TLS wawalalamikia Ma-DC

Rais wa TLS, Charles Rwechungura
Muktasari:
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari imeitaka mamlaka inayowasimamia wakuu wa wilaya kuchukua hatua stahiki dhidi ya matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu yaliyofanywa hivi karibuni na baadhi ya viongozi hao dhidi ya raia wake.
Dar es Salaam. Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimewataka wakuu wa wilaya kuacha kuingilia mamlaka na mifumo iliyowekwa katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kimaendeleo.
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari imeitaka mamlaka inayowasimamia wakuu wa wilaya kuchukua hatua stahiki dhidi ya matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu yaliyofanywa hivi karibuni na baadhi ya viongozi hao dhidi ya raia wake.
Kupitia taarifa hiyo, Rais wa TLS, Charles Rwechungura alisema amri zilizotolewa na viongozi hao dhidi ya raia zinashindwa kutofautisha makosa na matendo ya kijinai na yale ya kinidhamu ambayo yana mifumo tofauti ya uwajibishaji.
Miongoni mwa amri zinazolalamikiwa ambazo zilitolewa ni viongozi wa Wilaya ya Tarime kuamirishwa kukaa chini ya mabenchi yaliyokuwa yakikagulia kwa lengo la kushuhudia adha wanayokutananayo wanafunzi,
Amri nyingine ni ile iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, aliyeamuru kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa wanasiasa wanaodaiwa kuwakataza wananchi kuchangia ujenzi wa maabara.
Nyingine ni ya Mkuu wa Wilaya ya Musoma, kuamuru kuwekwa rumande kwa ofisa afya kwa kosa la kushindwa kusimamia usafi kama ilivyoagizwa na Rais John Magufuli, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda kuamuru kuwa kila mgonjwa wa kipindupindu aliyelazwa afikishwe mahakamani pale anapopona.
Tukio lingine ni lile ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni aliyeamuru kukamatwa kwa maofisa ardhi wa manispaa hiyo kwa kuchelewa kufika katika mkutano.