Tatizo linalokwamisha maendeleo ya Tanzania

Muktasari:

Upo gonjwa unaoisumbua nchi tangu uhuru. Wanazuoni wa siasa wanauita “Political Continuity “Mwendelezo wa Kisiasa” ndani ya Serikali.

Upo gonjwa unaoisumbua nchi tangu uhuru. Wanazuoni wa siasa wanauita “Political Continuity “Mwendelezo wa Kisiasa” ndani ya Serikali.

Historia itamweka huru Rais Samia Suluhu Hassan endapo atahakikisha anaunda mifumo thabiti, itakayoweka ugumu kwa kiongozi mpya kuacha miradi, maono, dira au sera za mtangulizi wake. Nitafafanua.

Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa wa maji. Hata hivyo, ajabu ni kuwa wananchi wake bado wanateseka kupata huduma hiyo muhimu. Yapo maeneo Tanzania watu wanakunywa maji machafu.

Miaka 61 baada ya Uhuru, kukosekana mvua kidogo tu, maji yalikata, nchi ikatikisika. Tena kuna viongozi walitokeza na kutoa utetezi mwepesi kuwa uhaba wa maji ulisababishwa na ukame, hivyo ni changamoto iliyokuwa juu ya uwezo.

Zimebaki siku chache nchi iadhimishe miaka 61 tangu ilipopata uhuru. Umeme bado ni msamiati mgumu. Mgawo na kukatika mara kwa mara. Yapo maeneo nchini watu wanakosa umeme hadi saa 24 na kuendelea.

Wapo watu wanahoji, mbona wakati wa Rais John Magufuli umeme na maji havikuwa shida? Ni swali lisilo na tija. Aghalabu, huulizwa na wale ambao hupenda kushughulika na mahali wanapoangukia badala ya pale wanapojikwaa.

Watu makini kabla ya kuuliza watatafakari muda ambao Rais Samia ameingia madarakani. Ni takriban miezi 20 (mwaka mmoja na miezi nane au wiki 85). Je, matatizo yote ya umeme na maji yangemalizwa ndani ya wiki 85?

Yule ambaye si tabia yake kulaumu bali kuusaka ukweli, atawauliza wanaosema wakati wa Magufuli umeme na maji havikuwa shida, je, alitatua tatizo kwa njia ya kudumu au alifanya utatuzi wa kisiasa?

Magufuli alijenga miundombinu ipi ambayo ilifanya umeme na maji visikatike? Je, wakati wa Samia, wamebomoa miundombinu hiyo hivyo kusababisha umeme na maji virudi kuwa shida?

Maswali hayo yatakuleta kwenye majibu kuwa Samia alikuta viraka. Kazi kwake, kuendeleza viraka au kujenga msingi wa ufumbuzi wa kudumu.


Tuweke muktadha sawa

Si kweli kuwa wakati wa Magufuli umeme haukuwa ukikatika. Na kwamba maji yalikuwa ya uhakika kipindi chote. Matatizo ya umeme na maji yalikuwepo. Tofauti ni kiwango.

Aprili 2019, aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, alieleza kuwa tatizo la kukatika umeme mara kwa mara lilisababishwa na ubovu wa mitambo iliyokosa matengenezo ya uhakika.

Angalau hapa tunakumbushana, kwamba tatizo la umeme lipo na lilikuwepo. Mwaka 2019, umeme kukatika mara kwa mara ilikuwa hoja ya CAG. Wakati huo, Rais alikuwa Dk Magufuli na Waziri wa Nishati aliyekuwepo ofisini ni Medard Kalemani.

Dhambi ni kusema tatizo la umeme limeanza wakati wa Rais Samia au kipindi cha uwaziri wa January Makamba. Na haya ni matokeo ya kitu kinachoitwa “post-truth”, yaani ukweli na usahihi unazidiwa nguvu na hisia pamoja na mitazamo binafsi.

Hatupaswi kuishi kwenye zama ambazo ukweli unafunikwa na uongo pamoja na mitazamo binafsi. Haitasaidia nchi. Vema kuujadili ukweli katika vipimo sahihi ili kupata majibu ya kudumu.

Tanzania imekuwa ikihudumiwa kwa mtindo wa kushona viraka. Kwamba tatizo likiwepo, linashughulikiwa kwa muda mfupi, mambo yatulie, maisha yaendelee. Hakuna tiba mahsusi.

Huoni kama nchi, ukiletwa mpango maalumu wa kumaliza tatizo la maji nchi nzima ndani ya kipindi tengwa. Kwamba asimilia 10 ya makusanyo ya mapato ya nchi, kwa miaka mitatu, yapelekwe kwenye kutatua changamoto ya maji. Iwe suluhu ya kudumu.

Kwamba asilimia 10 ya mapato ya nchi, ndani ya miaka mitano, yaelekezwe kwenye kumaliza shida ya umeme na ibaki historia. Hivyo ndivyo kumaliza matatizo. Sio huu mwendo wa kushona viraka. Kutuliza hali, usifiwe kisiasa, wakati gonjwa bado lipo.

Kumbe sasa, tatizo la umeme na maji ni matokeo ya Serikali kutokuja na suluhu ya kudumu. Vilevile kukosekana mwendelezo wa kisiasa. Rais wa Nne, Jakaya Kikwete aliiacha nchi kwenye uelekeo wa umeme wa gesi. Alipokuja Magufuli aliielekeza nchi kwenye umeme wa maji.

Kikwete alijenga bomba la gesi Mtwara, Magufuli aliibuka na Bwawa la Julius Nyerere. Uwekezaji wa bomba la gesi ukaachwa, ukaja mradi wa kukata miti ili kufanikisha ujenzi wa bwawa la umeme Mto Rufiji.

Unajenga miundombinu ya umeme yenye kutegemea maji, wakati huohuo ili kufanikisha ujenzi, unaharibu vyanzo vya maji. Kisha nchi inakosa mvua. Ukame unatamalaki. Taifa linakosa umeme na maji kwa wakati mmoja.

Bomba la Mtwara lingepata mwendelezo wa kisiasa, kutoka Kikwete mpaka Magufuli, pengine leo tungekuwa tunazungumza mengine. Alipofika Magufuli alianza na lake.

Vipi Rais Samia angeamua na yeye kuanza na miradi yake na kupuuza Bwawa la Julius Nyerere? Hasara kiasi gani ambayo nchi ingeingia? Inabidi nchi iimarishe mifumo, tena suala mwendelezo wa kisiasa liwe ndani ya Katiba.

Ukifuatilia jinsi viongozi wanavyofanya kazi unabaki na maswali mengi kama nia huwa kupata ufumbuzi wa kudumu, kutafuta sifa za muda mfupi au agenda nyingine. Unajenga Bwawa la Julius Nyerere, wakati CAG anasema tatizo ni miundombinu chakavu na mibovu.

Waziri January alisema bungeni kuwa Tanesco wanatumia nyaya zenye msongo mdogo, maalumu kwa ajili ya kugawa umeme kwenye nyumba, kusafirishia umeme.

Kwa kawaida umeme husafirishwa kwa nyaya zenye uwezo wa kubeba umeme wa msongo mkubwa, kuanzia kilovolt 400, 220, 132 na za chini kabisa ni kilovolt 66. Zinazosambaza umeme ni za msongo mdogo, kilovolt 33 na kilovolt 11. Kwa sasa, Tanesco wanasafirisha umeme kwa nyaya zenye uwezo wa kusambaza tu.

Yaani waya ambao unatosha kusambaza umeme ili ukufikie nyumbani kwako, ndio unaotumika kusafirisha kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Unajiuliza, umeme zaidi ya megawati 2,000 utakaozalishwa Julius Nyerere, utasambazwa kwa miundombinu ipi kama hali ndivyo inaelezwa?

Wanasiasa wanapaswa kutambua kuwa Serikali hubaki moja. Mabadiliko hufanywa kwa viongozi lakini Serikali huwa inabaki ileile. Hili ni eneo ambalo wanasiasa hawana budi kuheshimu.

Uwepo wa Serikali hujengwa na misingi yake, vilevile huwa na nguzo zake zinazoishikilia. Mabadiliko ya kiutawala hayapaswi kusababisha nguzo zote zinazoishikilia Serikali zibomolewe au hata msingi wenyewe.

Serikali ambayo inabadilika kila baada ya uchaguzi na kila baada ya utawala mmoja kwenda mwingine mpya hapo ni kama hakuna Serikali, bali nchi inaenda kulingana na matakwa ya mtawala aliyepo.

Serikali huonekana pale ambapo mtawala anaikuta Serikali, anaisoma mahali ilipofikia, anaendeleza yale mazuri, anaimarisha yenye udhaifu kisha maeneo anayoona yanahitaji marekebisho, anafuata mchakato wa kikatiba na kisheria kuyabadilisha.

Ni maelekezo ya kikatiba kwa Serikali kupitia Bunge kutungia sheria mabadiliko inayofanya, hii msingi wake ni kuwa asije kutokea mtawala mpya akafanya vinginevyo au mtendaji kwa kiburi tu akaacha kutekeleza. Sheria zinatungwa ili kuyapa nguvu na uhalali mabadiliko yanayofanywa.

Haina maana kuwa mtawala mpya hapaswi kufanya mabadiliko yoyote. Mtawala mpya anaruhusiwa kufanya mabadiliko ambayo anakuwa ameyapa uhalali wa kisheria. Haamki asubuhi tu na kuagiza mambo fulani yaanze na mengine yakome.

Utawala mpya hukaribisha mawazo mapya ya kiuongozi, lakini mawazo hayo hayawezi kuwa sera ya Serikali mpaka kwanza yachakatwe ndani ya Baraza la Mawaziri. Mawazo ya mtawala mpya hayawezi kutungiwa sheria pasipo kupitishwa bungeni.

Kurasimisha biashara

Oktoba 2004, Serikali ya Tanzania iliingia makubaliano na Serikali ya Norway, kuhusu kufanya mapitio ya biashara na rasilimali za wanyonge ili kuzifanya ziwe rasmi. Mapitio hayo ndiyo yaliyozaa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita).

Kuhusu Mkumkuta, Rais Mkapa alikaa na baraza lake Hoteli ya Ngurdoto, mtaalamu kutoka Peru, Jens Clausen, akawapiga msasa mawaziri kuhusu njia na mbinu sahihi za kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa mazingira ya Kitanzania.

Clausen pia ndiye alikuwa kiongozi wa timu ya wataalamu waliofanya mapitio ya rasilimali na biashara za Watanzania kisha kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuzirasimisha. Pitia miaka 10 ya Kikwete, huoni utekelezaji wa Mkukuta wala Mkurabita.

Dola za Kimarekani milioni 7 ambazo kwa sarafu ya wakati huo zilikuwa takriban Sh9.1 bilioni, zilitumika kwa ajili ya Mkurabita peke yake. Kutotekelezwa kwa mapendekezo ya wataalamu kuhusu Mkurabita, maana yake fedha hizo zilitumika bila faida yoyote.

Matokeo Makubwa Sasa

Kuhakikisha kuwa Tanzania inaongeza mwendo kuelekea Malengo ya Milenia 2025, mwaka 2012 iliweka vipaumbele nane na kuviweka kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Vipaumbele hivyo vya BRN ni Maji, Elimu, Nishati, Afya, Kilimo, Uchukuzi, Mazingira ya Biashara na Uhamasishaji wa Rasilimali. Ifahamike kuwa BRN ilipatikana baada ya Serikali ya Kikwete kuwapa kazi watunga sera wataalamu kutoka Malaysia.

Baada ya Kikwete kuondoka madarakani, mapambio ya BRN yamekoma. Hivyo, uwekezaji wote wa Serikali kwenye BRN ulipotea bure. Maana ilipuuzwa. Yupo mtu anaweza kusema, Magufuli aliamua kuachana na BRN kwa sababu ingekuwa kumpa sifa nyingi Kikwete aliyeasisi.

Hivyo ndivyo nchi inapaswa kuendeshwa? Kutelekeza mambo ya msingi kwa hoja kuwa kuyaendeleza ni kumpa sifa mtangulizi wako. Huu ni ugonjwa mkubwa nchini. Ndio maana maji, umeme na huduma nyingine za kijamii bado ni changamoto sugu. Viongozi wanachezea mno fedha kwa kukosa mwendelezo wa kisiasa.

Jukumu kubwa la Bunge ni kuisimamia Serikali ibaki ileile bila kuyumbayumba. Kwa bahati mbaya, Bunge huwa halifanyi kazi yake ipasavyo. Ndio maana mipango, miradi na hata sera, huishia njiani, huku fedha za umma nyingi zikiwa zimeshatumika.

Kisha, tunalia nchi ni maskini. Wakati fedha za umma hazisimamiwi vizuri na Bunge. Halafu, tunasema nchi bado changa, wakati Falme za Kiarabu (UAE), walipata uhuru miaka 10 baada ya Tanganyika. Kupitia mafuta na mipango bora yenye mwendelezo mzuri wa kisiasa, hivi sasa wameigeuza nchi yao ya jangwa kuwa ardhi tajiri.

Tanzania ina madini, ardhi yenye rutuba kutosha kila kilimo, kuna gesi mpaka maeneo ya urithi wa dunia, lakini miaka 61 inajitetea kuwa ni nchi changa. UAE wametumia miaka 50 kuwa tishio ulimwenguni. Kibiashara, uwekezaji, utalii mpaka starehe.