Wafuasi Chadema wamzomea Ryoba, wamuita ‘yuda msaliti’

Sehemu ya watu waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema mjini Mugumu wilaya ya Serengeti.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Samuel Ghati amsema chama hicho kimepitia wakati mgumu baada ya viongozi wa wilaya hiyo akiwemo Mbunge kuhamia Chama cha Mapinduzi wakati wa utawala wa Serikali ya awamu ya tano.

Serengeti. Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Samuel Ghati amesema chama hicho kimepitia wakati mgumu baada ya viongozi wa wilaya hiyo akiwemo mbunge kuhamia Chama Cha Mapinduzi wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tano.

 Ameyasema hayo mjini hapa leo Machi 15, 2023 alipokuwa akifungua mkutano wa hadhara ambao unatarajiwa kuhutubiwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja na viongozi wengine.

Hata hivyo, wafuasi wa chama hicho wamemzomea aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo alipokaribishwa kupanda jukwaani.

"Wilaya yetu awali ilikuwa ni ngome ya Chadema lakini baada ya viongozi wetu kuhama kwakweli tulipitia wakati mgumu sana lakini kwa mwitikio huu naamini 2025 jimbo litarejea kwetu," amesema.

Amewataja viongozi wengine waliohama pamoja na Mbunge Marwa Ryoba ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa wilaya, katibu wa wilaya pamoja na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Baada ya kuyasema hayo Msemaji wa mkutano huo (MC) amemkaribisha aliyekuwa Mbunge wa Serengeti (Ryoba) ili aweze kusalimia wananchi hali iliyopelekea watu katika mkutano huo kuanza kuzomea na wengine kuimba yuda! Yuda!

Baada ya kupanda jukwaani Marwa Ryoba ambaye tayari alitangaza kurudi Chadena amesema kuwa yeye ni tofauti na Yuda wa kwenye Biblia.

" Mnaniita Yuda lakini mimi ni tofauti na Yuda wa kwenye Biblia yule alijinyonga lakini mimi niko hapa na nimetubu mchana kweupe," amesema huku akiamsha shangwe na vigelele uwanjani hapo.

Amesema kuwa alihamia CCM kulingana na hali ilivyokuwa, huku akitolea mfano Godbless Lema na Tundu Lissu waliokimbia nchi kutokana na misukosuko ya kisiasa.

"Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni mimi ndiye mbunge niliyefanya makubwa katika jimbo hili lakini naomba mjue kuwa mimi ni muoga lakini sio mjinga," amesema.

Amewataka wana Serengeti kuachana na yaliyopita na wajiunge pamoja kukijenga chama chao kuelekea katika chaguzi zijazo.