Uteuzi wa Makonda unaakisi shida ndani ya CCM

Uteuzi wa Paul Makonda kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, unasogeza tafakuri ngumu kuhusu kesho ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Makonda, alikuwa Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (Nec) CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo.

Jenga tafakuri; Rais Samia Suluhu Hassan, anapenda kila mara kumwita Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, kumpa maagizo ya kutoa taarifa ya mabadiliko ya kila mara? Je, anajisikia raha kubadili watu au kutengua na kuteua wapya?

Yaani, Rais Samia anateua mtu kwa matakwa yake. Kisha yeye mwenyewe pasipo makosa yoyote, anaamua kumwondoa aliyemteua au kumhamishia kwingine. Ikiwa jibu lako ni hapana, basi utakuwa kwenye uelekeo wa kukubali kwamba kuna matatizo.

Utaunga mkono kuwa Rais Samia huteua watu kwa moyo mkunjufu, halafu anakosa matokeo anayoyataka. Ndipo, huamua kufanya mabadiliko ya mara kwa mara. Ukikubali hivyo basi ikupe mtazamo kwamba ‘nyumba inavuja’.

Rais Samia alipokamata usukani wa uenyekiti CCM, alijipambanua waziwazi kuwaamini vijana. Katibu Mkuu, Daniel Chongolo. Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka. Vijana kabisa. Kipimo cha juu cha imani.

Hadi sasa, Chongolo anaendelea kushikilia rekodi ya kuwa Katibu Mkuu CCM, mwenye umri mdogo zaidi. Pamoja na hivyo, Chongolo alijiuzulu kwa kashfa ya mambo binafsi ya kijamii, hivyo kuacha wazi nafasi iliyojazwa na Dk Emmanuel Nchimbi.

Shaka alidumu mwaka mmoja Itikadi na Uenezi CCM, akampisha Sophia Mjema, mwanamke wa kwanza kuongoza idara hiyo. Hata hivyo, naye alikaa mwaka mmoja, kabla ya kuondolewa, halafu akaingia Makonda.

Jinsi mabadiliko ya mara kwa mara yanavyofanyika CCM, tena yakihusu vijana, yanadhihirisha kuwa chama hicho kina changamoto kubwa ya viongozi wa kesho. Mtazamo huo, siyo tu unaonesha CCM inavuja kwenye eneo la viongozi vijana, bali pia unadhihirisha kuwa nchi ipo njiapanda.

CCM, kama chama cha siasa, pamoja na itikadi, falsafa, nadharia, sera, mipango na chochote chenye kukipambanua kuwa taasisi yenye kujenga matarajio bora kwa wananchi, siasa za sasa zinataka taswira yake ijipambanue kuwa tabaka la viongozi.

Chama cha siasa kinatakiwa kijipambanue kuwa chenyewe ni benki ya viongozi. Chama kionekane kinasimama mstari wa mbele na kujitangaza kuwa ni taasisi yenye akiba pana ya viongozi, leo na hata kesho.

Inapotokea Rais Samia anaamini vijana, halafu baada ya muda mfupi anawaondoa, inakuwa dhahiri kwamba ama CCM ina uhaba wa vijana walioiva kiuongozi, au hakuna kabisa. Lolote kati ya hayo ni janga zito.

Thamani ya chama cha siasa za mamboleo ni utajiri wake wa viongozi. Chama ambacho kina kada pana ya viongozi wanaoonekana wamejiandaa au kuandaliwa kuongoza wenzao,  hicho kina nafasi kubwa ya kuchaguliwa kwa mihula mingi ijayo.


Kunani UVCCM?

Oktoba 2, 1920, kiongozi wa zamani wa Urusi na Dola ya Umoja wa Kisovieti (USSR), Vladimir Lenin, alihutubia Jumuiya ya Vijana wa Kikomunisti wa Urusi na kueleza kuwa majukumu ya jumuiya yoyote ile ya vijana, yanapaswa kuwekwa kwenye neno moja; Kujifunza.

Lenin ambaye jina lake ndilo ambalo limebeba dhana, falsafa na itikadi za kisiasa za Leninism, aliwaambia vijana wa jumuiya hiyo kwa wakati huo kuwa pamoja na kila kitu, wanatakiwa kujifunza na kuziishi itikadi za kikomunisti ili waweze kuutetea ukomunisti dhidi ya ubepari.

Aya hizo mbili, zinatosha kutoa tafsiri ya kile ambacho Lenin alikisema, ni kwamba jumuiya za vijana zipo kwa ajili ya maandalizi ya vijana kuwa viongozi bora kupitia itikadi na falsafa ambazo wanapitishwa katika makuzi yao ya kiuongozi.

Mwaka 1944, mashujaa wa wakati wote wa Taifa la Afrika Kusini, Ashley Peter Mda, Walter Sisulu na Oliver Tambo, walipokuwa wanaanzisha Jumuiya ya Vijana ya ANC (ANC Youth League), walieleza malengo yake kuwa jumuiya hiyo ifanye kazi kama kiwanda cha kuchakata fikra za vijana ili wawe viongozi bora wa kizazi kipya.

Kitabu kuhusu uanzishwaji wa Jumuiya ya Vijana cha chama tawala cha Namibia, Swapo (Swapo Youth League), kinaeleza kuwa madhumuni yake ni kuwapika vijana kuwa wanajeshi imara wenye kujifunga mkanda kwa ajili ya kutetea itikadi za Swapo, vilevile kuwa viongozi wazuri nyakati zijazo.

Turudi kwenye tafsiri ya Lenin, ni kwamba palipo na kila jumuiya ya vijana, maana yake ni chuo cha mafunzo ambayo huwawezesha vijana kufuzu maono ambayo yanakuwa yamekusudiwa.

Hata Jumuiya ya Vijana ya Tanu (Tanu Youth League), na baadaye Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), shabaha yake ilikuwa ni kupika vijana kiitikadi, kiuongozi, vilevile kuwatengeneza kuwa wazalendo kwa nchi yao.

Hiyo ikawa sababu majukumu mengi yaliyokuwa yakitekelezwa na Tanu, wakati huo, kuingizwa kwenye mpango wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa wahitimu wa elimu ya kidato cha sita ili kuwajenga vijana kikakamavu, kuwa viongozi wazuri na wazalendo.

Jinsi ambavyo Rais Samia anavyopata shida na vijana anaowateua mara kwa mara, inaleta swali; kunani UVCCM? Ni kama malengo ya kuundwa kwake hayatimizwi au vijana wanaopita kwenye jumuiya hiyo hawaivi kiuongozi.

Je, viongozi wa CCM wanatambua dhima ya kuwanoa vijana kiuongozi? Wanawaacha vijana wanaojiunga UVCCM wajikuze wenyewe kiuongozi? Isije ikawa vijana wa sasa ni kama mawe, hata yapikwe kwa maji na moto mkali kiasi gani, hayaivi abadan!


Vyama vyote vya siasa vina jumuiya za vijana. Kuna vyuo, Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kivukoni) na Diplomasia. Vinaaminika kuwa chemchemi ya kujenga vijana kifikra, wawe viongozi wazuri kitaifa na hata kimataifa.

Kibaha, Pwani, kuna Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere (MJNLS). CCM kwa kushirikiana na vyama vya ANC (Afrika Kusini), Frelimo (Msumbiji), MPLA (Angola), Swapo (Namibia), Zanu-PF (Zimbabwe) na CPC (China), ni waasisi wa taasisi hiyo. Hata hivyo, haioneshi kukisaidia chama hicho katika kujenga vijana kuwa viongozi bora.