Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Mwiba mdogo-10

Ilipoishia jana...

...Pale Mwanza alikuwa akimiliki hoteli za nyota tano zaidi ya saba na mabasi zaidi ya hamsini yaliyoandikwa SHIBANDIKO CLASSIC yaliyokuwa yakienda mikoa yote.


Endelea...

“Haloo.”

“Mkuu za siku?”

“Mbaya naona mnazidi kupukutika tu.”

“Yaani nazidi kuchanganyikiwa, nimebaki mimi, wakati wowote nayaona mauti mbele yangu,” Mabula alisema kwa sauti ya kukata tamaa.

“Ni hivi nimetuma vijana hapo nyumbani kwako naomba kuanzia muda huu usitumie kinywaji na chakula chochote kutoka kwa mtu yeyote. Pia wafanyakazi wako wote wape likizo ya wiki, hakikisha unawapa pesa ya kutumia kwa wiki mbili. Kuanzia sasa watakaokulinda watakuwa askari kuanzia mlinzi mpaka mpishi.”

“Sawa mkuu, kidogo hapo napata ahueni.”

“Pia hakikisha hukai sehemu za wazi ambayo itampa nafasi muuaji kukuua kwa urahisi kwa risasi. Kazini kwako usiruhusu mtu yeyote kuingia ofisini kwako hasa akiwa

mwanamke anayependa kuvaa nguo ya kuziba macho,  ni kiumbe hatari kuliko kifo.

“Kingine ukiwa ofisini usiache dirisha wazi kwa vile muuaji anaweza kuutumia mwanya huo kukumaliza. Ukifuata maelekezo yangu vizuri itatupa urahisi wa kumkamata muuaji kwani lazima atajipenyeza akijua atafanya kama kwa Joseph Maliki, hivyo kuangukia mikononi mwa askari na kushikwa kama kuku wa mdondo.”

“Nitakuwa makini, nikiongeza na ulinzi wangu binafsi sidhani kama atasogea hata kwenye nyumba yangu au ofisini.”

“Naomba unisikilize mimi, hapo kwako usiweke ulinzi wowote zaidi ya vijana wangu wenye uzoefu wa kuwadhibiti wakorofi kama muuaji.”

“Walinzi wangu ni zaidi ya walinzi wa ikulu,” Mabula bado aliamini walinzi wake wana ujuzi mkubwa.

“Lazima tutachanganyana na kumpa nafasi muuaji aweze kutumia kutojuana kukumaliza. Kuchanganya walinzi ndiyo iliyosababisha Joseph Makiki kufa kikondoo katikati ya lundo la walinzi.”

“Mmh! Sawa nitafanya hivyo mkuu.”

Baada ya kukubaliana nyumba ya Mabula ilifanyiwa usafi wa kitaalamu kuhakikisha vyakula vyote vilivyokuwa ndani vinatolewa kisha kuingizwa vipya vyenye vipimo vya hali ya juu vya kimaabara ili kuhakikisha Mabula hali wala hanywi maji yasiyopita mikononi mwa jeshi la usalama.

Kutokana na wingi wa kazi, Mpelelezi mkuu Shila alirudi nyumbani usiku mkubwa akiwa amechoka sana.

Vifo vya watu maarufu vilizidi kumchanganya huku muuaji akionekana kuvipanga vifo kwa umahiri wa hali ya juu. Ilionekana muuaji yupo hatua moja mbele ya kila wanalolifikiria. Simu ya mezani iliendelea kuita kwa muda bila kupokelewa, mkuu wa upelelezi Juma Shila hakushughulika nayo. Akili yote ilikuwa kwenye ripoti ya mauaji ya kutisha ya siku mbili mfululizo, yaliyomfanya asipate hata lepe la usingizi kumfuatilia muuaji bila mafanikio, huku muuaji akimgeuza mwanasesere wa kumchezea atakavyo.

Siku zote Mkuu Shila aliamini hakuna kiumbe cha kuchezea sharubu za simba. Mauaji yale yalimchanganya sana kwa mwanzo, aliona mauaji yale ya mafutini lakini kumbe alikuwa akijidanganya yale maji yalikuwa ya kuzamisha mnazi. Alijiuliza ametoa wapi uwezo mkubwa wa kijasusi wa kuwazidi maarifa wapelelezi mahiri, lakini aliamini dharau aliyoweka mwanzo ndiyo iliyopelekea yote yale kutokea.

Lakini aliamini nguvu ya Mwanza atamnasa muuaji kwa vile kikosi kilikuwa kimekamilika.

Aliamini mpango alioutengeneza Mwanza lazima muuaji anaswe kama panya mjanja kunaswa na mtego mbovu. Ilikuwa tofauti kazi aliyowatuma kina Maliki kuisha mapema kuliko alivyotegemea na kumpa nafasi ya kutumia kikosi cha Maliki na vijana wake ambao waliwasili Mwanza kuongeza nguvu kitu kilichompa nafuu kubwa Mkuu Shila kwa kuamini jeshi lililotua Mwanza lilikuwa kamili hata angekuwa Osama bin laden angetulia.

Baada ya Maliki na Queen kufika Mwanza waliangalia mazingira ya jumba la kifahari ambalo lilikuwa limewekewa ulinzi wa kisasa kukamata kiumbe chochote kitakachojipendekeza hata awe jini.

Maliki baada ya kufanya uchunguzi wa kina aliwapanga vijana wake kisayansi kuhakikisha hakipiti kitu kisha alimjulisha mkuu wake Dar es salaam.

“Mkuu huku kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa, nakuhakikishia labda asije, akiingia hatoki.”

“Maliki hakikisha haingii kama akiingia jua tumefeli, yule hatakiwi kuisogelea hata nyumba ile, yule binti usimchukulie poa,” Mkuu Shila alitoa onyo.

“Chifu najua una wasiwasi, lakini mchezo huu ni mwepesi kutokana na muuaji kujiamini na kuelekeza anataka kufanya nini.”

“Narudia tena muuaji usimchukulie poa hata kidogo, uwezo wake ni mkubwa sana hivyo umakini uongezeke mara mbili ya kawaida. Mwanzo niliona ngoma ya kitoto kumbe sivyo nilivyodhania, amekuwa akijiamini sana na kuapa lazima atimize idadi yake ambayo ataikamilisha leo.”

“Mkuu ondoa shaka, tumekutana na watu wanaotishia dunia lakini walitulia, sembuse huyu,” Maliki alizungumza kwa majigambo.

“Nina wasiwasi mtego mlioutega akautegua huenda anatujua vizuri, anajua tupo wapi, pia anajua mpo Mwanza, kitu kinachomfanya kujiamini sana. Siamini ni mtu anatumia mpango wa aina moja kuua. Huyu binti hana tofauti na Manka, lazima amejipanga, hakurupuki hata kidogo, lazima tufikirie mara mbili yake.”

“Najua mkuu, tumeongeza ulinzi na umakini.”

“Ni kweli kabisa inaonekana anajua kutumia silaha za aina zote, pia ana shabaha ya hatari.”

“Nakuhakikishia akiingia hatoki, huwa sitaki kuchezewa akili na mtoto mdogo, japo tumechoka kazi hii itakuwa nyepesi sana, we subiri majibu, sijawahi kufeli nikipanga mipango yangu.”

“Chui, humjui ni binti anayeonyesha yupo tayari kufa kwa ajili ya kulipa kisasi cha wazazi wake. Mtu asiyejali kupotea ni mtu hatari sana tena sana.”

“Mmh! Basi tuwe makini, tukifanya makosa anaweza kuondoka na mtu.”

“Umeona, nina imani yupo Mwanza pengine anawaona kila mnalilofanya na mkifanya kosa basi tumeumia.”

“Chifu kazi ngumu ndizo zinazotupa mzuka.”

“Basi nikuacheni mmalizie kazi kisha mrudi mpumzike mchague mnataka kwenda wapi kupumzika. Ooh! Nilitaka kusahau mkuu anawasubiri kuna zawadi yenu kubwa sana.”

“Yote tukimaliza kazi nzito iliyo mbele yetu, nimeingiwa wasiwasi baada ya muuaji kuonyesha anajiamini na kufanya alichokitaka huku akikueleza atafanya nini na anafanya. Mtu kama huyo ni hatari japokuwa nina imani muuaji siyo yeye bali anamlinda mhusika.”

“Chifu hata mimi mwanzo niliwaza hivyo, matukio ya karibu yameonyesha muuaji ni yeye mwenyewe. Nikueleze kitu kingine alichokisema yule binti kuonyesha amedhamiria kulipa kisasi.”

“Kitu gani mkuu.”

“Inavyoonekana anajua uwezo wenu kuwa hatoboi, hivyo anajua wazi leo atakamatwa, hivyo amesema hata tukimkamata kabla ya kukamilisha hesabu yake lazima atatoroka gerezani na kuja kumuua kisha atajisalimisha mwenyewe na kuwa tayari kunyongwa.”

“Duh! Kweli ana hasira.”

“Alilonimaliza zaidi ni pale aliposema mmoja kati ya adui zake angekufa bila kupitia mkono wake basi angemfukua na kumuua mara ya pili ili kutimiza hesabu yake.”

“Duh! Kweli inaonekana kumzuia yataka kazi ya ziada, tunatakiwa kuhakikisha hamfikii Mabula, nina imani akifika mbele yake akitoa silaha hawezi kuirudisha, yupo radhi afe lakini amuue adui yake.”

“Kama ulivyosema tufikirie mara mbili yake.”

“Basi mkuu nikuache, nina kikao na vijana wangu ili tujadili kwa kina uwezo wa adui yetu na jinsi ya kumdhibiti bila kumwaga damu ya mtu yeyote.”

Baada ya kukata simu Mkuu Shila aligeuka na macho yake kutazama kioo cha kompyuta kupitia taarifa kutoka Geita.

Alisoma taarifa ile kwa umakini mkubwa kwa kufungua ukurasa mmoja hadi mwingine iliyokuwa ina maelezo mengi ya kusisimua na kusikitisha. Kabla hajaendelea kusoma, mlango wa ofisi ulifunguliwa na kuingia katibu muhtasi na kusimama mbele yake kikakamavu.

Mkuu wa upelelezi aliacha kusoma na kunyanyua macho kumtazama bila kusema neno.

“Chifu,” Sanjenti Suzana alimwita.

“Ndiyo Suzy.”

“Bosi mbona hupokei simu?”

“Suzy nilikuwa napitia taarifa kutoka Geita ambayo inatakiwa utulivu mkubwa kuisoma kwa makini.”

“Bosi hata mimi nakuonea huruma, kuna taarifa nyingine imeingia muda mfupi.”

“Taarifa gani tena Suzy?” mkuu wa upelelezi alishtuka.

“Mtoto wa marehemu anakupigia simu anasema pokea.”

“Dah! Kaishafanya tena mauaji, kweli huyu binti si wa kawaida pamoja na mitego kabambe ya kina Maliki ametegua. Mpaka hapo nimemvulia kofia sijui anataka kusema nini sasa,” alisema kwa sauti ya kukata tamaa.


Unaweza kufuatilia hadithi hii kupitia tovuti ya Mwananchi, pia Mwananchi Digital katika Mtandao wa Youtube.


Itaendelea Ijumaa