Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MJEMA: Hii ndio tume ya maridhiano tunayoitaka



Moshi. Tume iliyoundwa kuchunguza matukio ya vurugu za Oktoba 29, 2025 imekuja na pendekezo la kuundwa kwa Tume ya Maridhiano, lakini swali linalogonga vichwa vya wananchi ni hadidu za rejea, sifa na muundo wake.

Wasomi na wananchi mbalimbali waliozungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili, wanatamani tume hiyo iwe ya ukweli na maridhiano kama iliyoundwa Afrika Kusini mwaka 1995 na wale watakaotajwa kuhusika wawajibishwe.

Katika ghasia za siku ya uchaguzi na siku zilizofuata, watanzania 518 waliuawa katika mazingira tofauti tofauti, majeruhi 2,390 na uharibifu wa mali za umma na binafsi ambazo zinakadiriwa kuwa na thamani ya Sh125 bilioni.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda yeye alienda mbali na kusema ili maridhiano yafanyike kwa ufanisi, ni lazima mamlaka zikiri kwamba kulikuwa na makosa yaliyofanyika na wahusika wawajibishwe.

Tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiongozwa na Jaji mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, ilikamilisha kazi yake na kukabidhi ripoti yake kwa Rais Aprili 23, 2026 ikiwa na mapendekezo ya muda mfupi, wa kati na mrefu.

Kwa mujibu wa hotuba ya muhtasari wa ripoti hiyo, maridhiano na muafaka wa Kitaifa ni hatua muhimu katika kuponya majeraha na kurejesha amani, kuaminiana, mshikamo na utengamano ndani ya jamii na taifa kwa ujumla.

“Maridhiano yanapaswa kuwa mtambuka yakijumuisha nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kutathmini zaidi ukweli, kuponya majeraha, kutafuta suluhisho na kufikia muafaka wa kisiasa, kukubaliana juu ya msingi na mambo yanayohusu Katiba Mpya na kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa,” alisema Jaji Chande.

Kutokana na hayo yaliyojiri na ili kuliponya taifa na majeraha ya vurugu za Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata, tume imependekeza Serikali iunde Tume ya Maridhiano na Muafaka wa Kitaifa, kupitia mamlaka ya Rais chini ya Ibara ya 36.

Imetaka Tume iwe shirikishi na itakayosimamia na kuongoza maridhiano katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kutathmini zaidi ukweli na kutafuta suluhisho na muafaka wa kisiasa, na kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Tume imependekeza liundwe Baraza la Wazee la Ushauri litakalojumuisha baadhi ya viongozi wakuu wastaafu pamoja na wazee wengine wenye kukubalika katika jamii na wenye uzalendo ili kuisaidia Tume ya Maridhiano kunapotokea mkwamo.

Ni kutokana na mapendekezo hayo, wanazuoni na wananchi wametoa maoni mbalimbali juu ya muundo na sifa za wajumbe na kutahadharisha kuwa isiwe ni tume inayoundwa kusafisha wakosaji au kufunika kombe mwanaharamu aipite.

Baadhi ya wananchi wanapendekeza iundwe Tume inayofanana na iliyoundwa Afrika Kusini Kusini mwaka 1996 chini ya Askofu Desmond Tutu, kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu katika zama za ubaguzi wa Makaburu.


Tume ya Afrika Kusini

Tume ya Ukweli na Maridhiano au The Truth and Reconciliation Commission (TRC), iliundwa mara baada ya kumaliza kwa utawala wa ubaguzi wa rangi uliokuwa ukifanywa na makuburu wa Afrika Kusini, ambao waliokuwa wakiongoza Serikali.

Ikiongozwa na Askofu Desmond Tutu, TRC iliwaalika mashahidi ambao walitambuliwa kama waathiriwa wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, kutoa taarifa kuhusu uzoefu wao, na baadhi walitoa ushuhuda wao hadharani.

Wale waliotajwa kuhusika na matendo ya ukiukwaji wa haki za binadamu pia waliweza kutoa ushahidi na kuomba msamaha kwa mashtaka ya madai na jinai na Tume ilichunguza matendo yaliyotokea kati ya mwaka 1960 na mwaka 1994.

Kwa mujibu wa Wikipedia, TRC ilipewa mamlaka ya kutoa msamaha kwa wahusika wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi, mradi tu uhalifu huo ulichochewa kisiasa, sawia, na kufichuliwa kamili na mtu anayeomba msamaha huo.

Tume iligundua kuwa kulikuwa na vifo 7,000 vya kisiasa chini ya ubaguzi wa rangi kati ya mwaka 1948 na 1989 na kati ya vifo hivi, baadhi vilitokea wakati waathirika wakiwa kizuizini mikononi mwa polisi wa usalama na vyombo vya usalama.

Zaidi ya watu 19,050 walikuwa waathiriwa wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Waathiriwa zaidi 2,975 walitambuliwa kupitia maombi ya msamaha.

Jumla ya maombi 5,392 ya msamaha yalikataliwa, na kutoa 849 tu kati ya 7,111.

Ukiacha Afrika Kusini, zipo nchi za Afrika ambazo nazo ziliwahi kuunda tume inayofanana kwa kiasi fulani na TRC ikiwamo Uganda iliyoundwa kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo uliofanyika 1986 hadi 1995.

Nchi nyingine ni Nigeria ambayo mwaka 1999 iliunda Tume iliyojulikana kama ‘Human Rights Violations Investigation Commission Oputa Panel’ kwa ajili ya kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na wanajeshi.

Mbali na nchi hizo, lakini Julai 2002, Sierra Leone nayo iliunda Tume inayofanana na TRC kuchunguza mauaji yaliyotokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Nchi nyingine ni Liberia (2006), Kenya (2008), Rwanda (1999) na Gambia (2017).


Walichokisema wachambuzi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Richard Mbunda alisema ili maridhiano hayo yafanyike kwa ufanisi na uwazi, ni lazima mamlaka zikiri kwamba kulikuwa na makosa yaliyofanyika na wahusika wawajibishwe.

“Ni lazima mamlaka zikiri kulikuwa na makosa yaliyofanyika na waliohusika wawajibishwe ili kufanikisha maridhiano,” anasema Dk Mbunda.

Dk Mbunda alisema maridhiano hayo yatafanikiwa endapo Tume husika itapata wawakilishi kutoka katika makundi yote yaliyojeruhiwa, jambo litakalowezesha kupatikana kwa suluhu ya kudumu kutokana na yaliyotokea Oktoba 29.

“Ili maridhiano yafanyike ni lazima Tume hiyo ipate wawakilishi kutoka makundi yote yaliyojeruhiwa, wapate suluhu ya kudumu kutokana na kile kilichotokea. Hiyo ndio njia pekee ya kuponya majeraha,” anasema mwanazuoni huyo.

Kwa mujibu wa Dk Mbunda, makundi hayo ni pamoja na taasisi za kidini, asasi za kiraia, vyama vya kisiasa, vyombo vya habari hasa vya mitandao ya kijamii na wataaluma, akisisitiza kuwa yameathirika kwa kiwango kikubwa.

“Makundi haya yameathirika kwa kiwango kikubwa, hivyo ni muhimu yahusishwe kikamilifu katika mchakato wa maridhiano,” anasema.

Pia, ametaja makundi mengine kuwa ni wafanyabiashara hasa wamachinga, wazee waliothubutu kuzungumzia masuala muhimu, pamoja na vijana.

“Wafanyabiashara hasa wamachinga, wazee na vijana nao wameathirika kwa kiwango kikubwa, hivyo ni lazima wawe na wawakilishi katika mchakato huu,” alisema Dk Mbunda katika mahojiano hayo maalum.

Kwa upande wake, Lugete Mussa, mchambuzi wa masuala ya siasa anasema ili kufanikisha hilo ni lazima makundi ya kubali kuzungumza na kuaminiana.

“Kilichopo nchini ni tatizo hakuna hali ya kuaminiani lakini upande mwingine hautaki kuzungumza ukweli ni vigumu kupata muafaka ikiwa hali hiyo itaendelea. Lazima ukweli usemwe wote bila kumwonea mtu,” anasema Mussa.


Wananchi wanataka nini

Mkazi wa Pugu, jijini Dar es Salaam, Francis Mashaka anasema angependa kuona Tume ya Maridhiano inaongozwa na dhamira ya kweli ya kuliponya taifa na siyo kufunika mambo ili mradi ionekane jambo fulani limefanyika.

“Wanasiasa ni wajanja, wanaweza kuunda hiyo Tume lakini isifanye kazi ya kutibu majeraha mioyoni mwa watu, bali ikalinda maslahi ya watawala ya kufukia au kulinda uozo uliofanywa na baadhi yao,” anasema Mashaka.

Amesisitiza Tume hiyo ishirikishe makundi tofauti na mapendekezo yao yawe ni lazima kutekelezwa na Serikali, isiwe ni hisani ya kiongozi kuamua kutekeleza au kufungia kabatini kama ilivyoshuhudiwa kwenye Tume nyingi zilizopita.

“Watanzania tunataka Tume yenye dhamira ya kuleta hayo maridhiano, Tume inayojua hisia za Watanzania na yenye lengo la kuliponya taifa, nje ya hapo hakuna kitakachofanyika, watu wataendelea kuishi na maumivu yao,” anasema.

Anastazia Mollel ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Ngulelo Jijini Arusha, amesema muundo wa Tume hiyo usiwajumuishe wajumbe ambao wananchi watatilia shaka uadilifu huo kwani ikitokea hivyo wanaweza wasijitokeze.

“Wewe unadhani ile Tume ya Jaji Chande waathirika walijitokeza kikamilifu? Ingekuwa Tume Huru ya Kimataifa au yenye watu wenye uadilifu kwa rekodi zao kama Jaji Warioba (Joseph) ungeshuhudia mafuriko ya mashuhuda,” amedai.

“Lakini mule ndani ya Tume ya Jaji Chande zile sura tu na rekodi zao za nyuma katika utumishi wa umma zilikuwa hazileti hamasa ya watu kujitokeza. Hatutaki muundo wa Tume kama hiyo. Tunachotaka ni ukweli na uwajibikaji,” amedai.

Elibariki Massawe ambaye ni dereva bodaboda mjini Moshi, alitaka Tume hiyo ijumuishe makundi ya kijamii badala ya kuwa na sura zile zile ambazo baadhi ya wananchi wanaziona kama ni sehemu ya tatizo lililoikumba nchi Oktoba 29.

“Hatutaki sura zile zile hasa ikizingatiwa kuwa kiini cha zile vurugu ni mkusanyiko wa grievances (malalamiko) ya muda mrefu. Mie natamani Tume kama ile ya Afrika Kusini. Watu wajitokeza kueleza na waliokosea waombe msamaha,” amedai.

Hata hivyo, Massawe alisema ili maridhiano hayo yawe ya kweli, ni lazima kesi zote za kisiasa zifutwe na walioshtakiwa wote waachiwe akiwamo Tundu Lissu, akisema Lissu kuwapo uraini kuna maana kubwa katika maridhiano.

“Hii kumshikilia Lissu gerezani kwa hali yake ile inaongeza chuki kubwa sana. Wamwachie twende kwenye meza ya maridhiano tufungue ukurasa mpya. Kama tunataka kuridhiana basi kesi zote za kisiasa zifutwe,” ameeleza Massawe.

Grace Alex, mama Ntilie katika mji wa Moshi, alisema anatamani Tume kama iliyoundwa Afrika Kusini kwa sababu kupitia tume hiyo ukweli wote ulisemwa na waliohusika na matendo mabaya waliomba msamaha na kusamehewa.


Ahadi ya Rais na maridhiano

Baada ya kupokea ripoti ya Tume aliyoiunda kuchunguza ghasia za Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata, Rais Samia alisema Serikali itachukua hatua za haraka kwa kuunda Tume ya Maridhiano, ahadi aliyoitoa pia wakati wa kampeni.

Rais Samia alisema tume hiyo itazingatia pia ripoti hiyo ya Tume ya Jaji Chande ambayo imebainisha viashiria vya uwepo wa tuhuma za jinai, hatua ambayo inafanya Serikali kuhitaji chombo maalumu kuchunguza matukio ya kijinai.

Hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2025, Rais Samia aliahidi kuunda Tume ya Maridhiano ndani ya siku 100 akiingia madarakani, lakini ndoto yake hiyo ilitibuliwa na vurugu na ghasia zilizotokea siku ya uchaguzi na siku zilizofuata.