Sugu ambwaga Msigwa uenyekiti Chadema Kanda ya Nyasa

Muktasari:

  • Sugu ataiongoza Kanda ya Nyasa kwa miaka mitano hadi 2029 baada ya kumbwaga aliyekuwa mpinzani wake na mtetezi wa nafasi hiyo, Mchungaji Peter Msigwa.

Njombe. Aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini,  Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu ameibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Nyasa akimbwaga mpinzani wake Mchungaji Peter Msigwa.

Sugu amemshinda Msigwa ambaye alikuwa anatetea nafasi yake kwa kura 54 kwa 52 na sasa kada huyo ataiongoza kanda hiyo kwa miaka mitano hadi 2029.

Akitangaza matokeo hayo leo Mei 29, 2024 msimamizi wa uchaguzi huo,  Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Benson Kigaila amesema jumla ya wapiga kura walikuwa 106 na hakuna kura zilizoharibika.

Akizungumza baada ya matokeo hayo, Msigwa amewashukuru wapiga kura kwa maamuzi yao akieleza kuwa thamani yake itabaki vilevile bila kuwa kiongozi.

Amesema ataendelea kukitumikia chama kwani hakuingia Chadema kwa ajili ya uongozi na kumpongeza Sugu kwa kushinda na kumuahidi ushirikiano pale atakapohitaji msaada wake.

"Niwashukuru sana wajumbe kwa uamuzi wenu mmetaka mabadiliko na ninapokea vyema matokeo, naamini thamani yangu kichama itabaki hivyo nimpongeze Sugu na niko tayari kwa ushirikiano popote nitakapohitajika" amesema Msigwa.

Naye Sugu mbali na kutanguliza shukurani amesema wapiga kura kuridhia na kumpa  kura za kutosha inaakisi wajumbe kukubaliana na ajenda zake 10, hivyo kwa peke yake hatoweza akiomba ushirikiano.

Amesema kwa sasa suala ni moja kuwaunganisha wanachama haswa kwa kipindi hiki wakielekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu na kwamba ili awe bora anahitaji viongozi bora kuanzia mkoa,  wilaya na majimbo.

"Yale mazuri uliyofanya  Msigwa nitayachukua, lengo letu ni kukipa thamani chama na kuwaunganisha wote, kuanzia kesho Mei 30,2024  tunaanza upya kwani sijashinda mimi bali chama ndicho kimeshinda" amesema Sugu.

Katika nafasi ya  Makamu Mwenyekiti   Kanda ya Nyasa, amepita Frank Mwakajoka, huku nafasi ya Mweka Hazina akishinda Grace Shio.