Sura mpya zachomoza UWT, UVCCM

Muktasari:
Uchaguzi wa Jumuiya za Umoja wa Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake (UWT) wa Chama cha Mapinduzi jana umetimua vumbi, ukishuhudia vigogo katika jumuiya hizo wakibwagwa na kuibuka kwa sura mpya.
Dar/Mikoani. Uchaguzi wa Jumuiya za Umoja wa Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake (UWT) wa Chama cha Mapinduzi jana umetimua vumbi, ukishuhudia vigogo katika jumuiya hizo wakibwagwa na kuibuka kwa sura mpya.
Uchaguzi huo ni mwendelezo wa chaguzi za ndani za chama hicho zitakazokamilika mwezi ujao.
Juzi mkoani Mara uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti wa UVCCM uliingia dosari baada ya aliyekuwa mgombea, Baraka Magira kugoma kutia saini matokeo akidai kushindwa kwake kumechangiwa na uwepo wa vitendo vya rushwa.
Hatua hiyo ilikuja baada ya msimamizi wa uchaguzi huo, Novatus Kibaji kumtangaza Mary Joseph, kuwa mshindi katika nafasi ya uenyekiti kwa kupata kura 369 dhidi ya kura 207 alizopata mshindani wake wa karibu, Magira baada ya wagombea hao kupigiwa kura kwa awamu ya pili.
Uamuzi wa wawili hao kupigiwa kura mara ya pili ulitokana na wagombea watatu waliochuana kutofikia nusu ya kura kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa chama hicho.
“Rushwa ilianza kutembea wakati wa kura za awamu ya pili ambapo baadhi ya watu wasiokuwa wajumbe walionekana wakishawishi wajumbe kwa kuwapa fedha ili kumpigia kura mshindani wangu. Hii ni kinyume cha kanuni, miiko, utamaduni na taratibu, naomba hatua stahiki zichukuliwe,” alidai Baraka
Hata hivyo, Kibaji aliyesimamia uchaguzi huo, alisema hakushuhudia tukio lolote la vitendo vya rushwa ndani ya ukumbi, hivyo anaamini uchaguzi huo ulikuwa huru na haki kwa kufuata kanuni na taratibu zote.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Lengael Akyoo alisema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki na chama hakina mashaka na washindi waliotangazwa.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara, Hassan Mossi alisema ofisi yake inafuatilia madai hayo.
Mkoani Mbeya, UVCCM imepata viongozi wapya katika uchaguzi uliofanyika juzi, huku Yassin Ngonyani akichaguliwa kuwa Mwenyekiti.
Ngonyani alipata kura 266, akimshinda Agrey Mwaijange aliyepata kura 247 na Baraka Chalamila aliyepata kura 51.
Ngonyani alisema haikuwa kazi nyepesi kuaminiwa na kupewa nafasi katika Mkoa wa Mbeya, lakini ameipata sababu aliomba kwa ajili ya vijana wote wa Mbeya sio masilahi binafsi.
“Nimetumwa na vijana na ninakwenda kuwatumikia nikiishi katika ajenda ili nifanye kazi kwa kushughulikia changamoto za vijana, sababu mimi ndio mwakilishi wao ngazi ya mkoa nikiwa nimepewa jukumu la kuwasimamia,” alisema.
Sura mpya pia zimejitokeza mkoani Arusha, ambapo Saimon Maximilian Iranghe ambaye ni mtoto wa Meya jiji la Arusha, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti UVCCM mkoa huo.
Saimon alipata kura 345 akifatiwa na Ikoyo Kilaye Laizer aliyepata kura 155, Mwinyi Said Njuhe kura nane, Nicomed Axweso Josephat kura nne.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo katika ukumbi wa AICC Arusha, msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Thomas Apson ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, alisema katika uchaguzi huo kura zilizopigwa zilikuwa 555.
Akizungumza baada ya kutangazwa kushinda, Iranghe aliwataka vijana wote kufanya kazi kwa ushirikiano na kwamba uchaguzi umeisha na wote sasa ni kitu kimoja.
Mkoani Ruvuma, Kelvin Challe alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM kwa kura 266 kati ya 490 zilizopigwa na wajumbe.
Mchuano UWT
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwajabu Rajabu Mbwambo ameshinda nafasi ya Mwenyekiti Umoja wa Wanawake (UWT) kwa kupata kura 164 na kuwashinda wapinzani wake wanne.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija alisema kura zilizopigwa ni 271 na hakuna iliyoharibika.
Mkoani Njombe aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT mkoa huo, Scolastica Kevela, amefanikiwa kutetea nafasi hiyo baada ya kupata kura 242 kati ya kura 266 zilizopigwa na wajumbe wa jumuiya hiyo.
Mkoani Songwe UWT imepata viongozi wapya baada ya Anna Gidarya kushinda kwa kupata kura (155) na kumshinda mpinzani wake, Justina Kasunga aliyepata kura 82 na Betha Chifupa aliyepata kura tano.
Taarifa hii imeandaliwa na Beldina Nyakeke (Mara), Tuzo Mapunda (Dar), Seif Jumanne (Njombe), Stephano Simbeye (Songwe), Yohana Challe (Mbeya), Mussa Juma (Arusha) na Joyce Joliga (Ruvuma).