Waraka wangu kwa Joni Kanywaji Mugful

 Nkwazi Mhango

Nakusalimia na kukuandikia waraka wa kumbukizi baada ya kuanza kusahaulika kirejareja na kirahisi. Kwa niaba ya mafyatu wote akiwamo Bi Mkubwa wako, nachukua fursa hii kuzoza nawe hata kama hutajibu. Niende kwenye inshu.

Zimebaki siku mbili kuadhimisha miaka mitatu ya kuondoka kwako. Ulipofyatuka, walitufyatua changa la macho kuwa pengo uliloacha lisingezibika. Urongo mtupu. Sijui nani ataziba lao. Mbona lilizibika zamani hata kabla ya mwili wako kuoza?

Si hilo tu, hata ile miradi uliyozoea kuiita yako si yako tena. Wanapewa ujiko wengine ambao hawakuwa wala hawana maono, usongo na uzalendo kama wako. Kumbe asiyekuwepo na lake halipo? Pamoja na ukali wake, hata mzoga wa simba hugugunwa na panya na kunyonywa na machawa.

Madege uliyozoea kununua kwa cash kama vitumbua hayaongezeki ila matanuzi. Tunashangaa kuona dude linaopaswa kukatiza dunia likitumika kwenda kununua vitafunwa mikoani na matanuzi mengine uliyochukia.

Hata majipu uliyozoea kutumbuatumbua sasa hayatumbuliwi. Yapo mengi tu. Yanazidi kuumuka na kunuka. Hakuna daktari wa kuyatumbua. Kwa sasa, tuna madoktari feki wasioweza kutumbua hata chunusi. Siku hizi, kuna machawa. Twangojea kunguni.

Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa njuluku za mafyatu kila mwaka inaripoti upigaji wa kutisha. Hakuna anayetumbuliwa. Sijui kama wanagawana wote kuanzia chini hadi juu, vinginevyo maza angekasirika angalau akatumbua japo wachache lakini wapi.

Kabla sijasahau, siku hizi wenzi, wenza, sijui wake wenza wa wanene nao wanapiga mshiko na kuzidi kuwasikinisha mafyatu. Hata juzi, kuku wangu naye alitaka apewe mshiko kwa sababu mimi ni mnene wa mafyatu wanaofyatuliwa kirahisi wakaufyata badala ya kuufyatua na kufyatua wanaowafyatua.

Kabla sijasahau, ile SgR yako ipoipo. Juzi ilianza kufyatukafyatuka na kufanya majaribio ambayo hatujui lengo wala mwisho wake.

Bandari ya Bongo ishakwenda kwa deep weed ya Do buy inayonunua kila kitu kuanzia mafyatu, hewa, hata maji. Mambo yanazidi kunoga na kubadilika japo si kwa kufurahisha. Kile kikaragosi chako ulichokichonga na kukiita Bashiti baadae ukakiteketeza kilipoanza kukutisha, nacho kimefufuliwa na kinatanua kuliko hata yule uliyempa ulaji.

Kinafyatukafyatuka kikiwatapeli mafyatu kuwa kinawajali na kuweza kutataua mataizo yao. Kinazoza kama rahis na kinawapata kwa sababu wamekata tamaa, kufyata au kuunga juhudi kwa pambio na nyimbo badala ya kufyatuka na kufyatua.

Wale vihiyo au waloghushi uliowatumbua sasa wanatesa bila wasiwasi. Siku hizi kila fyatu anataka aitwe ama daktari au profesa hata kama hakufika darasa la saba. Mie hupenda kuwaita madoktari na maprofedheha kama yule aliyekuita Mungu.

Hata hivyo, alishawekwa pembeni. Yule Mnyalukolo Bill za Luku Ukuvi, ashawekwa pembeni. Kwanini hukumtumbua pamoja na kujua alituhumiwa kughushi vyeti vyake vya kitaaluma kama kibashiti?

Siku hizi kuna mgao wa kila kitu kuanzia hewa, umeme, maji mpaka sukari hata uroda. Hata ile Chato yako uliyoiacha siku hizi inakufa taratibu. Ule uwanja wako wa ndege na Chato vinaanza kugeuka Gbadolite kama ile ya jambazi wa Kongo Mombuto.

Mbuga ya Burigi-Chato ndo usiseme. Biashara zimedoda kiasi cha kuzidiwa hata Kizimkazi. Bwawa la Mzee Mchonga nalo linasusuasua kiasi cha mgao wa umeme kugeuka fasheni. Mambo yamebadilika na kuharibika sana.

Maswahaba zako kama yule doktari nshomile uliyekuwa ukimteua kila mara ashawekwa kando sambamba na homeboy wako doktari Keleman.

Harmfully Slowslow alishashushwa na kupandishwa wengine hasa wale uliowahi kuwanasa wakikunanga kwenye simu. Bi mkubwa wako kapotea na anaanza kusahaulika. Hata mie ninayekukumbuka simkumbuki. Hayo tuyaache.

Ukiachia hayo, Mzee Ruxa ameaga juzi siku chache baada ya Eddie Luwasha. Nadhani mshaonana. Cha mno, mafyatu wasiojulikana waliiokuwa wanapoteza mafyatu pingaji nao ima wamepotea au kuacha kale kamchezo.

Ukiacha hayo, siku hizi mazeri ni doktari na kila fyatu anataka aitwe ima doktari au profesa. Hakuna anayeweza kutaja jina lake bila kuanza na doktari na sifa nyingine kibao.

Siku hizi wewe hutajwi. Hata kwenye tule tumiradi wanatajwa wao sio wewe uliyeanzisha. Hata mvua ikinyesha wanamshukuru mazeri. Yule profedheha aliyekuita Mungu ashawekwa kando zamani gani. Unamkumbuka Mr. Sipika Jobless? Alibwabwaja wakamfyatua.

Sasa yupo yule sister asiyetulia. Ana nyodo na anajua kila kitu hata kama hajui. Sijui kama hana mpango wa kuchukua ulaji kama kibashiti. Akina Tunda Lishe na wenzake nao wanafyatukafyatuka.

Dk Silaha uliyempa ulaji ughaibuni, ashabwagwa. Amererejea ulikomtoa. Hakika, hapo utakakumbuka kamsemo ka mafyatu kuwa kunguru hafugiki.

Nisikuchoshe na kukatisha usingizi wako wa milele. Kifupi, mambo si mambo. Siku hizi tuna dhana mpya kama vile kikokotoo, tozo, na kila aina ya visingizio vya kupigia njuluku za mafyatu bila kuwarejeshea chochote zaidi ya mateso na umaskini.

Hata hivyo, tunajikongoja tukishuhudia vimbwanga na vibweka kwa wanaobweka. Ili kuukata, lazima uunge mkono juhudi kama legacy uliyotuachia ambapo unene na umungu havina mpaka.
Kwa leo ni hayo. RIP Joni Kanywaji Mugful.