Zitto asisitiza nchi kuitumia chuma ya Mchuchuma, Liganga

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa chama, Juma Duni Haji (kushoto), Makamu Mwenyekiti Bara, Dorothy Semu (wa pili kulia) wakiwasili katika soko la Mitumbani la Makambako kwa ajili ya kushiriki mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika mkoani Njombe leo Jumatatu Mei 29, 2023. Picha na Erick Boniphace.

Muktasari:

  • Chama cha ACT- Wazalendo, kimesema kitaendelea kuibeba ajenda ya mradi Mchuchuma na Liganga hadi mradi utakapopata ufumbuzi wa kutekelezwa kwa sababu una manufaa makubwa kwa Taifa.

Njombe. Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amewaahidi wakazi wa Mkoa wa Njombe kuwa chama hicho, kitaendelea kusukuma mradi wa Mchuchuma na Liganga akisema ni ajenda yenye maslahi makubwa kwa Taifa.

 Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Mei 29, 2023 wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Soko la Mitumba uliopo katika Mji wa Makambako mkoani hapa.

"Tuwe madarakani au tusiwe madarakani tutaendelea kuisemea Njombe hasa mradi wa chuma kwa sababu ni muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Inashangaza tunaagiza chuma kutoka nje ya nchi wakati chuma kimelala Ludewa mkoani hapa," amesema.

"Tunajenga maghorofa, madaraja tunahitaji nondo yote haya tunaagiza kutoka nje wakati chuma kimelelala.Ingekuwa tunaongoza nchi tungeanza na mradi wa Liganga kwa sababu una manufaa makubwa," amesema Zitto.

Amesema ACT- Wazalendo inaposema 'Taifa la Wote kwa Maslahi Wote' wakiwa na maana kwamba rasilimali zilizopo ikiwemo chuma ziwanufaishe wananchi wote hasa wa Mkoa wa Njombe.


"Kuna wakati wabunge wenu mliochagua wanajaribu kusema lakini hawasemi.Kwa niaba ya watu wa Mkoa wa Njombe tutaendelea kuifanya ajenda ya Mchuchuma na Liganga kuwa ajenda ya kiasiasa kila wakati," amesema Zitto.

Kiongozi huyo,  amesema Njombe ni mmoja wa mikoa ambayo nilikuwa mstari wa mbele kuzungumza masuala ya mbele ikiwemo mradi ya Mchuchuma na Liganga ambao ulikuwa ni moja ya ajenda alioisukuma akiwa bungeni na bado ataendelea kufanya hivyo.

Mei mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan aliidhinisha  Sh15.4 bilioni fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa Mchuchuma na Liganga.

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Juma Duni Haji maarufu 'Babu Duni' amesema wapo katika ziara ya kuimarisha chama hicho ili kujiandaa na chaguzi za Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Amesema ACT- Wazalendo, inaitazama Tanzania miaka 60 ijayo na endapo wakipata ridhaa mwaka 2025 itakuwa 'Taifa la Wote, kwa Maslahi Wote'  ili kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali zilizopo.