Prime
Uamuzi wa Dk Tulia kutimkia Uyole waacha mjadala Mbeya

Mbunge wa Mbeya Mjini Dk Tulia Ackson akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara katika shule ya msingi Asanga iliyopo Uyole, Jimbo ambalo ametangaza nia ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 25 mwaka huu. Picha na Saddam Sadick
Muktasari:
- Uamuzi huo umeonekana kuwafurahisha baadhi hasa sehemu aliyotangaza kuwania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2025 huku wengine wakionyesha sura za masikitiko kutokana na namna walivyoishi naye kwa kipindi cha miaka mitano.
Mbeya. Uamuzi wa Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson kutangaza nia ya kugombea jimbo jipya la Uyole, umeibua hisia tofauti kwa wananchi, baadhi wakiunga mkono na wengine wakipinga huku wadau na wachambuzi wa siasa wakitoa kauli.
Dk Tulia ambaye ameongoza Jimbo la Mbeya Mjini kwa miaka mitano, akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Joseph Mbilinyi 'Sugu' (Chadema), ametangaza nia hiyo jana Mei 23, 2025 wakati akizungumza na wafuasi wa chama hicho zilipo ofisi za CCM Mbeya Mjini.
Uamuzi huo umeonekana kuwafurahisha baadhi hasa sehemu aliyotangaza kuwania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2025 huku wengine wakionyesha sura za masikitiko kutokana na namna walivyoishi naye kwa kipindi cha miaka mitano.
Kauli za wananchi
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wananchi na makada wa CCM jijini Mbeya, wametofautiana mtazamo kuhusu uamuzi huo wa Spika wa Bunge la Tanzania kutangaza kugombea Jimbo la Uyole.

Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson akisalimiana na baadhi ya viongozi katika Kata ya Uyole hivi karibuni kabla ya kugawanywa kuwa Jimbo.
Renatha Maziku, mkazi wa Isanga na kada wa CCM, amesema Dk Tulia amekuwa karibu na wananchi akigusa maeneo yote ikiwamo familia na makundi mbalimbali ya vijana, wenye ulemavu na akina mama wenye changamoto.
Amesema wanamkumbuka kwa mengi kwani mbali na kutoa fedha zake mfukoni kusaidia wenye uhitaji, amegusa pia miradi mikubwa ambayo inawagusa wananchi wote bila kujali itikadi za vyama wala ukabila.
“Ndio maana ukiangalia wanaoshangilia kuondoka kwake ni wale wa Uyole, siyo wa hapa Mjini, sisi ni masikitiko tulikuwa na ukaribu naye akitusikiliza na kutusaidia moja kwa moja.
“Siyo kwa wanaCCM tu, hata wananchi wa Mbeya Mjini wamepata pigo kwa kuwa aliwafikia wote, amejenga nyumba za wenye uhitaji bila kujali kama ni CCM au vyama vya upinzani, kwa ujumla tumepigwa na kitu kizito,” amesema Renatha.
Dickson Hugho, mkazi wa Ruanda, amesema Dk Tulia amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jiji akiwabeba hata madiwani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali.
Amesema kilio cha kuondoka Jimbo la Mbeya Mjini, si kwa wananchi pekee, bali hata madiwani ambao walimtegemea kwa mengi kuwabeba akieleza kuwa ameacha pengo.
“Kwa Mbeya Mjini ni pengo kubwa, hata baadhi ya madiwani aliwabeba kwa kutoa fedha zake mfukoni kusaidia kutekeleza miradi, ndio maana wengi wao majukwaani walimtangaza yeye, hili ni pigo kwa wote,” amesema Hugho.
Kwa upande wake, Faisal Mwankemwa amesema yeye hakufurahishwa na uamuzi wa Dk Tulia kulihama Jimbo la Mbeya Mjini kutokana na wadhifa alionao akieleza kuwa hiyo inaweza kuwapa nafasi wapinzani kurejesha nafasi yao.
Amesema kutokana nafasi ya kuwa Spika wa Bunge, alipaswa kuendelea kuwaongoza waliompa kura badala ya kuwaachia wengine kipindi hiki kwa kuwa uamuzi huo unawapa maswali mengi.
“Wananchi hawa ndio walimpa nafasi ya kuwa mbunge kisha kuteuliwa kuwa Spika wa Bunge, akawa Rais wa Mabunge Duniani (IPU), amefanya mengi kwenye jimbo, sasa inakuwaje atangaze kuhama? Kidogo inafikirisha.
“Alipaswa kuwaheshimu waliompa nafasi hiyo, hilo jimbo la Uyole angeacha mwingine agombee ili aanze upya badala ya yeye kwenda huko, ili atimize yale aliyoahidi ambayo hajakamilisha kwa wananchi,” amesema na kuongeza:
“Tuliona kabla ya Dk Tulia kuwa mbunge hapa, jimbo lilikuwa mikononi mwa wapinzani (Chadema), sasa anapoondoka anaweza kuwapa nafasi wapinzani kutamba kwa lolote, hatujui atakayegombea wa CCM atakuwa nani, nguvu yake ikoje na ushawishi kwa wananchi.”
Beatha Mwakajoka, mkazi wa Nsalaga amesema matarajio yao kwa ujio wa Dk Tulia katika Jimbo la Uyole, ni kuona maendeleo kwa kuwa maeneo mengi wananchi wana changamoto nyingi ikiwamo miundombinu ya barabara na maji.
“Kilio chetu huenda kimepata mwafaka, tunataka vituo vya afya, barabara zetu ni mbovu na huduma ya maji hatuna, akituletea hayo tutashukuru na ndio tunachotarajia.
“Amekuwa Rais wa IPU na Spika wa Bunge kwa maana hiyo atakuwa na koneksheni kubwa na wadau ndani na nje katika kutufikishia huduma za kijamii,” amesema Beatha.
Wachambuzi wafafanua
Mchambuzi wa siasa mkoani Mbeya, Victor Yesaya amesema kitendo cha Dk Tulia kulihama Jimbo la Mbeya Mjini kinaweza kuwa mtego kwa mgombea ajaye kutokana na vita ya kisiasa kwa wapinzani.
Amesema licha ya kwamba Dk Tulia alikuwa na nguvu kutokana na nafasi yake kwenye chama, lakini ni kama ameona awahi jimbo jipya ambalo wengi wao hawakuwa na maandalizi ya kugombea.
“Kwanza jimbo hilo halitakuwa na mtifuano kwa kuwa Dk Tulia anayo nguvu kwenye chama, anawaweza wananchi wa Uyole kwa kuwa ni wachache tofauti na Mbeya Mjini, kazi amewaachia watakaochuana na upinzani.
“Chadema si kwamba hawatagombea, kimya chao ni cha kishindo, amesoma upepo kaona aanze mapema harakati ili baadaye awe ameshaweka mikakati ya ushindi,” amesema Yesaya.
Naye John Theophil amesema hatua ya Dk Tulia kuhamia Jimbo la Uyole anaona ni kete kwake katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kutokana na ushawishi alionao kwa wananchi na kile alichofanya Mbeya Mjini.
“Uyole ametengeneza makundi yake, kuna wale bodaboda, wafanyabiashara na wajasiriamali, wanamkubali sana kwa kuwa hata ofisi yake ipo huko, alishaandaa mazingira mapema kwa ajili ya uchaguzi.
“Kimsingi, ameacha pengo kule Mbeya Mjini na kazi ngumu kwa mgombea wa CCM ajaye, kama Sugu atagombea atawapa wakati mgumu kwa kuwa upinzani una nguvu pale mjini,” amesema mchambuzi huyo.
Anaongeza kuwa CCM kinapaswa kujifungia kufanya tathmini ya kumpata mbadala wa Dk Tulia katika jimbo hilo vinginevyo anaona upinzani ukirejea iwapo uchaguzi utakuwa huru, haki na uwazi kwa vyama vya upinzani.
Madiwani wanena
Diwani wa Kata ya Isanga ambaye pia ni Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa anakiri kuwa kuondoka kwa mbunge huyo jimboni humo ni pigo kwa kuwa alikuwa kiunganishi bora kwa chama na wananchi na alikuwa mstari wa mbele kupigania maendeleo.
“Ni uamuzi wa kuigwa, amefanya makubwa kwetu Mbeya Mjini, hivyo ni kama mzazi aliyepata mtoto mwingine, kwetu tutazidi kumpa na kumuomba ushirikiano, amekuwa kiongozi wa mfano mwenye kupenda kila mtu awe na maisha mazuri kwani amejitolea mengi,” amesema meya huyo.

Baadhi ya wananchi wakaimsikiliza Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson wakati akitangaza kugombea Jimbo la Uyole.
Diwani wa Kata ya Mwakibete, Lucas Mwampiki amesema ujio wa Dk Tulia katika jimbo hilo ni fursa kwake na wananchi wake kuamsha maendeleo huku akimpa sifa kwa kazi aliyoifanya Jimbo la Mbeya Mjini.
Amesema Dk Tulia ni mchapakazi, msikivu na kiongozi mwenye ushirikiano akieleza kuwa kutokana na nafasi aliyonayo kiuongozi ikiwamo Spika wa Bunge na Rais wa IPU inaenda kuchochea maendeleo zaidi.
“Siyo kwamba ana nguvu kiuchumi bali ni mtu mwenyewe moyo wa kujitoa, amekuwa kiongozi mtulivu, nitatumia fursa hii kunufaisha wananchi wangu wa Mwakibete na atarahishisha kazi yangu,” amesema Diwani huyo.
Dk Tulia alonga
Akizungumza na wananchi na wafuasi wa CCM, Mbunge huyo amesema haikuwa kazi raihisi kufikia uamuzi huo na ndio maana alishindwa kumtuma mwakilishi badala yake amefika mwenyewe.
Amesema pamoja na uamuzi huo, anawataka wananchi wa Jimbo la Mbeya Mjini kumchagua kiongozi na mtumishi ambaye ataendeleza maendeleo akieleza kuwa baada ya kuondoka yeye watakuja wengi.
“Wapo watakaokuja hapa nilipotoka, wapo watakaokuja ninapoenda japo wajipange, lakini rai yangu kwenu, watakuja wengi ila chagueni kiongozi, chagueni mtumishi ili kuendeleza maendeleo.
“Ipo miradi mikubwa ya maendeleo inaendelea ikiwamo stendi kuu ya mabasi, Soko Kuu la Sokomatola na mingine ambayo inahitaji kuendelezwa.
“Kwa hapa Mbeya Mjini mengi nimefanya, sasa ngoja niende kwingine kuongeza nguvu na kuweka mabadiliko kama barabara, maji, afya na mengine ila sijaawacha tutakuwa pamoja hakuna mtu anayeagwa hapa,” amesema mbunge huyo.
Hata hivyo, baada ya kuzungumza na wafuasi wa chama hicho, akifanya mkutano wa hadhara katika Shule ya Msingi Asanga Uyole akipokelewa na umati wa wananchi kwa shangwe.