Wako wapi wazee wa CCM katika kipindi hiki?

Waziri na Mbunge mstaafu Stephen Wasira akihutubia moja ya mikutano ya chama hicho hivi karibuni. Picha na Maktaba

“Wako wapi wazee wa CCM?” Hilo ni swali linalogonga vichwa vya baadhi ya watu wanaofuatilia siasa nchini, hasa katika kipindi ambacho mjadala kuhusu mkataba wa makubaliano ya uendelezaji wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai ukishika kasi.

Miaka ya nyuma ilizoeleka kwamba kunapotokea dhoruba ya kisiasa, wazee wa chama hicho hujitokeza ama kukitetea chama na kushusha joto la kisiasa au kutoa mwongozo wa namna nzuri ya kufikia suluhisho, jambo ambalo kwa sasa halionekani.

Kwenye sakata la mkataba wa bandari, ingawa baadhi ya wazee wamejitokeza na kutoa maoni yao, lakini si miongoni mwa wale ambao chama hicho kimewakabidhi jukumu la kukishauri, ukiondoa Mzee John Malecela, makamu mwenyekiti-Bara aliyesema haoni shida ya uwekezaji huo na amewashangaa wanaopinga akisema ndiyo demokrasia inavyowaruhusu.

Wazee ni hazina ya chama kama alivyowahi kusema Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, hivyo kunapotokea dhoruba, wana nafasi ya kushauri au kujitokeza kwa umoja wao kukitetea ili kivuke salama.

Mwaka 2013, CCM iliunda baraza la wazee wa chama hicho likiwahusisha wenyeviti wastaafu, makamu wenyeviti wastaafu na makatibu wakuu wastaafu, ambao umma ungetamani kusikia kauli au ushauri wao katika kipindi hiki ambacho CCM na Serikali yake wanapambana kuelimisha umma umuhimu wa mkataba huo.

Kwenye suala la mkataba wa bandari, mbali na wazee wa CCM, wapo baadhi ya wazee wastaafu kama Joseph Butiku, Joseph Warioba na Profesa Anna Tibaijuka ambao wamejitokeza kuukosoa na kusimamia wanachokiamini.

Akizungumzia hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Bara, Anamringi Macha anasema vizazi vinabadilika na kwamba haiwezekani kuendelea kutumia wazee walewale kila siku wakati chama hicho kina hazina ya watu wengi.

Baraza la Ushauri CCM lilizinduliwa Agosti 23, 2013 na mwenyekiti wa CCM wakati huo, Jakaya Kikwete na baadaye baraza hilo likamchagua Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kuwa mwenyekiti wake wa kwanza, huku katibu wake akiwa Pius Msekwa.

Katika hafla ya uzinduzi wa baraza hilo, iliyohudhuriwa na wazee hao isipokuwa Makamu Mwenyekiti mstaafu - Zanzibar, Dk Salmin Amour kwa sababu za kiafya, Rais Kikwete aliwamwagia sifa wenyeviti wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Hayati Benjamin Mkapa kuwa ni sawa na kamusi ya mageuzi makubwa yaliyotokea nchini nyakati za uongozi wao.

Waliohudhuria uzinduzi huo ni Hayati Mkapa, Mwinyi, Msekwa, Malecela na Amani Abeid Karume.

Baraza hilo linalotambuliwa ndani ya Katiba ya CCM, lilitokana na mapendekeo ya kamati ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama iliyoundwa mwaka 2011 kwa lengo la kushauri namna ya kufanya mageuzi mbalimbali ndani ya chama.

Kikwete alisema wakati huo kwamba wao ndani ya chama, hawana hofu ya kuwatumia wazee hao kwa njia hiyo kwa kuwa itakuwa njia mwafaka ya kutoa ushauri wao kwa namna watakavyoona inafaa.

Alipuuza madai kwamba wazee hao wanaondolewa kwenye vikao vya uamuzi, akisema mbali na mapendekezo ya Kamati ya Mukama, pia wazee hao walikuwa wanachoka kuitwa mara kwa mara kwenye vikao.

“Tumekuwa tukiwaita kwenye vikao vyetu na wao wanahoji, ‘kwa nini mnatusumbua, nyinyi hamuwezi kuamua wenyewe? Sisi tumeshatimiza wajibu wetu na nyinyi timizeni wajibu wenu’,” alisema Kikwete.

Aliongeza kuwa hata kwenye vikao, wastaafu hao walikuwa wanaona taabu kuzungumza kwa kuhisi wangeweza kuonekana wanamwingilia mwenyekiti, jambo ambalo alisema halitakuwapo wakiwa peke yao, kwa kuwa watakaa na kuamua nini cha kushauri na namna ya kushauri.

Kutokana na maelezo hayo, wengi walitarajia kwamba viongozi hao wangejitokeza kuzungumzia mkataba huo kama utamaduni wao wa kukipambania chama hicho, hasa kinapopita kwenye nyakati ngumu kisiasa kama hizi.

Hata hivyo, ukimya wa baraza hilo umewaibua wachambuzi wakieleza sababu tofauti za ukimya huo, huku wakimulika namna baadhi yao walivyonyooshewa kidole wakati wa awamu ya tano na wengine wakiamua kupumzika.

Wachambuzi hao wa masuala ya siasa wana maoni tofauti kuhusu kutoonekana kwa baadhi ya wakongwe hao, huku baadhi yao wakisema huenda wanakwepa minyukano kwenye siasa, hivyo wamechagua kupumzika.

Wanakwepa minyukano

Akijadili ukimya huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema mabadiliko huwa yanatokea na kwa hali ilivyo sasa inategemeana na jambo lililopo na hali ilivyokuwa huko nyuma; kwanza, miaka ya nyuma kulikuwa na minyukano ndani ya hiyo taasisi.

“Mnyukano huo umewaacha baadhi ya watu hawana furaha, utakumbuka awamu iliyopita kuna baadhi ya wazee walitakiwa kuomba msamaha, wengine walifukuzwa, minyukano ile haikukiacha chama salama,” anasema Dk Loisulie.

Anasema athari zake zinaendelea kujitokeza na wakati wa awamu ya tano wazee hao walikuwa hawapewi heshima wanayostahili ndani ya chama hicho.

Pili, anasema jambo linalozungumzwa sasa la bandari linahitaji watu makini watakaozama na kuchambua vipengele ndani ya mkataba huo, hivyo anadhani wengine wanakwepa aibu kwa sababu jambo hilo lina masilahi ya umma.

“Kuna wengine wako kimya na wasingependa kujitokeza na kuna wanaoona aibu kwa sababu suala hili lina masilahi kwa umma. Hii ni sababu ya baadhi yao kuendelea kukaa kimya,” anasema mwanazuoni huyo.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora nchini, Buberwa Kaiza anasema huenda baadhi ya wazee wanakaa kimya kwa kuwa wana posho zao na wanalipwa kwa mujibu wa sheria kwa kuwa ni viongozi wastaafu.

“Hawa hawahitaji kuonekana ili wafanyiwe mambo fulani, lakini mtu kama Stephen Wasira asipoonekana hakuna atakayemkumbuka na inawezekana nafasi hizo ni fursa kwao ya kuonekana wanaunga mkono Serikali yao,” anasema Kaiza.

Wasira, waziri na mbunge mstaafu ni miongoni mwa waliojitokeza kuunga mkono mkataba na kuzunguka kwenye timu ya katibu mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kuutetea mkataba huo.

Kaiza anasema katika sakata la bandari, baadhi ya sauti zinazotoka ni zile za watu wanaotoka Tanzania bara wakipinga baadhi ya vifungu vya mkataba wa IGA, kwa mtazamo wa kisiasa huenda hawakubaliani na mkataba huo na wanakosa sehemu ya kusemea.

“Wakati mwingine wanaogopa wasionekane kama wasaliti kwa kuwa sauti nyingi zinaonekana kutoka upande wa Tanganyika,” anasema Kaiza.

Akiwa na mtazamo tofauti, wakili wa kujitegemea, Rainery Songea anasema CCM ina mtaji wa watu wengi, hata kwenye sakata la bandari Wasira anaonekana kuwa mbele lakini kuna ambao wako chini wanafanya kazi, hao ni vigumu kuwajua.

“Historia inaonyesha katika matukio kama hayo kuna mtu wanamweka mbele anaonekana na kuna viongozi wengine wa kichama wanakuwa nyuma yao, Wasira yuko mbele kwa sababu anajua kujibu na kupangua hoja,” anasema Songea.

Mchambuzi huyo wa siasa anasema chama hicho kinaona Wasira ana uwezo wa kukipigania na kwa kuwa amekuwa nje ya ulingo wa siasa kwa muda, akipata fursa kama hiyo anaitumia vizuri ili kumrudisha kwenye majukwaa ya ushindani.

Wazee wengi

Hoja ya Wakili Songea inaungwa mkono na Macha, anayesema CCM ina wazee wengi ambao wanakisaidia chama, lakini kwa suala la mkataba wa bandari, wameamua kumtumia Wasira pekee.

Macha anasisitiza kuwa vizazi vinabadilika na kwamba haiwezekani kila siku waendelee kutumia wazee walewale wakati chama hicho kina hazina ya watu wengi.

“Wazee hawajakaa kimya, isipokuwa kizazi kinabadilika. Haiwezekani waliozoeleka wawe waongeaji wa kudumu tu, chama hiki kina hazina ya watu wengi na Wasira wakati anatembea alikuwa na jopo la watu wengine,” anasema kiongozi huyo.

Anasema licha ya Wasira kuwa mstari wa mbele kwenye suala la mkataba wa bandari, alikuwa anaambatana na Chongolo pamoja na jopo la watu wengine walioandaliwa kwa ajili ya kuzungumza na Watanzania.

“Walikuwa watu mahsusi walioandaliwa na chama kuongelea suala hilo na tuliandaa mpango, linatakiwa kuongelewa kwa mfumo upi? Si kila mtu alipaswa kwenda kuongelea, lakini chama hakikuzuia mtu mwingine kuongelea isipokuwa tuliona ni vizuri kukawa na watu maalumu wa kuwaeleza Watanzania,” anasema.

Naibu katibu mkuu huyo anasema miongoni mwa watu maalumu waliochaguliwa na chama hicho alikuwa Wasira, akiongozwa na katibu mkuu pamoja na watu wengine, na walifanya hivyo kwa makusudi na si bahati mbaya.

“Tuna mtaji wa makada wengi na mnaowaona wamekaa kimya, wakati ukifika watakuwa wanaongea, si lazima watu wawazoee watu fulani tu,” anasema Macha.