa Mahakama kuamua hatima ya washtakiwa hao.
Kabla ya kuanza uchambuzi wa ushahidi wa pande zote na hoja za mwisho za mawakili wa pande zote kuona kama washtakiwa wote au baadhi yao wana hatia au la, Jaji Hamidu Mwanga alianza kwa kujenga msingi wa kufikisha suala hilo katika hitimisho.
Jaji Mwanga alibainisha misingi ya kisheria na kikanuni ya kumuongoza kufikia hitimisho hilo, huku akibainisha vifungu mbalimbali hasa vya Sheria ya Ushahidi na kurejea kesi zilizowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufani.
Utangulizi hukumu ya Jaji
Jaji Mwanga akaanza kwa kusema kanuni ya kimatendo ni kwamba, mlezi anapogeuka kuwa mkaidi au mtesaji, mshikamano wa jamii huanza kuvunjika.
“Kauli hii inaelezea kwa usahihi msingi wa kihistoria wa hukumu ambayo ninakwenda kuitoa muda mfupi ujao,”alieleza Jaji Mwanga.
“Kesi hii inaonesha hali ya kusikitisha na ya kustaajabisha, kwamba askari polisi walioapa kulinda sheria na usalama wa maisha ya raia, sasa wameshtakiwa kwa kosa moja la kutisha sana la jinai, nalo ni mauaji ambalo linaweza kuvunja kabisa uaminifu mtakatifu uliowekwa kwao.”
“Badala ya kuwa ngome dhidi ya hofu, uwepo wao sasa unazua hofu. Mahakama hii inatambua kwa undani athari kubwa ambazo tuhuma hizi zinaweza kuwa nazo kwa hisia za usalama wa jamii”.
“Leo, Mahakama hii ina jukumu la dhati la kuchambua tuhuma hizi nzito na kutoa haki pale ambapo haki imevunjwa kwa kiwango kikubwa.”
Je, Jamhuri wamethibitisha shtaka?
“Nimepitia kwa umakini ushahidi uliowasilishwa na pande zote pamoja na hoja za mwisho zilizotolewa kwa ajili ya kuunga mkono ushahidi huo,” alisema Jaji.
“Swali la msingi linalopaswa kujibiwa ni iwapo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa kwa kiwango kinachohitajika kisheria, yaani, bila kuacha shaka yoyote.
“Katika mashtaka ya jinai, tuhuma peke yake, hata kama ni nzito kiasi gani, haitoshi kumtia mtu hatiani hasa katika shtaka zito kama la mauaji,”alisema Jaji Mwanga.
Jaji Mwanga alisema ni kanuni ya sheria, kama ilivyoainishwa chini ya vifungu vya 110(1), (2) na 112 vya Sheria ya Ushahidi, Toleo la 2022, kwamba mtu anayeshtaki ni lazima athibitishe madai yake na mzigo wa kuthibitisha uko juu ya yule anayeshtaki na haupaswi kamwe kuhamia kwa mshtakiwa.
“Kiwango kinachotakiwa cha uthibitisho kimeelezwa chini ya kifungu cha 3(2)(a) cha Sheria hiyo ya Ushahidi kwamba ni bila kuacha mashaka yoyote (beyond reasonable doubt),”alieleza Jaji.
“Neno ‘beyond reasonable doubt’ halijafafanuliwa kisheria moja kwa moja, lakini limeelezwa katika uamuzi wa kesi mbalimbali. Kwa mfano kesi ya Magendo Paul & Mwingine dhidi ya Jamhuri [1993] T.L.R. 219, Mahakama ilishikilia kuwa:
“Ili kesi ichukuliwe kuwa imethibitishwa bila shaka yoyote ya msingi, ushahidi wake ni lazima uwe imara dhidi ya mshtakiwa kiasi cha kuacha uwezekano wa mbali tu kwa manufaa yake, uwezekano unaoweza kuondolewa kirahisi.
“Ni jambo muhimu pia kuelewa kuwa, wajibu huu unaweza tu kutekelezwa iwapo upande wa mashtaka utathibitisha kwa mafanikio kila kipengele cha kosa linalodaiwa kutendwa na mshitakiwa au washitakiwa,”alisema Jaji Mwanga.
“Uthibitisho wa kipengele kama hicho haupaswi kuchukuliwa kimzaha, bali ni lazima uwe imara vya kutosha kuelekeza upande mmoja tu, kwamba mshitakiwa ndiye aliyefanya kosa, na si mtu mwingine yeyote.”
Haipaswi kubaki shaka
“Hii ina maana kwamba, ushahidi wa upande wa mashtaka ni lazima uwe na nguvu kiasi cha kuondoa shaka yoyote kuhusu hatia ya mshitakiwa,”alisema Jaji.
Jaji Mwanga akaongeza kusema: “Ushahidi huo ni lazima uelekeze moja kwa moja kwa mshtakiwa, na si mtu mwingine, kuwa ndiye aliyefanya kosa hilo.”
“Kwa kuzingatia yaliyotajwa hapo juu, kiwango cha uthibitisho ‘beyond reasonable doubt’ hakimaanishi kutokuwa na shaka hata kidogo au ‘beyond the shadow of doubt’ bali kinamaanisha uwezekano wa hali ya juu.
“Uthibitisho ‘beyond reasonable doubt’ haumaanishi ‘ hakuna kivuli kabisa cha shaka,”alisisitiza Jaji Mwanga.
Lazima kuwepo nia ya pamoja
“Kufuatia hayo yote, ni muhimu pia kutambua kuwa, ili upande wa mashtaka upate hukumu ya hatia katika kesi hii ambayo ina washitakiwa zaidi ya mmoja, ni lazima uthibitishe nia ya pamoja kulingana na kifungu cha 23 cha Kanuni ya Adhabu,”alisema Jaji.
“Kwa uelewa zaidi, kifungu hicho kinanukuliwa kama ifuatavyo:
“Wakati watu wawili au zaidi wanapokuwa na nia ya pamoja ya kutekeleza lengo lisilo halali kwa kushirikiana na katika kutekeleza lengo hilo, kosa linatendwa ambalo kwa asili yake lilitarajiwa kuwa matokeo ya utekelezaji wa lengo hilo, basi kila mmoja wao atachukuliwa kuwa ametenda kosa hilo.”
“Kwa kufafanua dhana ya nia ya pamoja, Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Issa Mustapha Gora & Mwingine dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 330 ya 2019 iliyotolewa Oktoba 19, 2022, ilisema na hapa nanukuu:
"Katika kuthibitisha nia ya pamoja, ni muhimu ushahidi madhubuti utolewe kuonesha kulikuwepo na makubaliano ya pamoja ya watu wawili au zaidi katika kutekeleza mpango wa pamoja wa kutenda kosa.
“Kwa hiyo, kuthibitisha nia ya pamoja hakuhitaji kuwa na makubaliano ya moja kwa moja kabla ya kutenda kosa. Nia hiyo ya pamoja inaweza kuhitimishwa kutokana na uwepo wao, matendo yao, na kushindwa kwao kujitenga na tukio hilo.
“Kwa kuzingatia kesi rejea mbalimbali zilizotajwa hapo juu, ni jukumu la Mahakama hii kuchambua ushahidi uliotolewa ili kubaini iwapo washitakiwa walitenda kosa linalowakabili ama la.”
Jaji Mwanga alijibu kwanza hoja za kisheria zilizoibuliwa na washtakiwa wakati wakijitetea.
Ni hoja gani waliziibua washtakiwa hao na Jaji Mwanga alizijibuje? Usikose sehemu inayofuata.