Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zungu afunguka zuio mikutano ya hadhara

Muktasari:

  • Kauli ya Zungu inakuja ikiwa ni siku sita tangu Serikali ilipotangaza bungeni kusitisha utoaji vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vyote vya siasa, ikieleza kubaini kuwepo viashiria vya uvunjifu wa amani.

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu ameunga mkono uamuzi wa Serikali kusitisha utoaji vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, akisema ni hatua nzuri kutokana na kipindi kilichopo.

Kauli ya Zungu inakuja ikiwa ni siku sita tangu Serikali ilipotangaza bungeni jijini Dodoma kusitisha utoaji vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vyote vya siasa, kwa kile ilichosema imebaini kuwepo viashiria vya uvunjifu wa amani.

Juni 26, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camilius Wambura awaelekeze wakuu wote wa polisi, wasitishe utoaji wa vibali vya mikutano.

Katambi, alitoa kauli hiyo akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Dodoma Mjini, Pascal Chinyele, aliyetaka kujua iwapo Serikali inafahamu kuhusu kuwepo tetesi za maandamano na Spika Zungu akataka majibu yatolewe na Serikali.

Hata hivyo, uamuzi huo umekosolewa na baadhi ya wadau wa siasa na sheria wakisema umekiuka misingi ya demokrasia na uhuru wa kikatiba wa mikusanyiko.

Alipoulizwa msimamo wa Bunge kuhusu suala hilo leo, Jumatano Julai 1, 2026, Zungu amejibu kuwa waziri mwenye dhamana ndiye aliyetoa tamko hilo na Bunge halikuwa na cha kuongeza.

"Ukizingatia Sabasaba imeanza kuna wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali wanakuja nchini na kiitifaki ni muhimu ugeni unapofika ukute watu tupo kwenye furaha," amesema Zungu alikuwa anazungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya miaka 100 ya chimbuko la Bunge na hatua mbalimbali ambazo limepitia.


Ajitenga na suala la Yuda

Alipoulizwa kuhusu madai ya kuwepo Yuda yaliyotolewa na Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Simai Said Mohamed ndani ya Bunge, Zungu amesema mbunge anapokuwa ndani ya Bunge anakuwa na uhuru kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.

Ameeleza kilichosemwa na mbunge kuhusu suala la Yuda ni kile anachokiamini yeye na ameachwa na imani yake, kwa kuwa siyo kinachoaminiwa na Bunge.

"Kilichosemwa kakisema anakiamini yeye na sisi tumemwacha na imani yake. Anachokiamini yeye sicho tunachokiamini sisi," amesema Zungu.

Amesisitiza kuwa Bunge ni uwanja unaokuwa na mambo mengi, akilifananisha na uwanja wa mpira wa miguu.


Bunge kukosa hamasa

Alipoulizwa kuhusu Bunge kukosa hamasa na ufuatiliaji wa wananchi, Zungu amesema ni vigumu kuona hamasa wakati tayari kuna hatua kubwa za maendeleo zilizopigwa akitaka SGR, barabara, shule, vituo vya afya na mengineyo.

"Kazi ya Bunge ni ustawi wa wananchi. Bunge siyo vita bali linasimamia masilahi ya watu.

Hata hivyo, ameeleza wakati mwingine wanajitokeza wabunge wanaosimama kusema uwongo ilimradi kuvuta hisia za wananchi.

Amesema hakuna Bunge, lililokuwa kali, dhaifu wala zuri, yote hayo kazi yake ni kusimamia ustawi wa wananchi.

Spika wa Bunge, Mussa Zungu akizungumza katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Julai 1, 2026. Picha na Michael Matemanga

"Hakuna Bunge dhaifu, asikudanganye mtu. Na Bunge sio kugombana. Ukiona huko watu wanagombana jua hicho kitakuwa kilabu cha pombe," amesema.

Ametoa mfano wa wabunge wanaohoji maswali ya kuiwajibisha Serikali, akisema “Tunaye Ado (Shaibu, Mbunge wa Tunduru Kusini-ACT Wazalendo) pale na ana maswali mazuri tu, lakini ni mpinzani," amesema.

Kuhusu kupungua wapinzani bungeni, amesema mwaka 2015 wapinzani walipata kuwa na mgombea aliyekamilika na kuimarika kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyekuwa na nguvu na ushawishi na kuwafanya wapinzani kuchaguliwa kwa wingi wakafika 102

Lakini mwaka 2020 na 2025, amesema hawakuweza, licha ya sheria, katiba na Tume ya uchaguzi kuwa ileile.

Amesema kwa sasa vyama vya upinzani vina viongozi wazuri lakini hawajafanikiwa kuwashawishi wananchi wawachague wagombea wao, kiasi cha kufanikisha wawe wengi bungeni.

"Waliingiaje 2015 na washindwe kuingia mwaka 2025. Nasikia kuna baadhi wanasema tupeni nafasi na sisi tuongoze, walipewa nafasi 2015 lakini matokeo yake utendaji wao mmeuona wananchi wakaamua kurudisha wale wanaosimamia ustawi wa wananchi," amesema.

Amesema licha ya uchache wao usiowapa sifa ya kuunda kambi rasmi ya upinzani (asilimia 12.5) wenyewe wakiwa asilimia tatu, Bunge liliamua kamati mbili za usimamizi wa Serikali wapewe wao kwa mujibu wa utaratibu wa nchi za Jumuiya ya Madola.

Kamati hizo, ni ile ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Serikali za Mitaa (LAAC).

Amesema hizi kamandio ndio hushughulikia maoni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kuwaita wote waliotajwa na CAG kuhojiwa na CAG akiridhika na majibu, hoja husika hufutwa," amesema.


Agusia maandamano

Zungu, amesema ni vema kujiuliza hayo yote yameanzia wapi, akisisitiza hakuna kiongozi wa dini yoyote, mwananchi wala mwandishi wa habari anayesema nchi imewezaje kufika hapo.

"Mnanyoosha vidole eneo lisilo sahihi. Rais Samia huyu aliwarudisha wapinzani wote nchini. Baada ya pale kitu gani kilichowafanya hawa waliorudishwa waamue haya yaliyotokea," amesema.

Ameeleza Rais alitimiza wajibu wake kuwarudisha wapinzani, lakini wenyewe wameamua kufuata njia yao.

"Niwaombe sana, tuwe na Tanzania mpya ya ukweli na uwazi. Tutapata kwa matokeo ya tume zilizoundwa. Uamuzi ufanye nini, nani afanywe nini, tutajua," amesema.

Amesema kama hali iliyopo itaachwa pasi na kuepukwa, nchi itafika mahali watu wake watapambana kwa ukabila na udini.

"Tunaweza kurudisha nchi hii na tukapendana. Usinipende mimi penda kazi zangu, hatulazimishwi kupenda mtu lakini penda kazi zake," amesema.

Kuhusu kuzushiwa kifo, amesema mitandao inatumia taarifa za uongo kuhusu vifo vya viongozi ili kupata wafuasi, lakini kwake anaona kama nafasi ya kumwongezea uhai.

"Wakinitangaza nimekufa ni furaha yao, nitafanya nini sasa," amesema Zungu.


Miaka 100 ya Bunge

Kuhusu maadhimisho ya Bunge miaka 100 ya chimbuko la Bunge, Zungu amesema kilele chake kitakuwa Januari mwaka 2027 na yanafanyika kukumbuka Bunge lilikotoka lilipo na linakoelekea.

Amesema chimbuko la muhimili huo ni Machi 19, mwaka 1926 wakati Tanganyika ikiwa chini ya ukoloni wa Uingereza ndipo ilitungwa Sheria ya kuanzisha Baraza la Kutunga Sheria.

Baraza hilo, amesema lilizinduliwa katika Ukumbi wa Shule ya Aga Khan ambayo kwa sasa ni Sekondari ya Tambaza.

Baraza la kwanza, amesema liliundwa na wajumbe 20 walioteuliwa na sheria zilizotungwa zilipelekwa Uingereza kupata idhini ya mfalme.

Mabadiliko yalishuhudiwa kwa kuingia kwa Watanganyika ndani ya Baraza wakianza Chifu wa Wachaga na Wasukuma.

Amesema katika miaka 100, Bunge limekuwa nguzo muhimu ya Demokrasia.

Maadhimisho hayo, amesema yatahusisha tafakuri ya Bunge na kuweka dira kwa miaka ijayo.

Katika kipindi hicho, amesema Bunge limefanikiwa kwa kuwa na uwakilishi wa kutosha wa wanawake ambao kwa mwaka huu ni takriban asilimia 40, kiwango ambacho ni cha juu.

Amesema uwakilishi wa vijana umefikia wabunge 72 na sasa kimeanzishwa chama cha wabunge vijana Tanzania, huku wabunge wenye ulemavu wakiongezeka na kufikia 11.