Prime
MWIBA MDOGO-8
ILIPOISHIA JANA...
“Ndiyo, wakati naandaa maziwa jikoni alikuja na kunieleza kikombe hiki nimpe baba na hiki nikupe wewe.”
ENDELEA...
“Kwa nini hukukataa au kumwambia baba?”
“Alinieleza kuwa nikienda kinyume ananiua na bastola alinionyesha, baada ya kuacha vinywaji nilirudi jikoni lakini sikumkuta. Nilipotaka kumwambia baba nilikuta tayari amekunywa nusu kikombe basi nikaishia kumuomba Mungu lisitokee jambo baya.
“Lakini kumbe nilikuwa nimechelewa, masikini nimemuua baba kwa mikono yangu mwenyewe bila kujua.”
“Aliweka nini kwenye kikombe?”
“Kwa kweli sikumuona akiweka kitu zaidi ya kukishika na kusema nimpe baba.”
“Basi pole, hukujua lazima tutamtia nguvuni muuaji,” Mkuu Shila alisema huku hali yake ikiwa mbaya sana na hofu kumtawala pamoja na ulinzi wote lakini muuaji amefanikiwa kuitimiza azma yake mbele yake.
Alimtuma kijana wake kufuatilia sumu iliyowaua ambayo inafanana na vifo vyote vilivyotangulia, tofauti ni kifo cha Balize aliyeuawa kwa kuchomwa na visu vingi mwilini.
Kauli ya marehemu Joseph ilizidi kumchanganya Shila, alijiuliza hiyo kafara ya damu na vifo vinavyoendelea mjini vinashabihiana vipi. Aliamini kama Joseph asingekunywa kahawa angepata mengi kutoka kwake ambayo yangempa picha kamili ya mauaji yale.
Siku mbili zilikuwa kama miaka kumi, zilikuwa ngumu sana kwa mpelelezi mkuu Shila baada ya vifo vinne mfululizo vilivyopangiliwa kwa ukamilifu wa hali ya juu.
Kwa siku mbili alipoteza watu wanne, tena vizito wa nchi, alirudi ofisini akiwa amechoka, akiamini muuaji hakuwa mmoja, bali kundi la watu waliojipanga kikamilifu wenye uwezo wa kijasusi ambao hutumia sauti ya kike kama muuaji.
Kwa mara ya kwanza aliamini kwa vijana wake waliobakia ngoma ile ilikuwa nzito kwao, alifikiri kuwarudisha kina Maliki ili kuongeza nguvu kuweza kumkamata muuaji. Wakati akiwa katikati ya mazungumzo simu iliita. Ilikuwa ya muuaji, aliipokea kwa kuhofia naye kugeuziwa kibao.
“Haloo.”
“Baba.”
“Naam.”
“Najua inaonekana kama nakufundisha kazi la hasha, vyote ninavyovifanya havifiki hata robo ya mateso na maumivu waliyoyapata wazazi wangu kabla ya kufa. Nina hofu na Mungu lakini bila hivyo ningewakatakata viungo vyao wakiwa hai na kuwachemsha supu.
“Maumivu yangu hata kama ningeua dunia nzima bado moto ulio moyoni mwangu hauwezi kuzimika hata umwagiwe maji ya bahari, maziwa, mito na chemchemi zote duniani hauwezi kuzimika.
“Ndiyo maana sitaki kuua wengi kwa ajili ya wachache, kila aliyehusika lazima afe hakuna wa kunizuia, najua nguvu yako yote utaihamishia Mwanza kwa vile Maliki na Queen wapo Geita, waache wafanye kazi uliyowatuma, kwangu watapoteza muda kwa vile lazima nitimize hesabu yangu, hata mkinikamata nitatoka na kumalizia hesabu zangu.
“Sikupenda uone mateso mazito aliyoyapata shetani Joseph kabla ya kifo, nimefanya hivyo ujue uwezo wangu jinsi gani nimejipanga. Katika watu wote watano kama kuna mmoja angekufa bila kupitia mkono wangu basi ningemfukua na kumuua mara ya pili ili moyo wangu uridhike kuwa nimekamilisha hesabu.”
“Duh! Ni hasira gani binti, kwa nini hukuwasamehe na kumuachia Mungu.”
“Ni kweli kuna usemi unasema samehe saba mara sabini, pia kuna usemi mwingine unasema kisasi ni haki lakini Mungu anampenda sana anayesamehe. Ningesamehe ningekufa kwa maumivu ya moyo pengine ningekufa kwa sonona. Baada ya dhuluma ya pesa hawakuridhika wakadhulumu uhai wa wazazi wangu ambao nilikuwa nawapenda sana.
“Mama kabla ya kufa alisema nilipe kisasi chao ili wapumzike kwa amani kaburini.
Hivyo basi sitaacha hata unywele wa waliohusika. Nimebakiza kazi moja ya kumuua Mabula kisha nitajisalimisha kwenu.”
“Kwa nini Mabula tusimfikishe mahakamani ili upate haki yako.”“Hakuna haki kati ya masikini kwa tajiri, siku zote masikini hana haki, huenda akatendewa bado pesa yake ikakufunga au ukanyongwa. Unafikiri wote waliofungwa wametenda kosa, wapo waliotendwa na mateso juu, hivyo malizana na mshambuliaji wako nje ya kumi na nane akiingia ndani atapewa tuta.” “Nitakupigania utashinda.”. “Nimeua unajua kisha nishinde kesi isiyo na ushahidi wakati muuaji unayemtafuta unanijua.”
“Basi nakuomba usimuue Mabula.”
“Usipoteze nguvu zako Mabula lazima afe hata akimficha chini ya ardhi nitamfukua na nitamuua kwa mikono yangu.”
“Mmh! Kazi ipo.”
“Wala siyo kazi wanachokipata ni haki yao, siku zote mwenye kiranga haliliwi wala hawekewi matanga. Usisumbuke kuwawekea matanga, hiki baba ni kiranga komo, nikutakie kazi njema.”
“Samahani, hivi wewe ni nani ambaye unajua mipango yangu.”
“Baba kuwa na subira ni hatua moja kufika ofisini kwako kuujua ukweli ambao hakuna yeyote angeusema bali mimi mwenyewe.”
Mkuu Shila baada ya kuachana na mtoto wa marehemu alitulia ofisini kwake, aliomba msaada kwa vijana wake kina Maliki waliokuwa Geita kufuatilia kutekwa kwa mwanamke albino ambako walielezwa huenda yupo huko na kutakiwa kuhakikisha kazi inafanyika kwa saa ishirini na nne jibu liwe limepatikana. (Jiandae kusoma mkasa wa kukata na shoka wa MSAKO WA NYANI)
Kwanza aliwasiliana na Seba Mabula Shibandiko ambaye alikuwa akimiliki boti za uvuvi, viwanda vya samaki kanda ya ziwa. Pia alikuwa mkulima mkubwa wa mahindi na mpunga na pale Mwanza alikuwa akimiliki hoteli za nyota tano zaidi ya saba na mabasi zaidi ya hamsini yaliyandikwa SHIBANDIKO CLASSIC yaliyokuwa yakienda mikoa yote tu.”
Itaendelea kesho...
Sasa unaweza kusoma hadithi hii kwenye Tovuti ya Mwananchi au kusikiliza kupitia Youtube ya Mwananchi Digital.