Mrithi wa Makonda CCM huyu hapa

New Content Item (3)
New Content Item (3)

Muktasari:

  • Ingawa ndani ya Chama cha Mapindizi kuna nafasi nne zinazohitaji kujazwa, mijadala ya wana CCM na Watanzania imejikita zaidi katika nafasi mbili za Uenezi na Naibu Katibu Mkuu hasa kutokana na umuhimu wake kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025.

Dar/mikoani. Nani kurithi mikoba ya Paul Makonda na Anamringi Macha? swali hili ndilo linalofanya macho na masikio ya Wana-CCM na Watanzania kuelekezwa katika vikao vya juu vya Chama cha Mapinduzi (CCM) vinavyotarajiwa kuanza keshokutwa Aprili 3, 2024.

Vikao hivyo vya kamati kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika cha ndani ya chama hicho, vitaanza keshokutwa jijini Dar es Salaam na tayari baadhi ya wajumbe wamekwishaanza kuwasili.

Vikao hivyo vinakutana kukiwa na nafasi nne wazi za wajumbe wa sekretarieti baada ya waliokuwa wakiongoza kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Nafasi hizo ni Naibu Katibu Mkuu-Bara, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho.

Fakii Lulandala aliyekuwa katibu mkuu UVCCM ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Gilbert Kalima aliyekuwa katibu mkuu Jumuiya ya Wazazi akiteuliwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga.

Kwa upande wa nafasi ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo aliyokuwa nayo Paul Makonda, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, huku Anamringi Macha aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa CCM (Bara) yeye akiteuliwa Machi 12 mwaka huu kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga na tayari alikwishaapishwa.

Ingawa ndani ya chama hicho kuna nafasi nne zinazohitaji kujazwa, lakini mijadala ya wana CCM na Watanzania imejikita zaidi katika nafasi hizo za Makonda na Macha, hasa kutokana na umuhimu wake kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025.

Nafasi aliyoiacha Makonda aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, inaonekana kuwa moto zaidi na baadhi ya makada wa chama hicho wanatajwa kuwa wanaweza kuiziba.

Katika kuonyesha bado CCM haijapata mtu wa kumudu nafasi hiyo, Tangu Rais Samia ashike wadhifa wa mwenyekiti wa Taifa wa CCM takriban miaka mitatu nyuma, nafasi hiyo imeshakaliwa na makada wa nne na aliyehudumu muda mfupi zaidi ni Makonda, akihudumu miezi mitano takriban siku 160.

Wengine ambao wameshika wadhifa huo ndani ya miaka mitatu ni Humphrey Polepole ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Cuba na Sophia Mjema ambaye sasa ni mshauri wa Rais masuala ya wanawake na makundi maalumu na Shaka Hamdu Shaka, mkuu wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.

Wanaotajwa kuwa huenda wakapata nafasi ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo ni waliowahi kuwa wakuu wa mikoa Amos Makalla (Mwanza), Ally Hapi (Mara) na John Mongella (Arusha).

Makalla na Mongella waliachwa kwenye nafasi hizo katika mabadiliko aliyoyafanya juzi Rais Samia Suluhu Hassan alipoteua, kutengua na kuhamisha wasaidizi wake mbalimbali. Taarifa ya Ikulu ilieleza wawili hao watapangiwa kazi nyingine.

Wengine wanaotajwa kuwa na uwezekano wa kuvaa viatu vya uenezi ni; Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM (UWT), Jokate Mwengelo na Mkuu wa Wilaya ya Momba, Kenani Kihongosi, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM.

Wakuu wa mikoa, Anthony Mtaka (Njombe) na Marthin Shigella wa Geita nao wanatajwa katika nafasi hizo hususan za uenezi.

Duru za kisiasa zinawaona Makalla na Mongella mmoja wao anaweza kuwa Naibu Ktibu Mkuu-Bara na mwingine Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi kutokana na haiba zao na umri.

Hawaonekana zaidi kwenye uenezi kutokana na kiti hicho kuhitaji zaidi vijana na hilo linathibitishwa na watangulizi karibu watano waliopita.


Mwenezi anayetakiwa

Kwa unyeti wa nafasi ya uenezi na kwa kuwa ndiyo inayobeba taswira ya chama, atakayemrithi Makonda anapaswa kuwa mtu mwenye uelewa wa kina juu ya siasa za watu wa tabaka la chini, kulingana na mtazamo wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Sabatho Nyamsenda.

Dk Nyamsenda amesema tabaka hilo ndilo lenye idadi kubwa ya watu na kwa namna lilivyo ni kama limeachwa bila mtetezi, hivyo anayehitajika ni yule atakayelimudu kundi hilo.

Mwanazuoni huyo ameweka wazi kuwa mwenyekiti aliyepita wa chama hicho, John Magufuli alifanikiwa kujenga ushawishi mkubwa kwa kundi hilo na ndipo umaarufu wake ulipotokea.

Lakini kwa sasa, amesema ndani ya chama hicho kuna mnyukano wa makundi mawili, lile linalosimamia misingi ya Magufuli na lingine la mtandao.

Kundi la mtandao, amesema ndilo lile lenye wana-CCM wa muda mrefu likihusisha wafanyabiashara wakubwa, wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, lakini wanahusishwa na vitendo ama vya ufisadi na kukandamiza wanyonge.

Kwa upande wa kundi linaloshinikiza kuendelezwa kwa misingi ya Magufuli, amesema ndilo lile linalotaka kusimamiwa kwa masilahi ya watu wa tabaka la chini.

“Atahitajika mtu anayefahamu si kwa kuigiza, afahamu kwamba watu wa tabaka la chini wanahitaji nini ili kukisukuma chama chake kiende mbele na awe na nguvu ya kukishinikiza chama chake kifuate hilo la kuangalia masilahi ya watu wa tabaka hilo,” amesema Dk Nyamsenda.

Kwa mtazamo wa mwanazuoni huyo, CCM inahitaji mwenezi mwenye uwezo wa kuleta upatanishi wa makundi hayo mawili yanayokinzana ndani ya chama hicho.

“Tumeona makundi hayo yameonekana waziwazi hivi karibuni na kusababisha Katibu Mkuu wa chama hicho (Daniel Chongolo) aondolewe kwa kashfa ambayo huwezi kuelewa kwa chama kilichoshika dola kama kina shida ya kumuondoa katibu mkuu kwa kumdhalilisha namna ile,” amesema.

Kinyume na kupatikana kwa mtu mwenye uwezo huo, ameeleza baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 huenda chama hicho kikaingia kwenye mpasuko mkubwa.

Sifa nyingine, amesema anahitajika mtu mwenye uwezo wa kufanya tafiti, kujibu hoja na mwenye haiba inayoweza kuwajibu wapinzani bila kutegemea vyombo vya dola.

“Bahati mbaya hiyo haina mtu,  aliyekuwa nayo alikuwa ni Humphrey Polepole, unaweza usimpende kwa jambo fulani lakini ni mtu ambaye uwezo wake wa kufanya tafiti ni mkubwa mno,” amesema.

Novemba 27 mwaka jana, Chongolo aliandika barua kwenda kwa Mwenyekiti wake, Rais Samia ya kujiuzulu wadhifa wake. Ombi hilo liliridhiwa na Rais Samia siku iliyofuata yaani Novemba 28.

Katika barua hiyo, Chongolo alijiuzulu kwa alichokifafanua kuwa anachafuliwa katika mitandao ya kijamii.

Miezi mitatu baada ya kujizulu kwake, Machi 9 mwaka huu, Rais Samia alimteua Chongolo kuwa mkuu wa mkoa wa Songwe, kuchukua nafasi ya Dk Francis Michael aliyewekwa kando.


Kuhusu wanaotajwa

Kuhusu wanaotajwa kurithi nafasi hiyo, Dk Nyamsenda amemtolea mfano Makalla akisema kwa wadhifa huo, mwanasiasa huyo ameshapitwa na wakati, badala yake apatikane mtu mwenye mvuto kwa vijana kwa kuwa ndilo kundi kubwa.

“Kwa hiyo mtu kama Makalla kushika nafasi kama hiyo haitasaidia. Kwa mbali mtu kama Jokate kwa kuwa ana uwezo mkubwa wa kutafiti lakini naye simuoni akiwa na uwezo wa kufanya siasa za amshaamsha kujibizana na wapinzani,” amesema.

Kwa upande wa Kihongosi, amesema si mzuri kwenye nafasi hiyo kwa kuwa amejikita zaidi kwenye propaganda, si mtafiti mzuri katika kujenga hoja.

Ameonya kuingizwa kwa watu wa namna hiyo, kutashinikiza wakatumie nguvu za dola kufanikisha kazi katika nyadhifa hiyo.

Akizungumza kuhusu hilo, Mwanahabari na mchambuzi wa masuala ya Siasa, Ezekiel Kamwaga amesema CCM inahitaji mtu mwenye nguvu ya kuunganisha wanachama.

Kigezo kingine ni mtu mwenye uwezo wa kukisaidia chama hicho kushinda uchaguzi ujao, bila kujali mazingira ya siasa za sasa.

“Watachagua mtu anayeaminiwa na Rais kwa sababu huu si wakati wa kupata mtu ambaye maneno na matendo yake yanapishana na mwenyekiti wa chama, mfano mwenezi aliyepita ukimtazama maneno anayozungumza ni tofauti na mwenyekiti wake, lugha zao zilikuwa zinapishana,” amesema Kamwaga.


Mtazamo wa makada

Makada wa CCM wanaona nafasi hiyo inahitaji mtu anayeweza kukabiliana na hoja za viongozi machachari wa upinzani kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu wake, Tundu Lissu na wabunge wa zamani, John Heche na Godbless Lema.

“Kwa siasa za sasa baada ya kifo cha Magufuli (John) na kuelekea chaguzi zilizo mbele yetu nakwambia tunahitaji katibu mwenezi aina ya Makonda, ambao wana uwezo wa kujenga hoja. Ndio hivyo Makonda kateuliwa RC,” alidokeza kada mmoja.

“Usisahahu mwenyekiti wetu ni mtu wa surprise (kufanya uamuzi usiyotarajiwa). Nani alijua kama atamteua Makonda kuwa Katibu wa Itikadi na sasa RC Arusha? Alifanya hivyo kwa Jokate Mwegelo kuwa katibu mkuu wa UWT,” alieleza kada huyo.

“CCM kwa sasa tunaangalia nani atatuvusha kwenye hiki kitimtim cha uchaguzi. Uchaguzi unaokuja ni mgumu sana, sio lelemama hasa kauli za Rais kutaka uchaguzi huru na wa haki. Chama kinahitaji safu yenye watu wa kujenga hoja na wenye msimamo. Hata Mtaka (Anthony-RC Njombe) anaweza”

Mmoja wa wabunge wa mikoa ya Kanda ya Ziwa aliliambia gazeti hili kuwa mwingine anayetajwa kuwa anaweza mikiki mikiki ya kisiasa kwa sasa ni  Kheri James aliyewahi kuwa mwenyekiti wa UVCCM Taifa ambaye sasa ni mkuu wa wilaya ya Iringa.

Ukiacha nafasi hiyo, wapo wanaotajwa kumrithi Macha ambao ni pamoja na RC Mtaka, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela ambaye ameachwa katika uteuzi wa juzi kwa kile kilichoelezwa atapangiwa kazi nyingine, mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigella.

Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Juma Issihaka na Tuzo Mapunda (Dar)